Mwinyi Zahera Atangaza Kikosi Kipya cha Yanga | ZamotoHabari.

MTAANI kwa sasa mashabiki wa Yanga ndiyo wanatamba kwa nguvu kutokana na uboreshaji wa kikosi cha msimu ujao uliofanywa na viongozi wa timu hiyo.



Yanga kwa msimu uliomalizika hivi karibuni walikuwa na timu ya ungaunga jambo ambalo liliwafanya wapinzani wao Simba kutwaa ndoo ya ubingwa wa ligi kirahisi.



Sasa kwa kutotaka kurudia makosa mabosi wa Yanga wameshusha nondo za kutosha ndani ya kikosi chao kwa kufuata maagizo maalum waliyoachiwa na kocha wao, Mwinyi Zahera.



Timu hiyo hadi sasa imeshafanya usajili wa wachezaji wapya ambao peke yao ukiwaweka bila ya kuongeza nyota hata mmoja kutoka wale waliobakia basi wanatosha kuunda kikosi chao.



Kikosi hicho ambacho kinawapa mashabiki wa Yanga jeuri ya kuhoji ni lini watakutana na wapinzani wao, kinaundwa na kipa Farouk Shikhalo ambaye amemwaga wino usiku wa juzi Ijumaa kwa miaka miwili akitokea Bandari FC ya Kenya.



Shikhalo atakuwa analindwa na mabeki Ally Ally ‘Mpemba’ aliyetokea KMC atakayecheza upande wa kulia wakati beki wa kushoto atakuwepo Ally Mtoni ‘Sonso’.



Mabeki wa kati watakuwa Mghana Lamine Moro na Mrundi Mustapha Suleiman. Kiungo mkabaji atakabidhiwa mikoba Abdulaziz Makame aliyetokea Mafunzo FC wakati kiungo mchezaji ni Balama Mapinduzi aliyejiunga akitokea Alliance Schools.



Viungo wa pembeni (mawinga) ni Issa Bigirimana ‘Walcot’ na Patrick ‘Papy’ Sibomana.
Pacha ya ushambuliaji katika kikosi hicho kipya kabisa cha Yanga ni Juma Balinya aliyetokea Polisi ya Uganda sambamba na Maybin Kalengo ambaye yeye ametua akitokea Zesco ya Zambia.



Mwenyekiti wa Yanga, Dk Mshindo Msolla amefunguka kuwa usajili wa wachezaji wote hao umetokana na mapendekezo ya kocha Mwinyi Zahera.



“Sisi tumekamilisha kazi yetu ya kusajili kama kocha Zahera alivyokuwa anataka na sasa imebaki yeye tu kuja kuwatumia wachezaji hao. Usajili wote huu ni kutokana na alivyohitaji yeye.”




Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipo
BOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini