WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameziagiza Wizara za Kilimo, Viwanda na Biashara, Uvuvi na Mifugo kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji kutengeneza mkakati wa kuanzisha viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi nchini.
Amevitaja viwanda kuwa ni pamoja na vya nyuzi, nguo, ngozi, maziwa, minofu, nyama, kubangua korosho, kutengeneza unga, mafuta ya kula, sabuni, usindikaji wa matunda na mbogamboga, “Kwani ndiyo msingi wa kauli mbiu yetu ya kufikia uchumi wa viwanda 2025”.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Agosti 8, 2019) katika kilele cha maadhimisho ya sikukuu ya wakulima nane nane Kitaifa kwenye viwanja vya maonesho Nyakabindi mkoani Simiyu kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli.
Waziri Mkuu amsema sambamba na mkakati huo, pia ameagiza kuimarishwa kwa vyama vya ushirika ili kumwezesha mkulima kuendelea kumiliki zao lake mpaka hatua ya kuuza sokoni. “Vyama vya ushirika vikiweza kuchakata mazao na kuyaongeza thamani vitamuwezesha mkulima kuwa na umiliki na kufaidika na bei ya soko”.
Amesema mfano uliooneshwa katika zao la Kahawa kupitia Chama Kikuu cha Ushirika Kagera (KCU) ni mzuri ambapo wanamiliki asilimia 100 ya Kiwanda cha Kukoboa Kahawa (BUCOP), pamoja na asilimia 54 ya Kiwanda cha Kuzalisha Kahawa – Tanganyika Instant Coffee (TANICA).
“Kwa upande wa Pamba, Nyanza Cooperative Union (NCU) walianza vizuri kwa kumiliki viwanda vinane vya kuchambulia pamba. Tunataka jitihada za namna hii zianzishwe katika shughuli za wakulima wetu na zilizopo ziimarishwe”.
Hivyo, ameitaka Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa kushirikiana na wadau, ifanye tathmini kwenye vyama vya ushirika vinavyomiliki viwanda ili kubaini hali ilivyo kwa sasa na kuweka mikakati ya kuvifufua na kuviongezea uwezo.
Amesema safari ya kujenga uchumi wa viwanda itaiwezesha Tanzania kuwa nchi yenye kipato cha kati imeanza na inaendelea vizuri na matarajio yake ni kuona wananchi wote bila kujali tofauti za kiitikadi, wataendelea kuunga mkono juhudi hizo kwa kuwa maendeleo wanayoyapigania ni kwa manufaa ya wote waliopo leo na vizazi vijavyo.
Waziri Mkuu amesema kwa mantiki hiyo, kila Mtanzania hanabudi kuongeza bidii katika kufanya kazi, kupiga vita rushwa, kulipa kodi ya Serikali na kulinda rasilimali za Taifa ili ziweze kutumika sasa na kwa faida ya vizazi vyetu vijavyo.
“Niwaombe muendelee kuiunga mkono Serikali ya Awamu ya Tano kwa namna ambavyo imeamua kwa makusudi kuanzisha miradi mikubwa ya ujenzi wa miundombinu ya kiuchumi inayoendelea kujengwa nchini ikiwemo reli ya kisasa ya mwendokasi, mradi mkubwa wa umeme wa Mto Rufiji, upanuzi wa viwanja vya ndege, bandari na ununuzi wa ndege kubwa”.
Amesema kuboreshwa kwa miundombinu hiyo, pamoja na mambo mengine kutachochea uwekezaji mkubwa katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, kurahisisha usafirishaji wa mazao, mifugo, samaki, na kupunguza gharama za uzalishaji na hivyo kuwezesha viwanda vya ndani kushindana kibiashara na bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya nje ya nchi.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kutoawito kwa viongozi wa Mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga kuendelea kushirikiana na Wizara za Sekta ya Kilimo kuhakikisha viwanja hivyo vya Nyakabindi, vinakuwa kituo cha mafunzo ya wakulima, wafugaji na wavuvi.
“Kumbukeni kuwa kila mmoja wetu akitimiza wajibu wake ipasavyo, maendeleo ya viwanda yanawezekana, ajira zitapatikana, uhakika wa chakula na lishe bora itakuwepo na sote kwa pamoja tutasonga mbele kufikia nchi yenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025”.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya Nane Nane ya mwaka huu inasema: - “Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa Ukuaji wa Uchumi wa Nchi”.Kaulimbiu hiyo inakwenda sambamba na azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kukuza uchumi wa viwanda na biashara, ikilenga kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja, Pato la Taifa na wakati huo huo kupunguza umaskini.
Awali, Waziri Mkuu alitembelea na kukagua mabanda mbalimbali katika maoneosho hayo. Miongoni mwa mabanda aliyoyatembelea ni pamoja na banda la EPZA, NMB, CRDB, NBC, BOT kitengo cha mifumo ya malipo ya Kielektroniki ya Serikali, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi na JKT.
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Bashiru Ally, Waziri wa Ulinzi Dkt. Hussein Mwinyi, Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina, Naibu Waziri Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, Naibu Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI, Josephat Kandege, Naibu Waziri wa Madini, Stansalaus Nyongo pamoja na maafisa wengine wa Serikali.
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipo
BOFYA HAPA
0 Comments