NA YEREMIAS NGERANGERA, NAMTUMBO
Wakulima 69 wa kijiji cha ligera wilayani Namtumbo Mkoani Ruvuma wamepatiwa mafunzo ya siku tatu ya Kupanda mpunga kwa njia ya Mfereji, kutawanya ,kwa njia ya ibaraki na kwa njia ya shimo ili kuwewezesha kupata mavuno ya kutosha.
Mafunzo hayo yalitolewa kwa vitendo na kwa nadharia na wataalamu wa kilimo kutoka chuo cha kilimo MATI Mtwara waliowafundisha wakulima njia za upandaji mpunga wa mabondeni na unaotegemea mvua.
Aidha wataalamu hao ni Doroth Mushi, Daudi Kasabuku na Kenedy Siame wote ni wakufunzi kutoka chuo cha kilimo MATI Mtwara ambao walifundisha namna ya kupanda mpunga aina ya Saro tano,Mtalimawangu na supermbeya.
Hata hivyo waliwafundisha wakulima hao namna sahihi ya kuvuna mpunga uliotayari kuvunwa na namna sahihi ya kuuhifadhi mpunga huo na kisha namna sahihi ya kukoboa mpunga tayari kwa kupelekwa sokoni.
Mwenyekiti wa kikundi cha wakulima wa mpunga kijiji cha ligera Lukanus Luena alisema watayatumia mafunzo hayo waliyoyapata kuongeza uzalishaji wa mpunga na kujipatia kipato kwa mwanakikundi mmoja mmoja na kikundi pia.
Bwana Luena alidai mafunzo hayo yamewaongezea morali ya kulima zaidi kwa kutumia njia sahihi za kilimo cha kisasa na kuahidi kuongeza wanachama wengine katika kikundi hicho kutokana na hitaji la wakulima wengine ambao wameonesha nia ya kujiunga na kikundi hicho cha wakulima wa mpunga.
Ofisa kilimo anayeshughulikia umwagiliaji Bwana Eleuter Mndendemi aliwataka wakulima wa kijiji cha Ligera kuyatumia mafunzo hayo vyema kwa kuonesha matokeo chanya y a mapato yanayoshabahiana na wakulima wanaolima kwa kitaalamu na kuonesha utofauti na awali kabla ya kupatiwa mafunzo hayo.
Mafunzo ya kilimo cha mpunga wa Mabondeni ( kutegemea maji ya Mvua) unafadhiliwa na JICA(Japan International Cooperation Agency) kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo pamoja na chuo cha Kilimo MATI-Mtwara.
Kikundi cha wakulima wa Mpunga wa kijiji cha Ligera kilianzishwa mwaka 2017 kikiwa na wanachama 30 na mwaka huu 2019 kikundi kina wanakikundi 80 na kati ya hao waliopatiwa mafunzo ni 69 ikiwa wanawake 29 na wanaume 40.
Mtaalamu wa kilimo Kenedy Siame (mwenye kofia nyekundu) akiwaelekeza wakulima umuhimu wa kuzingatia vipimo wakati wa upandaji wa mpunga,Picha ya pili wakulima wakiwa katika mafunzo kwa vitendo namna ya kukata mpunga na kuuhifadhi.
Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO
0 Comments