Hivi ndivyo Okwi anavyoisumbua Simba | ZamotoHabari.


Mshambuliaji wa Simba na timu ya taifa ya Uganda, Emmanuel Okwi ameendelea kuuwasha moto katika michuano ya mataifa ya Afrika inayoendelea nchini Misri.


Okwi ambaye alimaliza msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita kwa mabao 16, amekuwa msaada mkubwa katika kikosi cha Uganda 'Cranes' ambacho kimefanikiwa kushinda mechi moja na kutoa sare moja katika michuano ya AFCON, huku mwenyewe akifunga mabao 2 mpaka sasa.

Hali hiyo imezidi kuwatamanisha mabosi wa Simba ambao wanamuhitaji mchezaji huyo katika msimu ujao wa ligi, ambapo mpaka sasa wanahangaika kupata saini yake, huku mkataba wake ukiwa ukingoni kumalizika ndani ya Msimbazi.

Inaelezwa kuwa tayari mabosi wa Simba wametua nchini Misri ili kumalizana na mchezaji huyo, ambapo mwenyewe amekuwa akisita kuweka wazi endapo ataendelea kubakia Msimbazi msimu ujao au ataondoka, akisisitiza kuwa hawezi kusema chochote hivi sasa michuano ikiwa inaendelea.

Simba imewasainisha mikataba mipya wachezaji wengi waliokuwa nao msimu uliopita wakiwemo, Aishi Manula, Erasto Nyoni, Meddie Kagere, Shomari Kapombe, John Bocco, Mohamed Hussein na Jonas Mkude, huku kikwazo kikubwa kikiwa ni kwa Okwi ambaye bado hajaridhia kumwaga wino katika klabu hiyo.

Usiku wa leo majira ya saa 5:00, Uganda itaingia dimbani kuvaana na wenyeji Misri katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi ya michuano hiyo. Endapo Uganda itapata ushindi au sare yoyote katika mchezo huo itakuwa imejihakikishia kufuzu hatua inayofuata ya 16 bora.
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipo
BOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini