Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Shaaban Seif Mohamed Kulia na Mhadhiri Muandamizi wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar {SUZA} Dd. Zakia Mohamed Abubakar wakitia saini Mkataba wa kufanya Utafiti kugundua sababu zinazopelekea Zanzibar kuathiriwa na tatizo la mmongo’nyoko unaopelekea kudidimia kwa ardhi. Wa kwanza kulia aliyefika kushuhudia utiaji saini Mkataba huo ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Mohamed Aboud Mohamed.
Baadhi ya Wakurugenzi wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nchi Ofisdi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Mohamed Aboud Mohamed akizungumza mara baada ya kumalizika kwa utiaji saini Mkataba huo.
Mhadhiri Muandamizi wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar {SUZA} Dd. Zakia Mohamed Abubakar akielezea faraja yake kutokana na Serikali Kuu kuwaamini kuwapa fursa ya kutumia ujuzi wao katika masuala ya utafiti. Picha na – OMPR – ZNZ.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetiliana saini Mkataba na Wataalamu wa chuo kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) ili kufanya tafiti kugundua sababu zinazopelekea Zanzibar kuathiriwa na tatizo la mmongo’nyoko unaopelekea kudidimia kwa ardhi katika baadhi ya maeneo hasa wakati wa kipindi cha mvua kubwa zinaponyesha.
Utafifiti huo utakwenda sambamba na kuchunguza mbinu mbadala zinazoweza kutumika katika kuondosha takataka zitokanazo na mali ghafi za platiki ambazo zimekua chanzo kikubwa cha uchafuzi wa mazingira kwa muda mrefu ndani ya Zanzibar hali inayosababisha athari juu ya mripuko wa maradhi katika jamii.
Mkataba huo umetiwa Saini na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Shaaban Seif Mohamed kwa upande wa Serikali na Uongozi wa Chuo Kikuu ca Taifa Zanzibar ukatiwa na Mhadhiri Muandamizi wake Dr. Zakia Mohamed Abubakar.
Akizungumza mara baada ya utiaji saini huo katika ukumbi wa Kamati ya Sheria Baraza la wawakilishi Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mhe. Mohamed Aboud Mohamed alisema kitendo hicho kinachofanywa na Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar kitakuwa cha kihistoria ambacho matokeo yake yatavinufaisha vizazi vya sasa na vile vijavyo.
Waziri Aboud alisema ni kipindi cha muda mrefu sasa Zanzibar imekuwa ikikumbwa na tatizo la kudidimia kwa Aridhi katika maeneo mbali mbali ya unguja hasa inapowadia kipindi cha mvua kubwa hali inayozusha hofu kwa jamii na wakaazi wanaoishi katika maeneo yanayokubwa na kadhia hiyo.
“Kumekuwepo na tatizo katika visiwa vyetu hivi kila mvua kubwa zinaponyesha basi baadhi ya maeneo hudidimia na kutoa taharuki kwa serikali pamoja na wakaazi wa maeneo hayo” Alisema Mhe. Aboud
Sambamba na hayo alisema kutiwa saini kwa mkataba wa kufanyika utafiti kumempa imani na furaha kubwa kwani kitendo hicho kinaashiria kulipatia ufumbuzi tatizo ambalo wananchi wamekua wakipatwa na wasi wasi yanapotokea akitolea mfano kutokea kwa kudidimia kwa aridhi katika eneo la Jango’ombe mshelishelini, Kwerekwe “C” Mombasa na Tukio la juzi pembezoni mwa Madrasa Ismailia na Msikiti wa Mwanakwerekwe.
Akilitolea ufafanuzi tatizo la takataka pamoja na pemapasi Waziri Aboud alisema watafiti hao wana kazi ya kulichunguza kwa kina jambo ili kuja na suluhisho la kudumu juu ya mbinu mbadala zinazoweza kutumika ili jamii iondokane na kadhia hiyo huku akiwa na imani kwamba watafiti hao wataifanya kazi yao kwa ufasaha wa hali ya juu.
Nae Muhadhiri muandamizi kutoka chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar {SUZA} Dk. Zakia Mohamed Abubakar alisema watafiti kutoka chuoni hapo wanaishukuru serikali ya mapInduzi Zanzibar kwa kuwapa imani kubwa Ya kuwapatia kazi ya kufanya tafiti mbili ile ya kudiDImia kwa ardhi na tatizo la taka za plastiki na Pempasi na kuahidi kuwa wataifanya kazi hiyo kwa uweledi mkubwa katika kutokomeza tatizo hilo.
Dk. Zakia alisema timu ya watalamu hao itafanya kazi kwa ustadi ili kubaini kiini halisi cha tatizo hilo ili iwe rahisi kutoa maelekezo kwa wananchi juu ya sababu zinazopelekea kutokea kwa matukio hayo.
Aidha alisema jamii inapaswa kuondosha hofu juu ya matukio hayo kwani baadhi ya wakati hali hiyo inaweza kusababishwa na aina ya udogo au kutembea kwa udongo chini ya ardhi.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Ndu. Abdalla Hassan Mitawi alisema serikali imeamua kufanya tafiti hizo kusudi kubaini chanzo cha tatizo na alieleza kuwa matukio ya utafiti huo yatakapowasilishwa itaisaidia serikali kufahamu hatua za kuchukua kwa lengo la kupunguza athari hizo kwa wananchi wake.
Naibu katibu Mitawi Alisema matukio ya tafiti kwa upande wa matumizi ya plastiki na pempasi yataiwezesha serikali kubuni njia mbadala za kutumia ili kuviepushia visiwa vya Zanzibar kukumbwa na athari zinazoweza kuepukika.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa utafifiti na shahada za juu Dk. Makame Omar Makame alifafanua kuwa timu ya watalamu hao itajitahidi kuzifanya tafiti hizo kwa umahiri ili ije maelezo sahihi ndani ya kipindi cha muda mfupi kutokana na tatizo la taka za plastiki na pempasi kuzagaa kwa wingi mitaani hali inayosababisha kipindi cha mvua kubwa maji kutuwana na kuleta athari katika sehemu za makaazi ya wananchi.
Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO
0 Comments