Naibu Waziri wa Afya, Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile ametoa rai kwa Wizara yake na TAMISEMI kutoa elimu kwa Jamii hususani kuhusu mirathi na uandishi wa wosia ili jamii iweze kutambua umuhimu wa mirathi na wosia na kuondokana na migogoro mingi inayowakumba wajane Nchini.
Naibu Waziri Ndugulile ameyasema hayo leo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wajane Duniani yaliyofanyika Kitaifa leo Jijini Dodoma na kusisitiza kuwa elimu ya mirathi na uandishi wa wosia ni muhimu kwa sababu idadi kubwa ya watu bado haijui haki zake.
Aidha Dkt. Ndugulile amewataka wanandoa kote Nchini kuhakikisha wanasajili ndoa zao ili wajane na watoto waweze kupata haki zao lakini pia akawataka wananchi kuiga mfano wa Nchi za Ulaya ambapo kabla ya kufunga ndoa kila mmoja utaja mali zake ili zisiwe sehemu ya mirathi inapotokea kuna kufarakana au mmoja kufariki.
Dkt. Ndugulile ameonya kuwa maandalizi ya mirathi na wosia yaanze sasa bila kusubiri vifo na kuwataka watu kufahamu kuwa mtu kuwa mjane sio mwisho wa maisha bali watambue kuwa mwenzako anapoondoka maisha yanapaswa kusonga mbele.
Aidha Naibu Waziri Ndugulile amewataka wadau wote Nchini kukutana na Wizara yake ili kupitia Sera ya Taifa ya maendeleo ya Wanawake na Jinsia na kuahakikisha masuala yote ya mirathi na ukatili wa kijinsia yanazingatiwa kulingana na wakati huo akiwataka wasanii kutumia sanaa yao kuelimisha umma kuhusu madhira na madhara yawakutayo wajane hao.
Maadhimisho haya yanafanyika Duniani kote kwa lengo la kutoa Msukomo kwa Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za makusudi kutokomeza umasikini na uonevu unaowakabili wajane kote Duniani.
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipo
BOFYA HAPA
0 Comments