Serikali yatekeleza ahadi ya kupeleka umeme kwa wachimbaji wadogo Nyakafuru | ZamotoHabari.

Na Teresia Mhagama, Geita
Wizara ya Nishati kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) imetekeleza ahadi ya kupeleka umeme kwenye migodi ya wachimbaji wadogo katika Kijiji cha Nyakafuru wilayani Mbogwe hivyo kuwawezesha wachimbaji hao kutumia umeme badala ya mafuta katika kuendesha mitambo mbalimbali ikiwemo ya kuchenjulia madini.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani aliwasha umeme katika katika eneo hilo la wachimbaji wadogo tarehe 12 Mei, 2019 ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa mwezi Februari  mwaka huu wakati alipotembelea machimbo hayo na wachimbaji wadogo wa eneo hilo kumlalamikia kuhusu gharama kubwa wanazotumia katika ununuzi wa mafuta ambazo zinafikia hadi shilingi milioni Tatu kwa mwezi.

" Serikali inatekeleza ahadi zake badala ya kupiga maneno, hivyo tumeleta umeme hapa si kwa ajili ya kuwasha taa tu, bali umeme huu utawawezesha kuchimba kwa tija, Serikali inataka mchimbe kwa faida ili nanyi muweze kulipa kodi stahiki serikalini itakayotumika kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo." alisema Dkt. Kalemani.

Alisema kuwa, katika eneo hilo tayari imeshafungwa transfoma moja kubwa yenye uwezo wa kVA 315 na kwamba zitafungwa transfoma nyingine Tatu zenye uwezo wa kVA 315 ili kuwezesha eneo hilo kupata umeme wa uhakika utakaotosheleza mahitaji.

Pamoja na kuipongeza TANESCO kwa utekelezaji wa agizo hilo, Dkt. Kalemani alitoa agizo kwa watendaji wa TANESCO kuhakikisha kuwa hadi ifikapo mwisho wa mwezi wa Tano wawe tayari wameshafunga transfoma tatu na moja iliyosalia ifungwe mwezi Juni.

Aidha, Dkt Kalemani aliwaasa wachimbaji hao kuchangamkia fursa ya uuganishaji umeme  kwa bei ya REA inayoanzia 27,000 na  pia aliagiza TANESCO kupeleka umeme huo katika vitongoji vyote vya Kijiji hicho.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wachimbaji wa Nyakafuru, Walwa Katemi Walwa aliishukuru Serikali kwa kupeleka umeme katika eneo hilo ambalo lina wachimbaji zaidi ya 3000 na kuahidi kulipa kodi stahiki serikali.

Alisema kuwa wakati wakitumia mafuta kuendeshea mitambo katika eneo hilo walikuwa wakilipa kodi zaidi ya shilingi milioni 400 hivyo sasa wanaamini kuwa kodi hiyo itaongezeka maradufu kwani gharama za uendeshaji zitapungua na pia wataongeza uzalishaji kwa kuwa kuna uhakika wa nishati ya kuendeshea mitambo yao. 
 Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, akizungumza na wachimbaji wadogo katika Kijiji cha Nyakafuru wilayani Mbogwe mkoani Geita wakati alipofika kuwasha umeme katika eneo la wachimbaji wadogo kijijini hapo.
 Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani akiwasha rasmi umeme katika migodi ya wachimbaji wadogo iliyo katika Kijiji cha Nyakafuru wilayani Mbogwe mkoani Geita. Wengine katika picha ni watendaji kutoka Wizara ya Nishati, TANESCO na viongozi wa wachimbaji wadogo katika eneo hilo.
 Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani akikata utepe kuashiria kuwasha rasmi umeme katika migodi ya wachimbaji wadogo iliyo katika Kijiji cha Nyakafuru wilayani Mbogwe mkoa wa Geita. Wengine katika picha ni watendaji kutoka Wizara ya Nishati, TANESCO na viongozi wa wachimbaji wadogo katika eneo hilo.
 Wachimbaji wadogo katika Kijiji cha Nyakafuru wilayani Mbogwe wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani) wakati alipofika kuwasha umeme kwenye eneo la wachimbaji wadogo kijijini hapo.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (wa kwanza kushoto) akifurahi na wachimbaji wadogo mara baada ya kuwasha rasmi umeme katika migodi ya wachimbaji wadogo katika Kijiji cha Nyakafuru wilayani Mbogwe mkoani Geita.


Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini