Sera ya Ugatuaji wa Madaraka Imekwama Wapi- Waziri Jafo | ZamotoHabari.

Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI
Kutokuwepo kwa Sera ya Ugatuaji Madaraka iliyojengwa kwenye mfumo wa Sheria ni moja ya changamoto iliyofanya Serikali kufanya mapitio ya sera hiyo.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo(Mb) wakati wa kufungua kikoa kazi kilichokutanisha Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa kutoka Mikoa yote 26 kwa ajili ya kutoa maoni na mapendekezo kwenye Rasimu ya Sera ya Taifa ya Ugatuaji Madaraka ya 2019.
Alisema kuwa changamoto moja wapo ni kutokuwepo kwa sera ya ugatuaji iliyojengwa kwenye mfumo wa kisheria inayoelekeza mipaka, majukumu na utaratibu wa utekelezaji wake, jambo ambalo linafanya ionekane kama ni hiari na utashi (Voluntary and Willingness).
Jafo alisema changamoto nyingine ni kuwepo kwa mitazamo inayokinzana kati ya watendaji na viongozi wa kisiasa katika ngazi ya vijiji, kata na halmashauri katika kuweka vipaumbele na kutekeleza miradi ya maendeleo
Aliongeza kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa zimekuwa zikitegemea fedha kwa kiasi kikubwa kutoka Serikali kuu na kutolea mfano kwa mwaka 2018 zilitegemea zaidi ya asilimia 88 ya mapato.
“ Wizara za Kisekta kuandaa sera na sheria na kupeleka halmashauri kwa ajili ya utekelezaji bila kuambatanisha rasilimali fedha, vifaa na watu.”
Waziri Jafo alibainisha kuwa uelewa mdogo wa dhana ya Ugatuaji wa Madaraka (D by D)  kwa baadhi ya Wizara za Kisekta na hivyo Sera hii kuonekana kama ni suala ya OR-TAMISEMI  kwa kiasi kikubwa imechangia kufanya Sera hii kutotekelezeka kwa kiwango kilichotegemewa.
Jafo aliongeza: “Kwa ujumla hatujafikia kiwango cha mafanikio kilichotarajiwa kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeaza na ndio maana Serikali imeamua kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Ugatuaji ili kupata suluhisho la changamoto zilizojitokea.
Aidha, Jafo amewataka wakuu wa mikoa na makatibu tawala kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika kutoa maoni na mapendekezo hayo ili kuboresha rasimu hiyo kwa maslahi mapana ya wananchi, wadau na taifa kwa ujumla.
Aidha  Jafo alitumia fursa hiyo kuwahimiza wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa kuhakikisha wanasimamia kwa ukabilifu fedha na utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwamo ujenzi wa vituo vya afya, ujenzi wa hospitali za wilata, ujenzi wa mabweni, madarasa, vyoo katika shule za msingi na sekondari ambayo tayari fedha zake zimeshatolewa na serikali.
Naye Mwenyekiti wa wakuu wa mkoa ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Eng. Evarist Ndikilo aliahidi kushiriki mzuri wa wawakuu hao kwa kuwa wao ndio wanaotoka kwa wananchi.
Pia alimhakikishia Waziri Jafo kuwa watasimamia kwa umakini  utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuwa itakamilika katika muda uliopangwa na kwa ubora unaotakiwa.
Naye Mwakilishi wa UNICEF, Pius Chaya alisema agenda ya mapitio ya Sera ya Taifa ya Ugatuaji Madaraka imekuja wakati muafaka, kwasababu Serikali inatakiwa kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma wanazostahili na ambazo zinawafikia kwa wakati.
Aidha, Chaya alisema wadau wa maendeo ambao pia wameshiriki katika machakto wa mapitio ya sera hiyo wameahidi kuendelea kushirikiana na serikali ya awamu ya tano katika kuwaletea wananchi wake maendeleo
Sera ya Ugatuaji wa Madaraka  ni dhana ya Kupeleka Madaraka, Majukumu na Rasilimali kutoka Serikali Kuu kwenda kwa Wananchi kupitia vyombo vya kidemokrasia na Kisiasa ambavyo, wajumbe wake huchaguliwa na kuwajibika kwa Wananchi na vimepewa Mamlaka ya kutoa Maamuzi na kusimamia rasilimali (yaani vina uhuru, vinajitawala, na vina hadhi ya kisheria).
Sera hii ilianza kutekelezwa mwaka 1998 kupitia mpango wa maboresho ya Serikali za Mitaa ikiwa na lengo la kuwawezesha wananchi kushiriki shughuli za Maendeleo katika maeneo yao na kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa shughuli za Serikali.
 Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI  Selemani Jafo akifungua  kikao cha  Wakuu wa Mikoa  na Makatibu Tawala wa Mikoa  cha kupitia rasimu ya Sera ya Taifa ya Ugatuaji wa Madaraka kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa St. Gasper Jijini Dodoma.
 Katibu Mkuu OR-TAMISEMI Mhandisi Joseph Nyamhanga akitoa taarifa ya utangulizi kwenye ufunguzi wa kikao cha Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa cha kupitia rasimu ya Sera ya Taifa ya ugatuaji wa madaraka kilichofanyika katika ukumbi wa St. Gasper Jijini Dodoma.
 Baadhi wa Wakuu wa Mikoa wakimsikiliza Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI  Seleman Jafo wakati akifungua  kikao cha kupitia rasimu ya Sera ya Taifa ya Ugatuaji wa Madaraka kilichofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa St. Gasper Jijini Dodoma.
 Baadhi wa Makatibu Tawala wa Mikoa  wakimsikiliza Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI  Seleman Jafo wakati akifungua  kikao cha kupitia rasimu ya Sera ya Taifa ya Ugatuaji wa Madaraka kilichofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa St. Gasper Jijini Dodoma.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Selemani Jafo (watatu kutoka kushoto aliyekaa) akiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa Mikoa mara baada ya kufungua Kikao cha kupitia Sera ya Taifa ya Ugatuaji wa Madaraka kilichofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa St. Gasper Jijini Dodoma.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa  Selemani Jafo (watatu kutoka kushoto aliyekaa) akiwa katika picha ya pamoja na Makatibu Tawala mara baada ya kufungua Kikao cha kupitia Sera ya Taifa ya Ugatuaji wa Madaraka kilichofanyika leo katika ukumbi wa mikutano wa St. Gasper Jijini Dodoma.



Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini