Diamond Platnumz Aweka Rekodi Ujerumani | ZamotoHabari.



DAR ES SALAAM: Staa wa muziki wa Afro-Pop, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ ameweka rekodi ya kipekee nchini Ujerumani baada ya kuangusha shoo.

Shoo hiyo iliyoandika historia mpya kwa wanamuziki kutoka barani Afrika ilifanyika wikiendi iliyopita kwenye Ukumbi wa Colombia uliopo katika Mji Mkuu wa Ujerumani wa Berlin.

Kwa mujibu wa Idhaa ya Kiswahili ya Redio Deutsche Welle (DW) inayorusha matangazo yake kutokea nchini humo, Mondi ameweka rekodi kwa kuwa mwanamuziki wa pili kwa mwaka huu kuujaza ukumbi huo ambao huwa ni nadra mno kwa msanii kuujaza.

Pamoja na kufika Ujerumani na kufanya shoo kwenye miji mbalimbali huku kukiwa na kumbukumbu za vurugu zilizotokea kwenye shoo yake mwaka 2014 nchini humo, hii ilikuwa ni mara ya kwanza kufanya shoo kwenye ukumbi huo ambao hutumiwa na wasanii wakubwa kutoka barani Ulaya, Marekani na wachache mno kutoka Afrika.

Katika tamasha hilo lilihudhuriwa na maelfu ya watu ambao walijaa ndani ya ukumbi huo na wengine wengi kubaki nje.

Baada ya shoo hiyo, watu mbalimbali walikuwa wakimzungumzia Diamond kama mwanamuziki mkubwa kutoka barani Afrika anayependwa zaidi nchini Ujerumani.

Mbali tu na kufanya shoo ya viwango vya juu kwa kuwatumia madensa aliowakodi, pia shoo hiyo ilitumika kuwakutanisha Watanzania waishio nchini Ujerumani na kufurahi pamoja.

“Ilikuwa shoo nzuri sana, imefana sana. Lakini ingekuwa nzuri tena zaidi kama Diamond angeweza kuja na bendi yake nzima.

“Tofauti na hilo ilikuwa ni shoo kubwa sana ambayo hakuna Mtanzania aliyewahi kufika hapa na kufanya shoo kama hii.

“Wamekuja watu wengi, siyo Watanzania tu, Waafrika kwa jumla wameonesha sapoti yao kubwa na wana mapenzi makubwa kwa Diamond,” alisema Emmanuel Mtingwa, mmoja wa wahudhuriaji wa shoo hiyo ambaye ni Mtanzania aishie Ujerumani.

Kwa upande wake Diamond au Mondo, katika mahojiano na DW alisema kuwa kazi yake ni kuwapa watu burudani na hicho ndicho alichokifanya.

“Mimi ninaimba na kucheza. Kazi yangu ni kuwapa watu burudani kisha wafurahi halafu tukitawanyika tukumbukane,” alisema Mondi ambaye ana ziara ndefu ya kimuziki sehemu mbalimbali duniani

Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipo
BOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini