Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu leo amewasilisha makadirio ya Bajeti ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2019/20 kwa kutaja majukumu ya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii na kuongeza kuwa Idara hiyo itatumia kiasi cha takribani bil. 415 ili iweze kutekeleza majukumu yake ikiwemo matumizi ya kawaida na mishahara.
Waziri Ummy amevitaja vipaumbele vya idara hiyo pamoja na majukumu ya utekelezaji wa Idara Kuu Maendeleo ya Jamii kuwa ni Kuamsha Ari ya Wananchi Kushiriki katika Shughuli za Kuleta Maendeleo Wizara yake iliratibu ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo ili kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kutumia nguvukazi pamoja na rasilimali zinazowazunguka.
Waziri Ummy ameitaja miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa skimu ya umwagiliaji katika Wilaya ya Mvomero Mkoa wa Morogoro, ujenzi wa Shule Shikizi katika Wilaya ya Kibiti Mkoa wa Pwani kwa ajili ya watoto wadogo wasioweza kutembea umbali mrefu wa zaidi ya kilometa 5 kufuata shule ilipo.
Mengineyo ni ujenzi wa bweni la wasichana katika Shule ya Sekondari Kirare Tanga Jiji, ujenzi wa bweni katika Shule ya Sekondari ya Mikaranga mkoa wa Ruvuma, ujenzi wa zahanati katika Kijiji cha Mhagawa Asili, Wilayani Mbinga katika Mkoa wa Ruvuma pamoja na ujenzi wa wodi ya mama na mtoto kwenye Kituo cha Afya Kaloleni Arusha Jiji mkoani Arusha.
Aidha Waziri ameongeza kuwa kwa kushirikiana na wadau Wizara yake imeendelea kuhakikisha uwepo wa haki za mtoto za kuishi,kuendelezwa, kushiriki, kulindwa na kutobaguliwa katika jamii akiongeza kuwa Mwezi Desemba, 2018, Wizara kwa kushirikiana na wadau iliwezesha kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa Baraza la Watoto la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha Waziri Ummy ameongeza kuwa hadi Machi, 2019, ushiriki wa watoto katika ajenda ya maendeleo ulifanyika kupitia mabaraza ya watoto 1,669 yaliyopo katika ngazi ya Taifa, Mikoa, Halmashauri, Kata na Vijiji/Vitongoji na klabu za watoto 2,475 zilizoanzishwa katika shule za msingi na sekondari.
Kuhusu usawa wa Kijinsia Waziri ummy ameliambia Bunge kuwa Wizara yake imeandelea kukuza Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi ambapo uwezeshaji wanawake kiuchumi ni suala muhimu katika kufikia usawa wa kijinsia na kupunguza umaskini wa kipato katika jamii.
Aidha ameliambia Bunge katika hotuba yake kuwa Wizara yake imeendelea kusimamia Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ili yachangie katikakuleta maendeleo kwa Taifa. Katika kipindi cha mwaka 2018 hadi Machi, 2019, jumla ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali 617 yamesajiliwa na kupatiwa cheti cha usajili ikilinganishwa na mashirika 385 yaliyosajiliwa mwaka 2017 sawa na ongezeko la asilimia 60.
Aidha Waziri Ummy aliongeza kuwa kati ya mashirika 617 yaliyosajiliwa, mashirika 44 yamesajiliwa katika ngazi ya Kimataifa, mashirika 551 katika ngazi ya Kitaifa, mashirika 15 ngazi ya Wilaya na mashirika saba katika ngazi ya Mkoa.
Makadirio ya Bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa mwaka wa fedha 2019/20 yanaendelea kujadiliwa Bungeni Jijini Dodoma na yanatarajia kuhitimishwa hapo kesho kwa Bunge kuidhinisha Bajeti ya Wizara hiyo.
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu
Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO
0 Comments