Hatimaye ahadi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliyowaahidi wananachi wa Zanzibar kuwa Serikali anayoiongoza itanunua meli mpya ya mafuta MT MKOMBOZI II leo imetimia baada ya meli hiyo kuwasili katika Bandari ya Zanzibar ikitokea Shanghai nchini China.
Rais Dk. Shein akiwa Ofisini kwake Ikulu mjini Zanzibar alipata fursa ya kuiona meli ya MT MKOMBOZI II ikiwasili kutoka ukingoni mwa pwani ya Zanzibar ikitokea usawa wa kisiwa cha Chumbe na kuelekea katika Bandari ya Malindi Mjini Unguja ilipokwenda kutia nanga.
Akiwa katika varanda ya jengo la Ikulu mjini Zanzibar Rais Dk. Shein alionekana akiwa na furaha kubwa wakati akiiangalia meli hiyo ikiwasili ikiwa ni kutokana na ahadi aliyoitoa na azma yake juu ya ujio wa meli hiyo mpya ya mafuta.
Meli hiyo iliyotengenezwa na Kampuni ya Damen Shipyard ya nchini Uholanzi iliwasili rasmi katika Bandari ya Malindi Zanzibar majira ya saa saa tano za asubuhi na kupata mapokezi ya aina yake.
Wafanyakazi wa Wizara hiyo na viongozi wao pamoja na wafanyakazi wa taasisi nyengine za Serikali na sekta binafsi waliungana pamoja na baadhi ya waandishi wa habari waliohudhuria katika eneo la Bandari ya Malindi mjini Zanzibar kwa ajili ya mapokezi ya meli yao hiyo.
Mapema hapo jana Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, mawasiliano na Usafirishaji Mustafa Aboud Jumbe akitoa taarifa kwa wananchi huko ofisi kwake Kisauni, alithibitisha ujio wa meli hiyo na kueleza jinsi hatua mbali mbali zilizochukuliwa katika mchakato wa kununuliwa meli hiyo na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hadi kuwasili kwake hapa nchini hii leo.
Kwa maelezo ya Katibu Mkuu huyo meli mpya MT UKOMBOZI II, ni meli mpya ambapo majadiliano juu ya ujenzi wa meli hiyo yalianza mwaka 2017 na mkukuku wake uliwekwa rasmi mwezi Julai mwaka 2018 na hatimae meli hiyo ujenzi wake ulimalizika mwezi April mwaka huu 2019.
Katibu Jumbe katika taarifa yake alisema kwamba hivi karibuni ujumbe kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ulikwenda kuishuhudia meli hiyo mnamo Julai 8, 2019 ikiwa tayari imeshakamilika na ndipo wakafanya makubaliano na watengenezaji wa meli hiyo ya Kampuni ya DAMEN TANKER SHIP ya Uholanzi iliyoitengeneza.
Jumbe alieleza kuwa baada ya makubaliano hayo Meli hiyo iliza safari ya kusafiri kutoka bandari ya Shanghai nchini China kwa muda wa siku 28 na kuwasili hapo jana katika maji ya pwani ya Zanzibar na leo iliwasili kwa makabidhiano rasmi na Serikali na baada ya hapo itazinduliwa kwa ajili ya kuanza shughuli iliyokusudiwa.
Alieleza kuwa meli hiyo ni meli ya mafuta yenye urefu wa mita 86.2 na yenye uwezo wa kupakia tani 3500 za mafuta kwenye visima 4 vilivyomo katika meli hiyo.
Aidha, thamani iliyotumika kuitengeneza meli hiyo ni URO Milioni 14.3 sawa na wastani wa Bilioni 36 za Kitanzania ambapo meli hiyo itaungana na meli ya MT UKOMBOZI I ambayo ipo hapa nchini na yenye uwezo wa kupakia tani 2400.
Katibu Mkuu huyo alieleza kuwa madhumuni ya taarifa hiyo aliyoitoa hapo jana jioni ni kuwaarifu wananchi kuwa meli hiyo imeshawasili Zanzibar na maandalizi yanafanywa ili izinduliwe rasmi na tayari ameshaombwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa meli hiyo katika siku itakayopangwa.
Aliwashukuru wananchi wa Zanzibar kwa kufuatilia kwa makini juu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kama ilivyoelezwa kwenye ukurasa wa 152 kifungu cha 90 katika kifungu kidogo cha 4 ambacho kimeagiza kwamba Serikali itanunua meli mpya ya mafuta kwa ajili ya matumizi ya Zanzibar.
“Naomba sana kumshukuru Mhe. Rais kwa kutuamini kuisimamia kazi hiyo na hivi sasa tuko ukiongoni katika kuikabidhi meli hiyo”, alisema Mustafa Jumbe.
Hizo ni juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dk. Sheinkatika kuhakikisha sekta ya usafiri na usafirishaji inaimarika kwa kiasi kikubwa ambapo mnamo mwezi Disemba mwaka 2015 meli mpya ya MV MAPINDUZI II iliwasili Zanzibar ikitokea nchini Korea Kusini ilikotengenezwa ikiwa ni agizo la Rais Dk. Shein la kununuliwa meli hiyo.
MV MAPINDUZI II ambayo ilitengenezwa na Kampuni ya Daewoo International ya nchini Korea Kusini ilianza kutengenezwa Julai mwaka 2013 na hadi Disemba 2015 iliwasili Zanzibar ikiwa tayari kuanza kutumika.
Jumla ya Dola za Marekani 30.4 zilitumika kutengenezea meli hiyo ambapo ujenzi wake hadi kukamilika ulichukua miezi 18 ambapo meli hiyo ya MV MAPINDUZI II ina uwezo wa kuchukua abiria 1200 pamoja na tani 200 za mizigo.
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipo
BOFYA HAPA
0 Comments