WAZIRI LUGOLA: MAKANISA, MISIKITI ITAKAYOKWEPA KUHAKIKIWA NCHINI KUCHUKULIA HATUA KALI | ZamotoHabari.


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Mwiseni, Kata ya Butimba, Jimbo la Mwibara, Wilayani Bunda Mkoa wa Mara, katika Mkutano wa hadhara, uliofanyika Kijijini hapo, leo. Lugola ameyataka Makanisa na Misikiti pamoja na Taasisi nyingine za kiroho nchini zifanye uhakiki na endapo zitashindwa kufanya hivyo, zitachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria. 
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mwibara, Kangi Lugola, (kushoto), akimsalimia Mkazi wa Kijiji cha Mwiseni, Kata ya Butimba, Jimbo la Mwibara, Wilayani Bunda Mkoa wa Mara, baada ya kumaliza ya kuzungumza na wananchi katika Mkutano wa hadhara, uliofanyika Kijijini hapo, leo. Lugola ameyataka Makanisa na Misikiti nchini ifanye uhakiki na endapo yatashindwa kufanya hivyo, yatachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. 
……………………………………….. 
Na Felix Mwagara, Mwibara (MOHA) 
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amesema Makanisa na Misikiti nchini ambayo itashindwa kwenda kufanyiwa uhakiki itachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria. 
Waziri Lugola ameyazungumza hayo katika Mkutano wa hadhara wa Wananchi wa Kijiji cha Mwiseni, Kata ya Butimba, Jimbo la Mwibara, Wilaya ya Bunda, Mkoani Mara, leo, ambapo alifafanua kuwa; uhakiki huo ni lazima na unalenga kuzifuatilia taasisi hizo za dini kujua utendaji wake wa kazi kama unaendana na sheria za usajili. 
Lugola amesema Serikali haikuweza kuendelea na usajili wa Makanisa na Misikiti pamoja na Taasisi za kiroho nchini, wakati kwa hivyo ikaona ifanye uhakiki kwanza kwa lengo la kujua taasisi hizo zinaweza sawa na sheria za usajili. 
“Tuhakikishe tunaendesha Makanisa na Misikiti na hizi taasisi za kiroho na kijamii kwa mujibu wa masharti ambayo mmesajiliwa kufanya, na pale ambapo utakuta, Kanisa lolote, Msikiti wowote, taasisi ya kiroho yoyote inafanya shughuli zake kinyume ne kusajiliwa kwake, kujihusisha na mambo ambayo hawaruhusiwi, sisi kama Wizara tumeapa kumsaidia Mhe. Rais tutachukua hatua kwa mujibu wa sheria na utaratibu,” alisema Lugola. 
Aidha, Waziri Lugola aliwatoa hofu wananchi kutokana na kuwepo kero ya upatikanai wa vitambulisho vya taifa, alisema hakuna mwananchi atakayekosa kitambulisho hicho na mwanzoni mwa wiki hii amewaelekeza Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), kutoa namba kwa wakati ili waweze kufanyiwa na usajili wa simu zao za mkononi. 
“Narudia tena, kitambulisho ni haki ya kila mwananchi na hakuna atakayekosa kitambulisho cha taifa, pia nimewaelekeza NIDA waniletee takwimu za Wilaya zote ili kujua ukubwa wa tatizo la usajili wa vitambulisho hivyo unavyoendelea,” alisema Lugola. 
Pia, Waziri Lugola alisema Tanzania ina amani kwasababu inautamaduni wa kuwa na amani, hivyo asitokee mtu akaharibu utamaduni huo ambao nchi inaendelea kuhudumisha. 
“Ndugu zangu wana Mwiseni, Wana Mwibara, amani tulionayo ndiyo inatuwezesha leo tunalima vizuri, tunavua samaki, leo tunakula vizuri, leo tunafanya shughuli mbalimbali za maendeleo, hivyo tuendelee kuitunza amani hii,” alisema Lugola. 
Aliongeza kuwa, Wizara yake kupitia Jeshi la Polisi ipo imara, Serikali ya Rais Dkt. John Magufuli ipo imara na inaendelea kuwalinda Watanzania mahali popote walipo nchini, na hakuna mtu atakaye ivunja amani hiyo. 
Aidha, Lugola aliwataka wananchi hao kuhifadhi vyakula vizuri ili kuepusha janga la njaa kwa hapo baadaye na kusababisha wananchi kuja kuteseka kwa ukosefu wa vyakula na kusababisha mateso katika familia. 
“Tutunzeni vyakula vyetu, msitumie hovyo, kuweni makini na matumizi ya vyakula, sitaki nije kuona mnateseka na njaa, hakikisheni mnatunza vyakula kwa ajili ya matumizi ya baadaye, ogopeni njaa kama ukoma,” alisema Lugola. 
Lugola ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo hilo, ameanza ziara jimboni kwake ya kufanya ukaguzi wa miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi kupitia kufanya mikutano ya hadhara.


Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini