UKARABATI WA KIVUKO CHA MV. PANGANI II MBIONI KUKAMILIKA | ZamotoHabari.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle kulia akikagua kivuko cha MV. Pangani II kilichokuwa kinafanyiwa ukarabati mkubwa. Kivuko hicho kilihamishwa kutoka Utete Wilaya ya Rufiji ambapo kilikua kinatoa huduma kati ya Utete na Mkongo katika mto Rufiji. Kushoto ni Meneja wa TEMESA mkoa wa Tanga Mhandisi Margareth Gina.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle katikati akikagua injini ya kivuko cha MV. Pangani II ambacho kilihamishwa kutoka Utete Wilaya ya Rufiji. Kivuko hicho kimefanyiwa ukarabati mkubwa na kinatarajiwa kuanza kutoa huduma hivi karibuni katika mto Pangani kati ya Pangani na bweni, kushoto ni Meneja wa TEMESA mkoa wa Tanga Mhandisi Margareth Gina na kulia ni Mkuu wa Kivuko cha Pangani Mhandisi Abdulrahman Ameir.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle kushoto akikagua chumba cha kuhifadhia vipuri vya magari na vifaa vya matengenezo kinga katika karakana ya TEMESA mkoani Tanga. Katikati ni Meneja wa TEMESA mkoa wa Tanga Mhandisi Margareth Gina na kulia ni mhasibu Martin Joram.
PICHA ZOTE NA ALFRED MGWENO (TEMESA TANGA)
……………………..
ALFRED MGWENO (TEMESA) TANGA
Kivuko cha MV. Pangani II ambacho awali kilikua kikijulikana kama MV. Utete kinatarajiwa kukamilika hivi karibuni na kuanza kutoa huduma katika mto Pangani kati ya Pangani na Bweni mkoani Tanga. Kivuko hicho ambacho kilikuwa kikifanyiwa ukarabati mkubwa kilihamishwa kutoka Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani kilipokuwa kinatoa huduma kati ya Utete na Mkongo kutokana na mto Rufiji kukauka maji kwa kiasi kikubwa na kukosa kina na hivyo kusababisha kivuko kushindwa kufanya kazi kwa kipindi kirefu. Kwa sasa wakazi wa maeneo hayo wanahudumiwa na boti ya MV. Mkongo inayobeba abiria arobaini ambayo ina uwezo wa kutembea kwenye maji mafupi.
Akikagua kivuko hicho mapema leo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Maselle ambaye aliambatana na Meneja wa TEMESA mkoa wa Tanga Mhandisi Margareth Gina na mkuu wa kivuko Pangani Bweni Mhandisi Abdulrahman Ameir, aliridhishwa na kazi ya ukarabati huo, hata hivo aliagiza kazi hiyo ikamilike mapema ili kivuko hicho kiingizwe kwenye maji tayari kwa kufanyiwa majaribio ya mwisho na kuanza kutoa huduma.
‘’Baada ya hapa tunatarajia kufanya ukarabati mdogo wa kivuko cha MV. Tanga ikiwemo kukipaka rangi hivyo basi hakikisheni mnamaliza kazi hii kwa haraka ili tuweze kukamilisha ukarabati huo mapema na kuanza kutumia kivuko hiki’’, alisema Mhandisi Maselle.
Aidha Mtendaji mkuu alimuagiza msimamizi wa matengenezo hayo kuhakikisha anamalizia ukarabati huo kama ambavyo mkataba unamtaka.

Awali Mhandisi Maselle alitembelea karakana ya TEMESA mkoa ambapo alipata nafasi ya kuzungumza na wafanyakazi na kukagua baadhi ya miundombinu iliyopo katika karakana hiyo ikiwemo mitambo pamoja na kukagua chumba cha kuhifadhia vipuri vya magari na vifaa vya matengenezo kinga ambapo aliridhishwa na akiba kubwa ya vipuri iliyoko katika karakana hiyo na kumpongeza meneja wa mkoa huo kwa kuanza kutekeleza maagizo ambayo aliyatoa alipotembelea mwishoni mwa mwaka jana. Kuwepo kwa akiba ya kutosha ya vipuri vinavyotoka kwa haraka huwezesha karakana kutengeneza magari kwa muda mfupi na kwa uharaka zaidi.


Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini