Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Vijana, Kazi na Ajira, Antony Mavunde akiongea na wataalam wa kilimo jijini Dar es Salaam jana kabla ya kuondoka kwenda Israel kwa mafunzo zaidi juu ya kilimo. Kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Mnyepe.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Vijana, Kazi na Ajira, Antony Mavunde pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Mnyepe wakiwakabidhi baadhi ya wataalamu hati za kusafiria.
Serikali imekamilisha zoezi la kuwapeleka wataalam 100 wa kilimo nchini Israel kujifunza mbinu bora na teknolojia za kisasa za kuendeleza kilimo cha umwagiliaji nchini.Akiongea na wataalam hao wakati wa hafla ya kuwaaga jana jioni, Jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Mnyepe alisema kuwa nafasi hizo za masomo ya kilimo nchini Israel zitatoa fursa kwa wataalam hao kuongeza ufanisi katika Sekta ya kilimo nchini na kukifanya kilimo kuwa na tija zaidi hapa nchini mara baada ya kukamilisha mafunzo hayo.
Aidha, Dkt. Mnyepe alibainisha kuwa, Tanzania na Israel wana uhusiano wa muda mrefu na umeendelea kuimarika siku hadi siku katika Sekta mbalimbali za kiuchumi na maendeleo nchini. Sekta hizo ni kama vile Kilimo, TEHAMA, Afya na mafunzo katika fani mbalimbali. Fursa za mafunzo zinazotolewa na nchi mbalimbali ikiwemo Israel zinasaidia kuongeza ujuzi kwa wataalam wetu nchini ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi.
"Kupitia uhusiano huo, tarehe 8 Novemba 2018, Rais Dkt. John Magufuli, alifanya mazungumzo na Mhe. Noah Gal Gendler, aliyekuwa Balozi wa Israel na baada ya mazungumzo hayo alitangaza kuwa Serikali ya Israel imeipatia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nafasi za mafunzo ya Kilimo yatakayofanyika nchini Israel kuanzia Septemba 2019 ambapo mara baada ya kutangazwa kwa fursa hizo Mhe Rais ilielekeza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuratibu upatikanaji wa nafasi hizo" Alisema Dkt. Mnyepe
Aliongeza kuwa, zoezi la uratibu wa kupata nafasi hizo ilifanyika kwa ushirikiano wa karibu na Wizara za Sekta ya Kilimo na Mafunzo nchini pamoja na Wizara na Taasisi zinazohusika na masuala ya uendelezaji wa ujuzi kwa vijana kwa lengo la kutumia fursa ya mafunzo hayo kuongeza uzoefu na kuwa ni chachu ya kuchochea ajira kwa vijana watakohitimu mafunzo hayo. Katika mchakato huo jumla ya wanafunzi 1440 waliomba nafasi hizo na kuchujwa hadi kufikia 100 ambao wameanza kusafiri kwenda nchini Israel.
Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Vijana, Kazi na Ajira, Antony Mavunde aliwataka wataalamu hao kuhakikisha kuwa wanatumia mafunzo hayo vyema ili kuweza kupata na kuweza kuanzisha shughuli mbalimbali za kilimo watakaporejea nchini.
"Kama mnavyofahamu, Israel ni moja ya mataifa yaliyopiga hatua kubwa ya Teknolojia katika Sekta ya Kilimo hivyo mafunzo haya ni fursa adhimu ya kuboresha sekta yetu ya kilimo ambayo ni muhimu katika uendelezaji wa viwanda. Ni matarajio ya serikali kuwa mafunzo haya yatawawezesha kuanzisha shughuli mbalimbali za Kilimo watakaporejea nchini, vinginevyo hakuna sababu ya ninyi kwenda" Alisema Mavunde.
Aliongeza kuwa fursa hiyo ni hatua kubwa ambayo itapelekea kupata ujuzi ambao utapelekea mapinduzi ya kilimo nchini. Niwakumbushe tu kuwa, sekta ya kilimo ni sekta ambayo hutoa ajira nyingi sana ambapo huchangia asilimia 12 katika pato la taifa,
"Ni matumaini ya serikali kuwa mtakuwa wataalam bora na wakuigwa katika matumizi ya ujuzi na uzoefu juu ya kilimo kwa maslahi ya taifa na kusaidia watanzania wengi zaidi,"Aliongeza Mavunde, huku akipongeza juhudi za Rais Magufuli ambazo alizofanya hadi kupatika kwa nafasi hizi za mafunzo.
Mafunzo hayo hutolewa kwa vitendo kwa wanafunzi kutoka nchi zinazoendelea kama vile Asia, Amerika ya Kusini na Afrika ikiwemo Tanzania, ambao tayari wanamsingi wa elimu ya masuala ya Kilimo, kwa madhumuni ya kuwaongezea ujuzi katika maeneo mbalimbali ya uzalishaji kama vile mbogamboga na matunda, mifugo, uongezaji thamani mazao, kutunza ubora, kutumia teknolojia ya kisasa kama vile umwagiliaji na usindikaji pamoja na ubunifu katika biashara ili kutumia vyema mnyororo wa thamani katika shughuli za kilimo.
Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO
0 Comments