NA MWAMVUA MWINYI,KIBAHA
WAWEKEZAJI mkoani Pwani wametakiwa kujali maslahi ya wafanyakazi ili kuwapa hamasa ya kufanya kazi na kuwafanya kama sehemu ya familia ya wamiliki wa miradi ya uwekezaji.
Hayo yalisemwa na mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo wakati akiweka jiwe la msingi kwenye kiwanda cha vifungashio vya plastiki cha Wande Printing and Pakaging Co Ltd kilichopo wilayani Kibaha na kusema kuwa wawekezaji wanapaswa kuwafanya wafanyakazi wao kama watu wa familia moja.
Ndikilo alieleza,baadhi ya wawekezaji wameshindwa kufanikiwa kutokana na kutojali maslahi ya wafanyakazi jambo ambalo linasababisha miradi mingi kukwama na kushindwa kufikia malengo waliyojiwekea na kujikuta wakipata hasara.
“Natoa agizo kwa wawekezaji wote ndani ya mkoa wa Pwani kuhakikisha wanawalipa vizuri wafanyakazi wao na kuwafanya sehemu ya familia yao kwani kuwa karibu na wafanyakazi itasaidia wafanye kazi kwa moyo na kuwa na bidii ya kufanya kazi,”alisema Ndikilo.
“Kwa upande wa taasisi wezeshi zikiwemo zinazotoa huduma za umeme, maji na miundombinu lazima ziwe karibu wawekezaji na kuwasaidia wapunguze au kuondoa changamoto ili kuunga mkono serikali katika jitihada za kuifanya nchi kuwa ya viwanda na uchumi wa kati,”alisema Ndikilo.
Naye Mkurugenzi wa benki ya Azania Charles Itembe alisema kuwa benki hiyo ni ya kizalendo na inaunga mkono jitihada za serikali za kuhimiza ujenzi wa viwanda ili kukuza uchumi wa wananchi na nchi kw akutoa mikopo kwa watu mbalimbali wakiwemo wawekezaji.
Meneja uendeshaji John Wande alisema wanazalisha vifungashio vya plastiki kwa ajili ya bidhaa za viwandani,kilimo na sekta ya afya ambapo waliona kuwa kuna changamoto kubwa za upatikanaji wa vifungashio bora kwa ajili ya bidhaa .
Hadi sasa kimetoa ajira kwa watu 60 na baadaye itafikia ajira ya watu 350 na kiwanda hicho kina thamani ya shilingi bilioni 6.6 na kinatarajia kuanza kazi baada ya wiki mbili.
Naye mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa kampuni hiyo Joseph Wasonga alisema kuwa wamekuwa wakishirikiana na serikali kwa kuanzisha viwanda mbalimbali kwa ajili ya kutoa ajira na kukuza uchumi na kuisaidia jamii inayoizunguka kiwanda hicho.
Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO
0 Comments