YOULOU MABIALA ALIOA BINTI WA FRANCO MAKIADI | ZamotoHabari

Wapenzi wa muziki wa ‘soukous’ uliokuwa ukitawaliwa na wanamuziki toka nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Kongo Brazzaville, majina ya Youlou Mabiala hayawezi kuwa mageni kwao.

Mabiala ni mwanamuziki aliye na vipaji vya kutunga na kuimba, aliyepiga muziki kati ya miaka ya 1960 hadi 2008.

Majina yake halisi ni Gilbert Youlou Mabiala, alizaliwa Machi 03, 1947 katika kitongoji cha Linzolo, jirani na Brazzaville, ambao ndio mji mkuu wa nchi ya Jamhuri ya Kongo.

Msomaji wa makala hii, nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Jamhuri ya Kongo ni nchi mbili tofauti. Sehemu kubwa nchi hizo zimetengenishwa na mto Kongo.

Anajulikana sana kwa jina bandia ‘Prince Youlou’, alianza muziki kwenye bendi za mitaani katika jiji la Brazzaville, nchini Jamhuri ya Kongo.

Youlou mwaka 1963, alijiunga katika bendi ya T.P.OK Jazz, katika jiji la Kinshasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), akiwa kama mtunzi na mwimbaji. Bendi ya T.P.OK. Jazz, ilikuwa ikiongoza katika muziki wa Wakongo kwenye miaka ya 1960 hadi ya 1980.

Baadhi ya nyimbo alizotunga au kushiriki kuimba akiwa katika bendi ya T.P.OK. Jazz ni Télé Zaire ya mwaka 1975, Siddikh, Aboubacar za mwaka 2008 , "Asumani” , Ngaira na Amos.

Mwaka 1972, Youlou alikuwa mmoja kati ya wanamziki walioondoka katika bendi ya T.P.OK. Jazz, wakaenda kuunda bendi iliyoitwa Lovy du Zaïre, iliyoongozwa na Vicky Longomba.

Kwa taarifa yako mpenzi msomaji wa makala haya, Vicky Longomba ndiye aliyekuwa baba wa wanamuziki mashuhuri Awillo na Lovy Longomba.
Katika harakati za kutafuta maisha, Youlou baadaye aliiacha bendi hiyo, akaenda kuunda bendi ya Orchestra Somo Somo.

Aliwakusanya wanamuziki wengine akina Jean Kwamy Munsi, Diatho Lukoki, Master Mwana Congo na Nona Simon.

Kama wasemavyo Waswahili kuwa “ Ngoma ya watoto haikeshi” Mabiala mwaka 1975, aliamua kuondoka katika bendi aliyoianzisha na kurudi kwa gwiji la muziki Franco Luambo Makiadi aliyekuwa kiongozi wa bendi ya T.P.OK. Jazz.

Katika bendi hiyo aliachia kibao ‘matata’ sana cha ‘Kamikaze’ ambacho kilikuja kuwa maarufu sehemu nyingi Afrika na kwa baadhi ya Waafrika waishio nchi za Ulaya na Marekani ya Kaskazini.

Mabiala aliimba nyimbo nyingine za Ledi, Massi na Lekwey alioutunga akiwa pamoja na Franco Makiadi.Baada ya kuchota ‘maujuzi’ zaidi toka katika bendi ya T.P.OK. Jazz, mwaka 1977, Youlou aliondoka katika bendi hiyo jumla.

Akaenda kuunda bendi iliyopewa jina la Trois Frères akiwa na wanamuziki akina Loko Massengo, Mose Fan Fan, Michel Boyibanda na wengine wengi, wakipiga muziki hususani katika jiji la Brazzaville.

Watanzania watalikumbuka jina la Mose Fan Fan, aliyewahi kuishi humu nchini akipiga gitaa la solo katika bendi za Orchestra Makassy na Orchestra Matimila.Mnamo miaka ya 1980, Youlou aliimba katika bendi ya Kamikaze Loningisa, ambako alitunga na kuimba wimbo wa Djeliba na zingine.

Akitoa burudani za muziki katika sherehe za maadhimisho ya Uhuru wa nchi ya Kongo Brazzaville Agosti 15 2004, zilizofanyika hoteli ya Présidence de la République huko Pointe Noire, Youlou Mabiala alipatwa na ugonjwa kiharusi.Baada ya kupatiwa kuhuduma na kupata nafuu, katika hospitali ya jijini Brazzaville, alisafirishwa kwa ndege kupelekwa Paris, nchini Ufaransa kwa matibabu zaidi.

Hata baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini, alibakia katika nchini Ufaransa kwa ajili ya kujiimarisha kiafya.Youlou Mabiala baba wa familia aliye na mke. Mke huyo ni mmoja kati ya mabinti wa aliyekuwa ‘bosi’ wake Franco Luambo Makiadi.

Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini