Na Hafsa Omar, Tabora
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani ameendelea na ukaguzi wa kazi ya usambazaji umeme vijijini ili kuhakikisha kuwa lengo la Serikali la kuhakikisha kuwa vijiji vyote vinafikiwa na nishati ya umeme ifikapo mwaka 2021 linafanikiwa.
Tarehe 21 Agosti, 2019, alikagua kazi hiyo katika Kijiji cha Mwisi, Uswaya na Isenegeja wilayani Igunga ambapo aliwasha umeme katika Kijiji cha Isenegeja.
Aidha, akizungumza na wananchi kwa nyakati tofauti, alilisisitiza kuhusu wananchi kulipia gharama ya shilingi 27,000 tu, na bila kujali aina ya nyumba wanazomiliki.
“ Umeme ndiyo nguzo kuu ya maendeleo, hivyo nawasisitiza kuchangamkia huduma hii inayotolewa na Serikali ili muweze kujifanyia shughuli mbalimbali za kiuchumi, kama tulivyosema umeme hautachagua nyumba, umeme wa Serikali hii unapelekwa kwa watanzania wote bila kujali masikini, tajiri au mtanzania wa kawaida.”alisema Dkt Kalemani.
Aidha, Dkt Kalemani aliwaagiza wakandarasi kuacha tabia ya kuchelewa kuwaunganishia umeme wananchi “ nimeshasema ni marufuku kuchelewa kuunganishia umeme wananchi, mtu akishalipia muunganishie umeme ndani ya siku Saba bila kisingizio chochote.”
Kuhusu hali ya umeme nchini, alisema kuwa, hali ya umeme ni nzuri na endapo kunatokea kukatika kwa nishati hiyo, ni kwasababu ya hitilafu tena ya dharura ama kwasababu ya matengenezo.
Kwa nyakati tofauti wananchi wa Vijiji hivyo waliishukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kusambaza nishati ya umeme vijijini na kueleza kuwa itawawezesha kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo kuanzisha mashine za kukoboa nafaka ambapo hapo awali walilazimika kutumia dizeli ili kuziendesha lakini kwa sasa watatumia nishati ya umeme na hivyo kupunguza gharama za uendeshaji.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (katikati) akikata utepe kuashiria uwashaji rasmi umeme katika Kijiji cha Isenegeja wilayani Igunga.
Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (katikati) akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Uswaya wilayani Igunga wakati alipofika kukagua kazi ya usambazaji umeme kwenye Kijiji hicho.
Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO
0 Comments