Na Woinde Shizza Michuzi TV, Monduli.
SERIKALI ya Ujerumani kupitia Balozi wake nchini Tanzania Dkt Detlef Waechter imekabidhi funguo za Hospitali ya Kanda ya Jeshi iliyopo katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli wilayani humo iliyogharimu kiasi cha shilingi Bilioni 5.6.
Akikabidhi funguo kama ishara ya ufunguzi na makabidhiano kwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa Balozi Dkt Waechter alisema kuwa hospitali hiyo ni moja ya mkataba kati ya Wizara ya Ulinzi nchini Ujerumani na Wizara ya Ulinzi nchini Tanzania kupitia sekta ya afya huku akiahidi kuendelea kufadhili katika miradi ya serikali ya Tanzania.
"Mradi huu ulianza 2017 ulitakiwa kuisha mwaka 2020 lakini tumeongeza muda wa mradi hadi 2024 ili kuendelea kusaidia serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Ulinzi"alisema Balozi huyo.
Kwa upande wake Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa Dkt Hussein Mwinyi aliiomba Serikali ya Ujerumani kuendelea kutoa msaada kwakuwa hospitali za Kanda hazihudumii wanajeshi pekee bali zinasaidia wananchi kwa asilimia 80 huku wanajeshi asilimia 20.
"Wenzetu wa Ujerumani wametusaidia sana walitusaidia katika ujenzi wa chuo cha wataalam wa tiba,vifaa na maabara na niwashukuru kwa kuongeza muda wa mradi.....
"Lakini Hospitali hii ina vifaa bora na vya kisasa pengine kuliko hata hospitali nyingine na itasaidia kupunguza idadi ya wagonjwa waliokuwa wakienda nje kutibiwa" alisema Waziri Mwinyi.
Naye Mkuu wa Majeshi nchini Generali Venance Mabeyo alisema kuwa hadi kukamilika kwa ujenzi wa hospitali hiyo kumeghalimu kiasi cha shilingi Bilioni 5.6 ambapo Bilioni 2.8 zilitumika kwa ajili ya vifaa tiba na Bilioni 2.8 kwa ajili ya miundombinu kwa ufadhili wa serikali ya Ujerumani.
"Aidha pia mbali na hii Walijenga chuo cha Tiba Dar es salaam, Mbeya, Mwanza na hapa na zote ni za viwango vya juu" alisema Generali Mabeyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Tawi la Tiba wa Jeshi la Wananchi Tanzania Meja Jenerali Denis Janga alibainisha matibabu yataanza mapema ambapo kutakuwa na wataalam wa Idara zote ikiwemo Meno,Uzazi na picha(Xray) huku akibainisha kuwa hospitali hii ina uwezo wa kulaza wagonjwa 50 kwa siku na kuhudumia wagonjwa wa nje 300 kwa siku.
balozi wa Ujerumani nchini Tanzania pamoja na waziri wa ulinzi na jeshi la kujenga taifa akikata utepe ishara ya kuonyesha hospital hii ipo tayari kutumika
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa Dkt Hussein Mwinyi akionyeshwa moja ya chumba kwa ajili ya Upasuaji
Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Dkt Detlef Waechter akimkabidhi funguo za Hospitali ya Kanda ya Jeshi Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa Dkt Hussein Mwinyi .
waziri wa ulinzi na jeshii la wananchi wa Tanzania pamoja na Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania akiwa pamoja na maofisa mbalimbali wa jeshi hilo pamoja na ujerumani.
Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO
0 Comments