RC MTAKA ATAKA MAFUNDI WANAOTOKA KWENYE JAMII WATAMBULIWE, WAJENGEWE UWEZO | ZamotoHabari.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(kushoto) akizungumza na Viongozi wa Wilaya ya Busega, Itilima na Bariadi katika majumuisho ya Ziara ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa katika Hospitali za Wilaya hizo, iliyofanyika Julai 04,2019. 
Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Mhe. Benson Kilangi(kushoto) akimuongoza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka na wajumbe wengine wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa kukagua ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Itilima, Julai 04, 2019. 
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(mwenye koti jeusi) na viongozi wengine wakitoa katika moja ya majengo ya Hospitali ya Wilaya ya Bariadi wakati wa ziara maalum ya kukagua ujenzi wa hospitali hiyo iliyofanyika Julai 04,2019 
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(mwenye shati la kitenge mbele) na viongozi wengine wakitoa katika moja ya majengo ya Hospitali ya Wilaya ya Busega wakati wa ziara maalum ya kukagua ujenzi wa hospitali hiyo iliyofanyika julai 04, 2019 
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(mwenye shati la kitenge mbele) na viongozi wengine wakitoa katika moja ya majengo ya Hospitali ya Wilaya ya Busega wakati wa ziara maalum ya kukagua ujenzi wa hospitali hiyo iliyofanyika Julai 04, 2019 
Baadhi ya viongozi wa Mkoa wa Simiyu wakikagua Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Bariadi Julai 3, 2019. 
Baadhi ya majengo ya Hospitali ya Wilaya ya Busega yakiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi 
Baadhi ya majengo ya Hospitali ya Wilaya ya Bariadi yakiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi 
………………………………….

Na Stella Kalinga, Simiyu 
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kupitia kwa wahandisi wa ujenzi kuwatambua na kuwajengea uwezo mafundi wote wanaotoka kwenye jamii wanaofanya kazi za serikali kwa kutumia mfumo wa ujenzi usiotumia wakandarasi (Force Account) hususani waliofanya kazi nzuri kwenye ujenzi wa hospitali za wilaya ya Mkoa wa Simiyu. 

Mtaka ameyasema hayo mara baada ya kufanya ziara katika hospitali za wilaya ya Itilima, Bariadi na Busega zinazoendelea kujengwa lengo ni kujua hatua ziizofikiwa katika ujenzi, ambapo amesema mafundi hao wakitambuliwa na kujengewa uwezo utendaji wao utaimarishwa na kazi watakazofanya zitafanywa katika ubora. 

“Ni lazima kama Mkoa tuwe na mfumo wa kuwatambua mafundi wote waliofanya kazi ya kujenga hospitali zetu zote tatu na tuanze kuwajengea uwezo,ili miradi yetu ya Serikali tunayoendelea kuifanya tusiwe na watu wapya sana na kama tukipata wapya watakuwa wanafanya kazi chini ya uangalizi wa watu wenye uwezo mzuri zaidi” Mtaka 

Mbali na hayo amezipongeza wilaya hizo kwa mfumo walioutumia wa kununua vifaa kiwandani moja kwa moja kwani umesaidia kuokoa fedha nyingi ambazo zimefanikisha ujenzi kufikia katika hatua nzuri, huku akizisisitiza wilaya hizo kuwashirikisha Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kwenye ununuzi wa vifaa vya umeme ili kupunguza gharama zisizo za lazima. 

Kwa upande wao Wakurugenzi wa Halmashauri za wilaya SACF James John (Bariadi) Elizabeth Gumbo (Itilima) wamesema kuwa miongoni mwa changamoto zilizopelekea kutokamilisha kwa miradi hiyo ambayo ilitakiwa kukamilika Juni 30 , 2019 ni fedha kutotosheleza na kusisitiza kuwa ikiwa watapokea fedha mapema watakamilisha majengo yote. 

“Tulipokea bilioni 1.5 tumebakiwa na shilingi milioni 75 kwa ajili ya kulipa mafundi tulioingia nao mkataba, ili tuweze kukamilisha hatua zilizosalia katika ujenzi wa majengo saba ya awali tunahitaji shilingi milioni 370” alisema James John mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi. 

“Tulipokea shilingi bilioni 1.5 tumebakiwa na shilingi milioni ambazoo zimetengwa kwa ajili ya malipo ya mafundi, tukiongezewa shilingi milioni 360 tutamaliza majengo kwa hatua zilizobaki” alisema Elizabeth Gumbo mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Itilima. 

Hata hivyo Mkuu wa Wilaya ya Busega Tano Mwera amebainisha kuwa kwa hatua walioyofikia fedha zinatosha kukamilisha mradi na kwamba changamoto iliyopelekea wasiweze kukamilisha kwa wakati ni ucheleweshwaji wa mfumo na kwamba ikifanyiwa kazi mradi utakamilika kwa wakati. 

Naye Katibu Tawala wa mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini amesisitiza Halmashauri za Wilaya ya Bariadi, Busega na Itilima kumalizia ujenzi wa Hospitali za wilaya kwa wakati ambapo pia alitoa rai ya kuhakikisha barabara zinatengenezwa, miti na bustani za maua zinapandwa katika maeneo hayo ambayo hospitali hizo zinajengwa. 

Katika ujenzi wa hospitali za wilaya ya Bariadi, Itilima na Busega ambao ni wa awamu ya kwanza kuna jumla ya majengo takribani ishirini na moja yanapaswa kujengwa (21) ikiwa ni majengo saba kwa kila Hospitali (kwa awamu ya kwanza) ambayo yapo katika hatua mbalimbali.


Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini