Mwanamuziki Nicki Minaj amelazimika kuvunja tamasha alotakiwa kulifanya nchini Saudi Arabia wiki ijayo akisema anaunga mkono haki za wanawake na wapenzi wa jinsia moja.
Taarifa za nyota huyo wa miondoko ya rap kutumbuiza Saudia ziliwashtua wengi na kusababisha kelele kali kutoka kwa wanaharakati wanaokosoa rekodi ya haki za binadamu ya nchi hiyo.
Wengine wakawa wanajiuliza msanii huyo atavaaje kwenye tamasha hilo kwa kuwa nchi hiyo inafuata mfumo wa kihafidhina wa Kiislamu, na Minaj ni maarufu kwa kuvaa nusu uchi.
Saudi Arabia imekuwa ikijaribu kulegeza vikwazo kwenye sekta ya burudani ili kukuza sekta ya sanaa kwa ujumla ya nchi hiyo.
Ukoselewaji wa Saudia kwenye eneo la haki za binadamu uliongezeka zaidi baada ya mauaji ya mwanahabari Jamal Khashoggi katika ubalozi mdogo wa Saudia jijini Istanbul, Uturuki mwezi Oktoba mwaka jana.
Mwezi Machi mwaka huu, nchi hiyo ikaingia lawamani zaidi baada ya kuwafungulia mashtaka wanawake 10 ambao ni wanaharakati wa haki za binaadamu.
"Baada ya kufikiria kwa kina, nimemaua kutoendelea na tamasha langu jijini Jeddah," mwanamuziki huyo amesema kwenye taarifa yake.
Haki miliki ya pichaGETTY IMAGES
"Japo ninapenda kwelikweli kutumbuiza mbele ya mashabiki zangu nchini Saudia, lakini baada ya kujipatia elimu zaidi kwa masuala kadhaa, naamini ni muhimu kwangu kuweka wazi kuwa naunga mkono haki za wanawake, wapenzi wa jinsia moja na uhuru wa kujieleza."
Ijumaa iliyopita, Taasisi ya Haki za Binaadamu yenye maskani yake nchini Marekani ilimuandikia barua ya wazi Minaj ikimtaka aachane na taasha hilo la Julai 18.
Walimuomba nyota huyo "akatae pesa za utawala (wa nchi hiyo)" na kutumia ushawishi wake kushinikiza kuachiliwa huru kwa wanaharakati wanawake waliokamatwa.
Watumiaji mbalimbali wa mitandao ya kijamii walimshambulia Minaj kuwa kukubali kutumbuiza Saudia ilikuwa ni unafiki.
Mashambulizi hayo yanatokana na Minaj amekuwa akijitokeza kwenye matukio ya kuungamkono mapenzi ya jinsia moja na kukubali kutumbuiza kwenye nchi ambayo inapiga marufuku mahusiano ya kimapenzi ya aina hiyo.
Minaj si nyota wa kwanza kuzua 'makelele' kwa kukubali mwaliko wa kwenda kutumbuiza Saudia.
Mapema mwaka huu, mwanamuziki Mariah Carey aliyapa kisogo maombi ya wanaharakati kuacha kutumbuiza nchini humo huku Disemba mwaka jana mwanamuziki Nelly alikosolewa vikali kwa kutumbuiza kwenye tamasha la wanaume pekee nchini humo.
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipo
BOFYA HAPA
0 Comments