WANAFUNZI KUANZA KUIMBA NYIMBO ZA KUHAMASISHA UZALENDO WIKI IJAYO | ZamotoHabari

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo akihutubia maelfu ya wanafunzi, walimu na wakazi wa mkoa wa Mtwara wakati wa hafla ya kufunga mashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA jana katika uwanja wa Nangwanda Sijaona Mtwara. 
Sehemu ya washiriki wa mashindano ya UMITASHUMTA kutoka mkoa wa Tabora wakipita mbele ya jukwaa kuu, wakati wa hafla ya kufunga mashindano hayo jana kwenye uwanja wa Nangwanda Mtwara. 
Mhe. Jafo akisalimiana na wachezaji wa timu ya soka wavulana ya mkoa wa Dar es salaam kabla ya kufanyika kwa fainali ya soka kati ya Dar es salaam na Geita ambapo Geita walifanikiwa kutwaa ubingwa wa soka kwa njia ya mikwaju ya penati jana katika uwanja wa Nangwanda, Mtwara 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo akiwa katika picha ya pamoja na mabingwa wapya wa Soka wavulana UMITASHUMTA 2019 kabla ya mchezo baina ya Geita na Dar es salaam jana katika uwanja wa Nangwanda. 
………………………….. 

Na Mathew Kwembe, Mtwara 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo amewataka Maafisa elimu wa mikoa, na wilaya kuhakikisha kuwa kuanzia wiki ijayo julai 8, wanasimamia agizo la serikali linalowataka wanafunzi wote wanaosoma katika shule za msingi na sekondari zilizo chini ya Ofisi yake, kuimba nyimbo tatu za kuhamasisha uzalendo kila siku asubuhi kabla ya kuanza masomo. 

Akifunga mashindano ya Umoja wa Michezo ya Shule za Sekondari (UMISSETA) na yale ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi (UMITASHUMTA) yaliyofanyika kwenye uwanja wa Nangwanda mjini Mtwara jana, Mhe.Jafo amesema kuwa kuanzia jumatatu ijayo, pindi shule zitakapofunguliwa maafisa elimu wa mikoa, wilaya na maafisa utamaduni wahakikishe kuwa wanafunzi wanaimba wimbo wa Taifa, wimbo wa tazama ramani, na wimbo wa Tanzania, Tanzania. 

Ameongeza kuwa nyimbo hizi ni nzuri sana kwani zikiimbwa kwa pamoja zinaweza kumtoa mtu machozi kwani kielelezo cha kujenga umoja na utaifa kwa watanzania. 

“Nyimbo hizi zinajenga umoja wetu, zinajenga utaifa wetu, lakini siyo wote wanaoweza kuimba nyimbo hizo, wengine wakianza kuimba nyimbo hizo wanaishia kugugumia gumia tu,” amesema Mhe.Jafo 

Waziri Jafo amesema kuwa uamuzi wa kuagiza nyimbo hizo ziimbwe na wanafunzi kila siku asubuhi kabla ya kuanza masomo unalenga kujenga uelewa kwa wanafunzi ili waweze kuzielewa na kuziimba kwa ufasaha nyimbo hizo zinazojenga utaifa na umoja wa Tanzania. 

Hivyo Mhe.Jafo ameagiza kuwa shule zote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zilizo chini ya Ofisi ya Rais TAMISEMI zihakikishe kuwa wanafunzi wake wanaimba nyimbo hizo tatu kila siku asubuhi kabla ya kuanza masomo ili kuhamasisha uzalendo, kujenga umoja na utaifa kwa wanafunzi. 

Amesema maafisa elimu wahakikishe kuwa wanasimamia utekelezaji wa agizo hilo la serikali na wawafundishe wanafunzi wao ili waweze kuimba kwa ufasaha nyimbo hizo tatu za wimbo wa taifa, Tanzania Tanzania, na Tazama ramani. 

Mhe.Jafo amesema kuwa licha ya ugumu utakaojitokeza mwanzoni mwa utekelezaji wa agizo hilo kwa kuzingatia kuwa hata baadhi ya walimu wanaweza wasiimbe kwa ufasaha nyimbo hizo, viongozi hao wanapaswa kuhakikisha kuwa agizo hilo linatekelezwa kwa shule zote nchini. 
“Ninajua mtakapoanza jambo hili pengine, hata baadhi ya walimu watakuwa hawajui kuimba nyimbo hizo, nitoe maelekezo kuwa kila shule iwe na nyimbo hizo na ziimbwe kila siku asubuhi ili kujenga umoja na utaifa wetu watanzania,” amesema. 

Mhe.Jafo amesisitiza kuwa hata atakapokuwa akifanya ziara zake shuleni jambo la kwanza kabla ya kufanya ukaguzi wowote litakuwa ni kuhakikisha kuwa anasikiliza jinsi vijana katika shule atakazotembelea wanavyoziimba. 
Ameongeza kuwa serikali inaamini kuwa maafisa elimu mikoa, wilaya, maafisa utamaduni na wakuu wa shule, na walimu wakuu watasimamia utekelezaji wa agizo hilo ili kuwawezesha wanafunzi wa kitanzania kuweza kuimba nyimbo hizo kwa ufasaha. 

“Hatutaki kuona vijana ambao wanapoteza hata uzalendo, hawajui hata kuimba wimbo wa taifa, tutengeneze uzalendo wetu, tutengeneze utaifa wetu kama taifa letu, imani yangu jambo hili litaleta faraja,” amesema. 
Kuhusu mashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA Mhe. Jafo amesema kuwa Ofisi ya Rais TAMISEMI itaendelea kuhakikisha kuwa michezo hii inaendelea kudumishwa kwa nguvu zote kwa kuhakikisha vipaji vya wanafunzi vinaendelezwa. 

Aidha Mhe.Jafo amemwagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI kuhakikisha kuwa taarifa za wanafunzi wote walioshiriki UMISSETA na UMITASHUMTA mwaka huu zinahifadhiwa katika kanzi data ya wizara na akataka kazi hiyo ikamilishwe ndani ya wiki mbili kuanzia sasa.


Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipoBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini