Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, wakati alipowasili kwenye viwanja vya Nyakabindi, Bariadi mkoani Simiyu, katika kilele cha Maonyesho ya 27 ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi (Nane Nane) 2019.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wakulima nchini kuchangamkia fursa zinazotolewa na Benki ya CRDB kupitia akaunti ya “FahariKilimo” ambayo ni maalum kwa ajili ya wakulima. Akizungumza wakati wa kilele cha maonyesho ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi (Nane Nane) 2019 nchini iliyofanyika kitaifa mkoani Simiyu, Waziri Mkuu alisema akaunti hiyo ya “FahariKilimo” ambayo imeambatana na fursa nyingine za uwezeshaji ikiwamo mikopo kwa wakulima itasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha mnyororo wa thamani wa kilimo nchini.
"Serikali inaridhishwa sana na jitihada kubwa zinazofanywa na Benki hii ya CRDB katika kuboresha sekta ya kilimo nchini. Ubunifu huu wa huduma na bidhaa mnazozitoa kwa wakulima nchini unaambatana na dhamira ya Serikali ya kujenga uchumi wa kati wa viwanda ukizingatia malighafi ya viwanda vyetu inapatikana katika sekta hii mama ya kilimo,” alisema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimsikiliza Mkurugenzi wa Kampuni ya NSAGALI ambaye pia ni Mteja wa Benki ya CRDB Mkoani Simiyu, Emmanuel Silanga alipokuwa akitoa ushuhuda wake wa kuwezeshwa Mkopo uliomuwezesha kununua Pamba kutoka kwa Wakulima, wakati alipotembelea Banda la Benki ya CRDB, katika kilele cha Maonyesho ya 27 ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi (Nane N ane) 2019, kwenye Uwanja wa Nyakabindi, Bariadi mkaoni Simiyu. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela.
Akielezea mkakati wa Serikali katika urasimishaji wa wakulima ilikuwajengea mazingira mazuri ya upatikanaji wa mikopo katika taasisi za fedha, Waziri Mkuu alisema Serikali kupitia Wizara ya Kilimo na Wizara ya Ardhi imeandaa mpango mkakati wa upimaji wa ardhi ya wakulima nchini kote, jambo ambalo pia litasaidia kuongeza thamani ya ardhi ya wakulima hao.
“Nafahamu changamoto kubwa inayopelekea riba za mikopo ya kilimo kuwa kubwa ni pamoja na wakulima kukosa dhamana na mashamba yao kukosa hatimiliki hivyo kuongeza hatari ya mikopo. Jambo hili tunalifanyia kazi lakini pia niyaombe mabenki yote nchini kuweka mkakati madhubuti utakaopelekea kupungua kwa riba kwenye mikopo ya kilimo, riba ikipungua hata wale ambao ni wakopaji wazuri lakini wamekuwa wakihofia gharama za mkopo nao watakuja kukopa,” alisema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akichukua moja ya vipeperushi wakati alipotembelea Banda la Benki ya CRDB, katika kilele cha Maonyesho ya 27 ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi (Nane N ane) 2019, kwenye Uwanja wa Nyakabindi, Bariadi mkaoni Simiyu. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela.
Abdulmajid Nsekela, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, alisema akaunti ya FahariKilimo ni sehemu ya mkakati mpana wa Benki hiyo kuwahudumia wakulima kwa ukaribu zaidi kwa kuzingatia mahitaji yao. “Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba nikujulishe kuwa akaunti hii ya FahariKilimo hufunguliwa bure kabisa na hakuna gharama zozote za uendeshaji wa akaunti kwa mkulima, tukilenga kumpa mkulima unafuu wa kupokea malipo yake pindi anapopokea malipo baada ya kuuza mazao,” aliongezea Nsekela.
Nsekela alisema mpaka sasa wakulima zaidi ya 30,000 tayari wameshajiunga na akaunti ya FahariKilimo na hivyo kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa na Benki ya CRDB kwa wakulima. “Mkulima anapofungua akaunti ya FahariKilimo tunamuingiza moja kwa moja kwa mpango wetu maalum wa uwezeshaji ambapo atakuwa akipata mafunzo mbalimbali juu ya kuboresha kilimo chake kupitia huduma na bidhaa za Benki yake ya CRDB,” alisema Nsekela.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Ester Mwambapa, wakati alipowasili kwenye viwanja vya Nyakabindi, Bariadi mkoani Simiyu, katika kilele cha Maonyesho ya 27 ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi (Nane Nane) 2019.
Nsekela aliendelea kusema baadhi ya fursa ambazo Benki hiyo imekuwa ikitoa kwa wakulima ni pamoja na mikopo ya pembejeo, matrekta ya kulimia, mashine za kupandia, mashine za umwagiliaji, mikopo ya vifaa vya ujenzi pamoja mikopo kwa wawekezaji katika viwanda vya kilimo. “Tumekuwa na utaratibu wakushirikiana na wadau mbalimbali wa kilimo nchini katika kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo za kisasa zitakazopelekea kuongeza kiwango cha uzalishaji na faida wanayopata. Kama unavyoona leo hii hapa tupo na wenzetu wa ETC Agro ambao kwa pamoja tunatoa mikopo ya matrekta kwa wakulima kwa vigezo na masharti nafuu kabisa,” alisema Nsekela.
Nsekela alisema ilikupata mkopo huo wa trekta mkulima anatakiwa kuchangia asilimia 35 wakati asilimia 65 itatolewa na Benki ya CRDB ambapo mteja atalipa kwa muda wa miaka 3. “Katika mkopo huu wa trekta mkulima hahitaji kuwa na dhamana, trekta litatumika kama dhamana ya mkopo,” alisema Nsekela.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimuelekeza jambo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela wakati alipotembelea Banda la Benki ya CRDB, katika kilele cha Maonyesho ya 27 ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi (Nane Nane) 2019, kwenye Uwanja wa Nyakabindi, Bariadi mkaoni Simiyu.
Nsekela alimwambia Waziri Mkuu kuwa asilimia 40 ya mikopo ya kilimo nchini imetolewa na Benki ya CRDB, jambo linaloashiria utayari wa Benki hiyo katika kuboresha sekta ya kilimo nchini. “Kwa mwaka jana pekee Benki ya CRDB kipindi cha mwaka 2018/2019, tumetoa zaidi ya shilingi bilioni 650 katika kilimo,” alisema Nsekela.
Aliendelea kusema kati ya fedha hizo zaidi ya shilingi bilioni 97.3 zilielekezwa kwenye zao la pamba katika kununua mbegu (bilioni 36) na kulipia pamba (bilioni 61). Nyingine zilielekezwa katika kilimo cha miwa (bilioni 167.3), Kilimo cha kahawa (bilioni 36.6), kilimo cha chai (bilioni 60).
“Leo hii hapa tumeambatana na mteja wetu ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha uchakataji pamba ambacho hivi karibuni tumewapatia mkopo kwa ajili ya ununuzi wa zao la pamba,” aliongezea Nsekela.
Nsekela alimalizia kwa kumhakikishia Waziri Mkuu kuwa Benki ya CRDB imedhamiria kwa dhati kuunga mkono sekta ya kilimo na viwanda ili kutimiza azma ya Serikali ya awamu ya tano yakufikia uchumi wa kati unaoshamirishwa na viwanda. “Ahadi yetu kwa Serikali ni Tupo Tayari,” alihitimisha Nsekela.
Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO
0 Comments