LEMA AWATAKA WAKAZI WA JIJI LA ARUSHA KUTOKUWA NA HOFU | ZamotoHabari.

Na,Jusline Marco -Arusha

Mbunge wa Arusha Mjini Mhe.Godbless Lema amewataka wakazi wa jiji la Arusha kutokuwa na hofu katikati mwao kwani hofu lazima ishindwe kwa vitendo.

Lema aliyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya soko kuu  jijini Arusha ambapo alisema hofu imepandikizwa katika nchi na kuwafanya watu kuwa waoga na wengi wao kukata tamaa  ya kupiga kura katika uchaguzi ujao.

Kufuatia hali hiyo aliwaondoa hofu wananchi wake na kuwataka wafahamu kuwa hao wanaowatisha na kuwafanya waogope kushiriki zoezi la upigaji kura mwaka ujao wanaweza wasiwakute kwasababu mungu ana nguvu kuliko wao.

Alisema shauku yake ya kupigania haki inazidi maumivu ya mauti hivyo amewataka wananchi hao kuendelea kuimarika katika umoja wao na kuimarisha imani zao pindi wasikiapo maneno ya kuwatia hofu katika mapambano ya kudai haki.

"Safari ya wana wa israel kufika kanani haikuwa rahisi lakini walifika,tunamjua mungu tunaye muamini".Alisema Mbunge Lema

Aliongeza  kuwa madiwani wengi wa chama cha demokrasia na maendeleo wamenunuliwa kwasababu ya hofu iliyotanda mioyoni mwao."Kuliko nijiunge na chama cha mapinduzi nitaenda kuwa Mwalimu wa madrasa au Sunday school hiyo pia ni kazi ya utume"Alisema Lema

Naye katibu wa Wilaya wa chama hicho Innocent Kisanyage alisema kuwa nchi ya Tanzania inaongozwa kwa mujibu wa katiba,taratibu na kanuni ambapo katika katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 18 kifungu cha (D)kikielezea ni haki ya Kila mmoja  kupataji wa taarifa za matukio mbalimbali yahusuyo jamii wakati wote.

Sambamba na hayo amewakata wananchi walio na umri kuanzia miaka 18 na kuendelea kujitokeza kwa wingi kwenye zoezi la uandikishwaji katika daftari la kudumu la wapiga kura linalotarajiwa kuanza Julai 18 hadi 24 mwaka huu ambapo ametoa wito kwa wananchi wote wa jiji la Arusha walio katika kata zote 25 na vituo 185 kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo litakalowawezesha kupiga kura katika uchaguzi wa mwaka 2020.
 Mbunge Lema akiweka msisitizo kwa wakazi wa Arusha akiwataka kutumia akili kwenye kuchuja mambo na kuondoa hofu katika utafutaji wa haki
Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema akizungumza na wakazi wa jijini Arusha kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika  viwanja vya soko kuu.


Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini