Na Bakari Kimwanga,aliyekuwa Bangkok, Thailand
SAWADIKA ni salamu ambayo hutolewa kwa mwanamke, na Sawadikrapu
hutolewa kwa mwanamume ikimaanisha habari pindi uingiapo nchini
Thailand.
Unaponunua au kumpa mtu chochote basi utajibiwa kwa neno Koponhka,
likiwa na maana ya ahsante sana.
Haikuwa kazi rahisi kufika katika Jiji la Bangkok nchini Thailand,
lakini tu kwa uwezo wa Mungu, nami nilibahatika kufika nchini humo.
Ilikuwa Agosti 17, mwaka huu, ilipofika saa 7 mchana nilianza safari
kutoka nyumbani na kueleka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius
Nyerere, ambapo nilisoma maelezo ya tiketi yangu ya ndege ya Shirika
la Ndege la Qatar ikiniambia kwamba ninataka kuwa uwanja wa ndege mpya wa Terminal III kuanzia saa 9:5 alasiri kwa ajili ya safari.
Nilifika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere saa 8 mchana, ambapo mimi
na wasafiri wenzangu ambao tulikuwa tukisafiri na ndege ya Qatar
tulipewa maelezo ya kututaka kuanza kukaguliwa kuanzia saa 9:5
alasiri. Nikiwa nimekaa kwenye viti na abiria wenzangu nilianza kuvuta
taswira nzito kuhusu safari itakavyokuwa kutoka Dar es Salaam hadi
katika Jiji la Bangkok nchini Thailand.
Hakika muda ukafika tukakaguliwa na kuingia ndani ya uwanja mpya wa
ndege huku mawazo yaliyoambatana na usingizi yalikuwa ni jinsi
nitakavyoshuhudia mji huo.
Naam; ilipofika saa 11 jioni abiria tulitangaziwa kwamba sasa tunaaza
kuingia ndani ndege awamu kwa awamu, ambapo mimi nakumbuka tiketi
yangu ilikuwa imeandika ‘Zone 3’ tukaitwa nami nikajongea huku nikiwa
na picha sasa tunaanza safari lakini je, ndani ya ndege itakuwaje?
Nikiwa ndani ya ndege kwenye kiti changu namba 24 E huku jirani yangu
akiwa ameketi mwenzangu, Exper Pius, ambaye ni mtaalamu wa mazingira
na mtumishi wa Taasisi ya Kimataifa ya RTI iliyo chini ya USAID
Protect Tanzania, chini ya mradi wa Wildlife Combating Crime, ikiwa
inaangazia masuala ya usafirishaji haramu wa wanyama.
Ndani ya ndege nikaanza kumuuliza maswali kadhaa je, hii safari yetu
itakuwaje? Jibu lake lilikuwa jepesi, tuombe Mungu tutafika salama
Thailand, hakika tunakwenda mashariki ya mbali, ambapo tutafika kesho
mchana wakati huku kwetu itakuwa ni asubuhi.
Licha ya wahudumu kupita na kunipa viburudisho, lakini bado akili
yangu ilikuwa ikipiga picha Thailand hasa Bangkok ikoje!
Ilipofika saa 12 jioni abiria wote tuliokuwamo ndani ya ndege,
tukatangaziwa tena umuhimu wa kufunga mikanda huku wahudumu wa ndegewakiwa wanapita katika kila kiti na kumkagua abiria kama amefunga
mkanda.
Kazi hiyo ikakamilika likatoka tangazo ya kwamba sasa tunaanza safari,
mara ndege ikachochewa injini kelele zikawa nyingi, huku mitetemo
ikitamalaki watu tukiwa vitini kwa utulivu huku kila mmoja amefunga
mkanda.
Ndege ukajisogeza taratibu kwenye njia yake na kuanza kupaa angani,
huku nikiwa kitini na kazi ya kusima ramani kupitia ‘tv ndogo ya
kwenye kiti’ na kuona tunamaliza anga ya Tanzania kuingia Kenya na
kisha Somalia, baada ya muda usingizi ukanipitia na ilipofika saa 7:30
usiku tulitua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Hamadi mjini Doha nchini
Qatar.
Tukashuka na kuanza kutafuta ndege nyingine ya kuelekea Bangkok nchini
Thailand, ukubwa wa unjwa wa Kimataifa wa Hamadi Doha, ulinishangaza
na kuona alaa kumbe dunia ina mambo mazuri na kila mtu yupo mbio na
baada ya kutembea kwa umbali mrefu hatimaye tulilifikia geti namba
nane, tulilotakiwa kupita ili kuanza safari yetu ya pili.
Mungu alitusaidia na tulitimiza wajibu wetu ikiwamo ukaguzi na kukaa
mapumziko kidogo na ilipofika saa 8 usiku tulitangaziwa na abiria
kuanza ukaguzi wa tiketi zetu kwa ‘zone’ ambayo nami ilinifikia tena
zone namba tatu huku nikiwa na tikiti yangu.
Tulikamilisha taratibu na kuingia ndani ya ndege tukafunga mikanda na
ilipofika saa 8:30 usiku safari ikaanza ya kukata anga na na
tukafanikiwa kufika saa 7 mchana ya siku ya pili na kutua katika
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Suvarnabhumi ambao ni mkubwa huku
ukiwa unapokea idadi kubwa ya ndege za kimataifa na wageni kutoka
mataifa mbalimbali.
Tuliposhuka tu, wahudumu tuliowakutana nao walianza na salama
Sawadikrapu, wote wakiinamisha mikono yao kwenye kifua na kuinama nami
nikajibu Sadika, kwa kuwa alikuwa ni mwanamama.
Lakini cha kuashangaza kila tulipokuwa tunapita pale uwanjani, raia wa
Thailand nyuso zao zilijawa na tabasamu kiasi kwamba hata mgeni
kujihisi nipo eneo salama na kila nikiulizwa swali na maofisa wa
uhamiaji pale uwanjani nalijihisi kwamba sina tatizo kwa kuwa hawakuwa
ni wenye kukunja uso kama tulivyozoea kwa askari wengine wawapo katika
majukumu yao.
Tulikamilisha taratibu na kuanza kutoka pale uwanjani, kwa kweli
ilikuwa ni safari nzuri huku wenyeji wetu wakiwa ni wenye furaha mno
kwetu wakati wote.
Tulifika hadi Hoteli ya Grande Centre Point na kupokewa na wahudumu
wenye tabasabu wakati wote huku nikiwa na shauku kubwa ya kujua kwa
undani kwa nini watu wake ni wakarimu wakati wote.
Mwenyeji wetu Dararat Weerapong, akatuchukua hadi katika moja ya
mgahawa na kupata mlo wa mchana, lakini wale wahudumu muda wote
wakizunguka kuhakikisha natimiziwa mahitaji yangu.
Siku zangu zote nilizokuwa Thailand nilipata maelezo kadhaa kutoka kwa
mmoja wa marafiki zangu Pratch Rujivanarom, akaniambia kwamba moja yautamaduni kwa watu wa Taifa la Thailand ni tabasamu wakati wote, kwanihata historia inaonesha kwamba Thailand ni nchi ya ‘tabasamu’.
Pia alikwenda mbali zaidi na kunieleza kwamba wananchi wa taifa hilo
wengi wao ni watu wachakarikaji si wa kukaa na kuletewa na hata pindi
wanapokuwa katika biashara zao, muda mwingi huongozwa na ukarimu
unaombatana na tamasabu kiasi cha kujenga imani kwa wateja wao wakati
wote.
“Tabasamu ni sifa kubwa kwetu kwani Thailand ni ‘Business Hub’ kwa
nchi zote za Asia ya Kusini. Ndio maana hii Bangkok ina watu asilimia
30 ya watu wote wa Thailand ambao kwa sasa wanakadiriwa kufikia zaidi
ya milioni 67.
“Lakini hata hivyo, hapa tumeweza kuendelea, tuna treni ya umeme
ambayo inachukua watu wengi mno, pia tuna barabara nyingi zikiwamo za
juu lakini zipo pia njia ya kulipia ‘By pass’, ambazo zimekuwa ni
msaada mkubwa mno,” anasema Rujivanarom.
Kidogo akanipeleka kwenye historia ya taifa hilo na kusema kuwa nchi
hiyo ilijulikana kama Uthai (Siam) ni nchi ya kifalme katika Asia ya
Kusini – Mashariki.
Imepakana na Laos, Kambodia, Malaysia na Myanmar.
Ina pwani kwenye Ghuba ya Uthai ya Bahari ya Kusini ya China, upande
wa Kusini na Bahari Hindi upande wa Magharibi. Nchi hiyo ina wakazi
zaidi ya milioni 67 hivyo, inashika nafasi ya 20 duniani.
Mji Mkuu na mkubwa ni Bangkok, ukiwa na wakazi zaidi ya milioni nane.
Nchi iliitwa rasmi Siam hadi mwaka 1939, tena kati ya 1945 na 1949.
Neno Thai linamaanisha ‘uhuru’ kwa Kithai, pia ni jina la kundi kubwa
la watu nchini ambao ni Wathai asilimia 75 – 85, mbali na
Wathai-Wachina asilimia 12.
Tangu Septemba 19, 2006 nchi imekuwa ikitawaliwa na kamati ya jeshi.
Jeshi ilipindua Serikali ya Waziri Mkuu Thaksin Shinawatra, bila
kumwaga damu. Viongozi wa kijeshi walipatana na mfalme kwamba
wataandaa uchaguzi mpya.
Nchini Uthai kuna lugha za asili 73 kati yake, Kithai ndiyo lugha rasmi.
Wathai walio wengi, asilimia 94.6 hufuata dini ya Ubuddha katika
madhehebu ya Theravada. Kusini, mpakani kwa Malaysia, kuna Waislamu
asilimia 4.6 na Wakristo ni asilimia 0.7.
Kwa hakika nimefika Thailand na kushuhudia kuwa ni nchi ya tabasamu
wakati wote huku maendeleo yakishika kasi.
Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO
0 Comments