Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Omary Mgumba akipata amelezo ya ujenzi wa vihenge vya kisasa kwa upande wa ndani kutoka kwa Mhandisi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Makao Makuu Bwana Iman Nzobonaliba kulia kwake na wengine ni Mkurugenzi wa Uhifadhi Bwana Mikalu Mapunda na kushoto kwake ni Mhandisi Mgole Chambili Msimamizi kutoka Kampuni ya Feruum
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Omary Mgumba akipata amelezo ya ujenzi wa vihenge vya kisasa kutoka Mhandisi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Makao Makuu Bwana Iman Nzobonaliba kulia kwake na wengine ni Mtendaji Mkuu wa NFRA Bwana Milton Lupa
Mafunsi wa Kampuni ya Feruum wakiendelea na kazi ya kuunganisha vyuma vya ujenzi wa vihenge vya kisasa eneo la Kizota Jijini Dodoma wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Omary Mgumba alasiri ya leo
…………………………
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Omary Mgumba amesema Serikali ya Tanzania imepokea maombi mapya ya kuuza mahindi kwenda nchini Kenya yenye jumla ya Tani milioni 1.
Mhe. Mgumba ameyasema hayo wakati alipofanya ziara ya gafla kwenye Ofisi za Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA – Makao Makuu) Jijini, Dodoma alipotembelea leo alasiri ili kujionea maendeleo ya ujenzi wa vihenge vya kisasa vya kuhifadhia chakula katika eneo la Kizota, Jijini Dodoma.
Naibu Waziri Mgumba amesema wakati Serikali ikiwa kwenye hatua ya kuiuzia Zimbabwe kiasi cha mahindi Tani laki saba (700,000) na tani laki moja (100,000) kwa mazao mengine ya nafaka, Serikali ya Kenya imewasilisha ombi rasmi la kununua kiasi hicho kutoka Tanzania.
Naibu Waziri Mgumba amesema huu ni wakati muhafaka kwa Wakulima wa Tanzania kuchangamkia fursa ya kuuza chakula cha ziada nje ya nchi na kwa bei nzuri ambayo italeta tija na maendeleo na uchumi wao.
Aidha Mhe. Mgumba alidokeza kuwa amefanya ziara hiyo lengo lake likiwa ni kujionea maendeleo ya ujenzi wa vihenge vya kisasa (Silos) vya kuhifadhia mazao kwa lengo la kuongeza akiba ya taifa ya chakula kwa Kanda ya Kati yenye kuhudumia mikoa ya Dodoma, Singida kutoka uwezo wake wa sasa wa kuhifadhi, tani elfu thelasini na tisa (39,000) hadi kufikia tani elfu hamsini na tisa (59,000).
Mradi wa ujenzi wa vihenge hivyo vya kisasa, ulizinduliwa rasmi tarehe 24 Aprili, 2018 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa na ulianza rasmi Mwezi Juni 2018 huku Kampuni ya Feruum kutoka nchini Poland ndiyo iliyoshinda zabuni ya ujenzi huo.
Akijibu swali la Mhe. Mgumba, Mhandisi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Bwana Iman Nzobonaliba amesema Mradi unataraji kuisha kwa wakati mnamo Mwezi Disemba 2019.
Akijibu swali la Naibu Waziri Mgumba ambaye alitaka kufaham namna Wakala ilivyojianda kununua mazao ya Wakulima katika msimu wa kilimo wa 2019/2020 Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula Bwana Milton Lupa amemwambia Naibu Waziri Mgumba kuwa NFRA imeanza zoezi la kununua chakula cha ziada kutoka kwa Wakulima tangu tarehe 17 Juni 2019 katika Kanda ya Makambako na Sumbawanga na kwamba kiasi cha shilingi bilioni 2.5 kitatumika kwa sasa.
Bwana Lupa amesema NFRA imejipanga kutumia bajeti ya kiasi cha bilioni 15 pamoja na kuomba mkopo kutoka Benki ya Kilimo wenye riba nafuu na kuongeza kuwa zaidi ya shilingi bilioni 62.6 zitatumika kwa ununuzi wa nafaka kwa msimu wa kilimo wa 2019/2020.
Akizungumzia bei ya kununulia mahindi kwa kilo, Mtendaji Mkuu amesema bei ya ununuzi itakuwa ikitofautiana kutoka eneo moja na eneo linguine.
“Niseme tu kuwa tutaanza na bei ya shilingi 400 hadi 500 kwa kila kilo moja ya mahindi lakini bei hii pia itakuwa ikibadilika kutokana na sababu mbalimbali” Amekaririwa Bwana Milton Lupa.
Naibu Waziri Mgumba ameongeza kuwa NFRA ni Taasisi ya Serikali na imeaminiwa kusimamia jukumu la uhifadhi wa chakula na kuwa Taifa linatarajia makubwa katika kuhakikisha Taifa linakuwa na akiba ya chakula ya kutosha.
“Sisi kama Viongozi wenu, hatuna shaka na uzoefu wenu na umahiri wenu katika nyanja ya uhifadhi wa chakula hususan nafaka kama mahindi, endeleeni mbele na sisi tutahakikisha mnapata mahitaji yenu, nawahakiki kuwa fedha za ununuzi mtazipata kwa kuwa Wizara ya Fedha na Mipango imetuahidi kuwa zitakuja mapema kama mlivyopanga” Amekaririwa Mhe. Mgumba
Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO
0 Comments