KATIBU MKUU MWAKALINGA ATOA ONYO KWA WATENDAJI WA MIZANI NCHINI | ZamotoHabari.

Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Singida Eng. Matari Masige, akifafanua jambo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Arch. Elius Mwakalinga, wakati alipowasili mkoani humo kwa ajili ya ukaguzi wa barabara, madaraja na mizani.Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Arch. Elius Mwakalinga, akipita juu ya Daraja la Msingi lililopo sasa wakati alipokuwa akikagua hatua za ujenzi wa Daraja jipya la Msingi litakalokuwa na urefu wa mita 75 na barabara unganishi za KM 1 kwa kiwango cha lami, mkoani Singida.Mkandarasi Mzawa wa kampuni ya M/s Gemen, Eng. Eradius Raphael, akimwonesha Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Arch. Elius Mwakalinga, mchoro wa Daraja jipya la Msingi litakalokuwa na urefu wa mita 75 na barabara unganishi za KM 1 kwa kiwango cha lami, mkoani Singida.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Arch. Elius Mwakalinga, akitoa maelekezo kwa Bw. Emmanuel Magandi, ambaye ni Msimamizi wa Mzani wa Nala wakati alipofanya ziara ya kushtukiza katika mizani hiyo, jijini Dodoma.Mtaalam wa Mzani wa Nala Bw. Noel Gabriel, akitoa maelezo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Sekta ya Ujenzi, Arch. Elius Mwakalinga, kuhusu mfumo wa namna ya upimaji wa uzito wa magari katika mizani hiyo, wakati Katibu Mkuu huyo alipokagua utendaji kazi wake, jijini Dodoma.Gari likipima uzito katika mzani wa Njuki uliopo katika barabara ya Singida – Shelui, mkoani Singida. Mzani huo ni moja kati ya mizani mitatu iliyopo mkoani humo ambapo mizani mingine ni Mzani wa Itigi katika barabara ya Manyoni – Itigi – Chaya na Mzani wa Mughamo katika barabara ya Singida – Babati.


……………………
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Arch. Elius Mwakalinga, amekemea vikali vitendo vya rushwa kwa watendaji wote wanaosimamia mizani hapa nchini na hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayehusika.

Kauli hiyo ametoa mjini Dodoma wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi ya kukagua hali ya miundombinu ya barabara, madaraja, mizani, Magari na Mitambo ya Serikali ambapo alianzia mkoani humo katika mzani wa Nala na kusisitiza kwa wafanyakazi wa mizani kuacha kucheza na mizani, kupokea rushwa na kuzembea kazini.

“Serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya matengenezo ya barabara kwani barabara nyingi zinaharibika kutokana na kubeba mizigo mizito na nyie watu wa mizani hamfanyi kazi yenu kikamilifu”, amesisitiza Arch. Mwakalinga.

Arch. Mwakalinga, amesema elimu elekezi itatolewa kwa wafanyakazi wa ngazi zote hata maaskari wanaolinda katika mizani ili kuepusha vitendo vya rushwa na kuingizia gharama kubwa Serikali.

Katika hatua nyingine Katibu Mkuu huyo amekagua mzani wa Njuki uliopo mkoani Singida ambapo Serikali iliamua kujenga mzani huo wa kupima uzito wa magari katika mwendo (Weigh in Motion) ili kupunguza tatizo la msururu mrefu wa magari wakati wa kupima uzito na kuagiza kupatiwa taarifa ya utendaji wa mzani huo kutoka kwa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) wa mkoani humo.

Aidha, amekagua ujenzi wa daraja jipya la Msingi lenye urefu wa mita 75 na barabara za maingilio zenye urefu wa KM 1 kwa kiwango cha lami linalojengwa na mkandarasi mzawa Gemen Engineering na kusimamiwa na Kitengo cha TECU kwa gharama ya shilingi bilioni tisa na kumtaka mkandarasi huyo kuongeza kasi ya ujenzi kabla ya majira ya mvua kuanza.

Kwa upande wake Meneja wa TANROADS mkoa wa Singida Eng. Matari Masige, amemueleza Katibu Mkuu huyo kuwa ujenzi wa daraja hili utakamilika kwa muda wa miezi 24 na mkandarasi yupo katika hatua za awali za kuandaa msingi wa daraja na kuahidi kuusimamia kwa ukaribu mradi huo ambao una miezi mitatu toka kuanza kwake.

Ameongeza kuwa daraja hilo likikamilika litaunganisha wilaya ya Mkalama mkoa wa Singida na Wilaya ya Meatu mkoa wa Simiyu na hivyo kuendelea kufungua mtandao wa barabara kwa kiwango cha lami hapa nchini.

Kuhusu miradi mingine ya kitaifa ya ujenzi Eng. Masige, ameendelea kumueleza Katibu Mkuu huyo kuwa ujenzi wa daraja la Sibiti umekamilika na magari yanapita juu ya daraja na wananchi walioathiriwa na mradi washalipwa fidia wote na hakuna mwananchi yeyote anayedai fidia.



Ujenzi wa Daraja la Msingi ni ahadi ya Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa wananchi wa wilaya ya Mkalama na wilaya jirani na likikamilika litapunguza umbali wa safari kwa watu wanaoelekea mikoa ya Kanda ya Ziwa.


Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini