MAKATIBU TAWALA WAOMBWA KUENDELEA KUZISIMAMIA HOSPITALI ZA RUFAA | ZamotoHabari.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Zainab Chaula akisema jambo kwa wajumbe wa kikao cha Viongozi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa kilichofanyika jana Jijini Dodoma.
Mwakilishi wa Makatibu Tawala Mikoa Bi. Zena Said, Katibu Tawala Mkoa wa Tanga akisema jambo katika kikao kazi cha Viongozi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa kilichoandaliwa na Wizara ya Afya na kufanyika katika ukumbi wa mikutano Chuo cha Mipango Dodoma.
Makatibu Tawala Mikoa nchini Tanzania wakisikiliza mada zinazowasilishwa katika Kikao Kazi na Viongozi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Zainab Chaula amewataka Makatibu Tawala nchini kuendelea kuzisimamia Hospitali za rufaa za mikoa ambazo kwa sasa zinasimamiwa na Wizara ya Afya.

Dkt. Chaula amesema hayo leo alipokutana na Makatibu Tawala kutoka Mikoa ya Tanzania Bara katika Kikao Kazi cha Viongozi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa kinachoendela kufanyika katika ukumbi wa Chuo cha mipango Jijini Dodoma.

“Licha ya Hospitali hizi kuhamishiwa usimamizi kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)  lakini bado zipo kwenye maeneo yenu, tunawategemea nyie Makatibu Tawala kuzisimamia hospitali hizi.” Amesema Dkt Chaula.

Dkt. Chaula amesema kuwa ni dhahiri lengo lilikuwa ni jema tuu kutoka kwa Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli, kwamba Hospitali zisimamiwe na Wizara ya Afya ili ziweze kuwa na mahusiano ya moja kwa moja na Wizara ya Afya ambayo ndiyo Wizara mama inayotunga Sera na Miongozo pamoja na kusimamia Wadau.

Naye Mwakilishi wa Makatibu Tawala wa Mikoa katika kikao hicho Bi. Zena Said amempongeza Katibu Mkuu Wizara ya Afya kwa kuandaa kikao hicho cha kihistoria ambacho hakijawahi kufanyika kabla.
“Hili ni jambo la busara, pamoja na kwamba hizi Hospitali zimeondolewa kwenye mamlaka za Tawala za Mikoa lakini bado kuna mambo mengi ambayo bado tunayafanya kwa niaba ya Wizara” amesema Bi. Zena na kuendelea “Sisi kama viongozi tupo mikoani hatuwezi kukaa kuangalia mambo yakiharibika tukisea hizi Hospitali sio za kwetu” 

Bi Zena Said amesema kuwa Bado wanawajibika kwa njia moja au nyingine kuzisimamia kwa ajili ya kuleta ustawi kwa wananchi wetu na sisi wenyewe ambao tunatibiwa huko” amesema Bi. Zena Said.

Kikao hicho cha kihistoria kinafanyika kwa mara ya kwanza tangu kuhamishiwa kwa usimamizi wa wa Hospitali za Rufaa za Mikoa tarehe 25, Novemba 2017 ambacho kitakuwa endelevu kila mwaka huku kikiwakutanisha viongozi wa hospitali, Waganga wakuu wa Mikoa pamoja na watendaji na wadau wa Sekta ya Afya nchini.



Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini