Rubani azimia ghafla angani, Mwanafunzi wake aomba msaada wa maelezo jinsi ya kutua | ZamotoHabari.

Mwanafunzi wa mafunzo ya Urubani aitwaye Max Sylvester (29) kutoka nchini Australia amefanikiwa kutua ndege salama baada ya mwalimu wake kuzimia angani akiwa anamfundisha mwanafunzi huyo jinsi ya kurusha ndege.


Max amesema wakiwa angani, Alishangaa ghafla mwalimu wake akimlalia kwenye bega jambo ambalo lilimsitua na kuanza kumuamsha.

Alitumia dakika mbili kumuamsha lakini hakuamka, Ndipo alipoanza kuwapigia waongoza ndege wa uwanja wa ndege wa  Jandakot uliopo mjini Perth akiomba msaada wa maelekezo ya namna ya kutua ndege uwanjani hapo.

Max ambaye amejitambulisha kuwa ni baba wa watoto watatu, Amesema ilikuwa ni mara yake ya kwanza kufundishwa kwa vitendo namna ya kurusha ndege aina ya Cessna.

“Nilipatwa na hofu kidogo, Ila nikaona ni bora niombe maelekezo kutoka kwa Waongoza ndege uwanjani. Hili ni somo langu la kwanza, Nilishawahi kufundishwa namna ya kurusha ndege mara mbili tu na haikuwa aina hii ya ndege,“amesema Max kwenye mahojiano yake na waandishi wa habari baada ya kutua ndege hiyo.

Max Sylvester aliwahi kupata mafunzo ya kurusha ndege angani mara mbili chini ya uangalizi wa mwalimu wake ambaye alizimia na ilikua ndege aina nyingine.

Akielezea tukio lilivyotokea, Max amesema baada ya kufika katika anga la uwanja wa ndege wa Perth, Alikaa angani kwa takribani saa moja akifuata maagizo ya jinsi ya kutua, hatimae alifanikiwa kutua salama huku maafisa wa usalama na hali ya dharura pamoja na familia yake wakimsubiri.

Mwalimu wake baada ya kutua airport alipelekwa hospitali na Max alipongezwa na Mmiliki wa Chuo alichokuwa akisoma.

“Ndege haikuharibika hata kidogo. Kusema kweli alitua kama rubani mzoefu, Hii ndio ingekuwa ajali mbaya zaidi kwenye chuo chetu tangu mwaka 1980,” alisema Chuck McElwee, mmiliki wa chuo cha urubani cha Air Australia International ambacho ndio kimemuajiri rubani huyo aliyezimia.

Tukio hilo limetokea Jumamosi ya wiki iliyopita majira ya mchana, Ambapo mmiliki wa ndege hiyo amesema hakukua na taarifa yoyote ya kiafya kutoka kwa rubani.

Bongo5
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipo
BOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini