MAMENEJA TANESCO TUTAWAPIMA KWA KAZI ZENU – NAIBU WAZIRI MGALU | ZamotoHabari.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, akizungumza na wananchi wa wananchi wa Mtaa wa Vitendo, Kata ya Misugusugu, wilayani Kibaha, Mkoa wa Pwani, kabla ya kuzindua rasmi uwashaji wa umeme katika Mtaa huo, kupitia Mradi wa REA Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Kwanza, Juni 22, 2019. 

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kulia), akiwa amefuatana na Mbunge wa Kibaha Mjini, Silivester Koka (wa pili-kulia), Mtendaji wa Mtaa wa Vitendo wilayani Kibaha, Juma Hamisi (wa pili-kushoto), wataalamu kutoka REA, TANESCO pamoja na wananchi; akiwa katika ziara ya kazi wilayani Kibaha, Mkoa wa Pwani, Juni 22 mwaka huu. 
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, akiwahamasisha wananchi wa Mtaa wa Vitendo, Kata ya Misugusugu, wilayani Kibaha, Mkoa wa Pwani, kutumia kifaa cha Umeme Tayari (UMETA), alipokuwa katika ziara ya kazi na kuwawashia umeme, Juni 22 mwaka huu. 

****************** 



*Na Veronica Simba – Pwani* 

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu ametoa wito kwa Mameneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Ngazi ya Mkoa na Wilaya nchi nzima, kufanya kazi kwa bidii kwani ndicho kigezo kitakachotumiwa kuwapima iwapo wanafaa kuendelea kushikilia nyadhifa hizo. 

Ametoa wito huo leo Juni 22, 2019 wakati akizungumza na wananchi wa Mtaa wa Vitendo, Kata ya Misugusugu, wilayani Kibaha, Mkoa wa Pwani, kabla ya kuzindua rasmi uwashaji wa umeme katika Mtaa huo, kupitia Mradi wa REA Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Kwanza. 

“Meneja wa TANESCO ujisikie aibu kukuta Mtaa una nyumba 300 na hauna umeme; wewe upo tu! Tuwawapima kwa kazi,” alisema Naibu Waziri. 

Akifafanua, Naibu Waziri Mgalu alisema, hakuna mantiki kuwa na Meneja wa Wilaya au Mkoa, ambaye wananchi wa eneo lake wanaomba umeme miaka minne hadi mitano mfululizo wakati yeyé mwenyewe hana andiko wala ubunifu na wala hafuatilii. “Maeneo mengine yasiyo na umeme yanahitaji ubunifu tu wa Meneja.” 

Akizungumzia mikakati ya Serikali kupitia Wizara ya Nishati, kuhusu upatikanaji na usambazaji wa umeme nchini, Naibu Waziri alisema iko miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa, ambayo kukamilika kwake kutawezesha nchi kuwa na umeme mwingi zaidi na wenye uhakika. 

Aliitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni pamoja na wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza, Mradi wa Ujazilizi (Densification) Awamu ya Pili pamoja na ule ujulikanao kama Miji Vijiji (Peri-Urban). 

Kuhusu Mradi wa Miji Vijiji, alisema upo katika hatua za mwisho ambapo mchakato wa zabuni umekamilika, wakandarasi wa kuutekeleza wamepatikana na mikataba imewasilishwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kama taratibu zinavyoelekeza. 

“Tuna matarajio hadi kufikia wiki ya kwanza ya mwezi Julai mwaka huu, mikataba itakuwa imerudi na tutawakabidhi wakandarasi waanze utekelezaji,” alisema. 

Alisema takribani shilingi za kitanzania bilioni 86 zimetengwa kwa ajili ya kuwasambazia wananchi umeme kupitia mradi huo ambao utahusisha maeneo ya Ukonga, Kigamboni, Kibaha na Bagamoyo. 

Vilevile, Naibu Waziri Mgalu alisema kuhusu Mradi wa Ujazilizi Awamu ya Pili, takribani shilingi za kitanzania bilioni 169 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji. 

Akiendelea kubainisha jitihada mbalimbali za kuboresha sekta ya umeme nchini, alisema TANESCO wamebainisha maeneo 754 ambayo yamepitiwa na umeme mkubwa hususan barabarani lakini hayajashushiwa nishati hiyo kwa lengo la kutatua changamoto husika. 

“Tumewapa miezi sita, hadi Desemba 2019 wawe wamekamilisha,” alisisitiza na kuongeza kuwa jumla ya shilingi bilioni 400 zimetengwa kukamilisha kazi hiyo. 

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri aliuagiza uongozi wa TANESCO Mkoa wa Pwani, kuhakikisha wanatimiza pasipo kuchelewa ahadi walizotoa mbele yake, ikiwemo kuziwashia umeme Kaya 10 za Mtaa wa Vitendo, ambazo zimekwishalipia huduma hiyo, ifikapo kesho (Jumapili), Juni 23, mwaka huu. 

Nyingine ni kukamilisha kazi ya makadirio ya gharama za kuunganishiwa umeme kwa Kaya 30 za Mtaa huo, ifikapo Jumanne ijayo, Juni 25 mwaka huu ili Mkandarasi aziwashie umeme siku ya Alhamisi ya Juni 26, 2019. 

Akizungumza katika tukio hilo, Mbunge wa Kibaha Mjini, Silivester Koka, aliwasihi wananchi ambao bado hawajafikiwa na huduma ya umeme kuwa na uvumilivu kwani zoezi la kuunganisha nishati hiyo ni endelevu. 

Naye Kaimu Meneja wa TANESCO, Mkoa wa Pwani, Mhandisi Kenneth Boymanda, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu kwa Ofisi yake katika eneo husika, alimweleza Naibu Waziri kuwa, vitongoji 25 vya Wilaya ya Kibaha vimenufaika kwa kupata Mradi wa umeme wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza. 

Akizungumzia hatua iliyofikiwa katika utekelezaji, alisema Mkandarasi amekwisha washa jumla ya transfoma 24 na kuunganisha wateja wapatao 554. 

Alizitaja Kata zinazonufaika na Mradi huo kuwa ni Gwata, Mlandizi, Kilangalanga, Janga, Kikongo, Kwala, Boko, Kawawa na Soga.


Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini