Charles James, Michuzi TV
MKUU wa Wilaya ya Dodoma, Mhe Patrobas Katambi ameingilia kati mgogoro uliopo baina ya wafanyakazi wanaojenga miradi ya Soko, Stendi ya kisasa ya mabasi na eneo la michezo la Chinangali dhidi ya Kampuni ya Mohamed Builders inayosimamia miradi hiyo.
DC Katambi amechukua hatua hiyo baada ya wafanyakazi hao kuandamana kwenda kwenye Ofisi yake kudai haki zao za malipo kutoka kwenye Kampuni hiyo ambapo wanadai malimbikizo ya mishahara yao.
Wakizungumza na Mkuu huyo wa Wilaya ambaye alifika na kuzuia maandamano hayo, wafanyakazi hao kwa pamoja wamemueleza DC Katambi kuwa wamefikia hatua hiyo baada ya kuchoshwa na danadana za malipo ambazo wamekua wakipigwa na muajiri wao.
" Mheshimiwa DC sisi wananchi wako yapata mwezi wa nane huu unaenda hatujalipwa stahiki zetu, tukidai kwa nguvu wanatulipa kidogo kidogo na kututishia kutufukuza. Tunashangaa kwanini wanatufanyia hivi ilihali Serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi hii.
Unavyotuona hapa wengine hatuna hata fedha ya kula na Watoto wetu. Tunaomba uingilie kati na kusaidia tuweze kupata haki zetu, " Amesema mmoja wa wafanyakazi hao, Makwata Alfred.
Mfanyakazi mwingine Ramadhan Masha amesema kwa muda mrefu wamekua wakiangaika kufuatilia malipo yao lakini hakuna msaada wowote wanaoupata zaidi ya kutishiwa kufukuzwa kazi.
" Utaratibu ni sisi tulipwe fedha zetu kila siku lakini wao wamekua wakitucheleweshea wakabadilisha utaratibu tuwe tunalipwa kwa wiki na bado hiyo imekua ni tatizo. Tunaomba Mhe uingilie kati tuweze kulipwa haki zetu, " Amesema Masha.
Akijibu malalamiko hayo, DC Katambi amesema ofisi yake haijawahi kupokea kero za malipo kutoka kwa wafanyakazi hao na kuahidi kulishughulikia huku akitoa maagizo matano kwa Kampuni na kuitaka kufika ofisini kwake mara moja kueleza sababu za wafanyakazi hao kutolipwa.
" Ndugu zangu nimesikia kilio chenu, mimi siku zote niko upande wa wananchi, sitokubali kuona haki ya wananchi waliompigia kura Rais Magufuli ikipotea. Hivyo nawahakikishia nyinyi nyote mliopo hapa hakuna yeyote atakayefukuzwa kwa kudai haki yenu.
La pili kupitia viongozi wenu wa katika miradi yote mkae kwa pamoja mniletee barua inayohusiana na madai yenu, jambo la tatu madai ya NSSF nitamuita Meneja wa NSSF leo na mkandarasi kwa kuwa atakuepo wanieleze hizo fedha wanazowakata zinaenda wapi na mtazipataje ikitokea mmeacha kazi," Amesema DC Katambi.
Aidha ameahidi kusimamia ulinzi na usalama kwa wafanyakazi hao pamoja na kukaa kikao na wafanyakazi hao wote na uongozi wa Kampuni hiyo ili kujua mustakabali wao ili waweze kulipwa haki zao kwa haraka.
DC Katambi amewataka wafanyakazi hao kuacha kugomea miradi hiyo kwani kufanya hivyo siyo tu wanamkomoa mkandarasi huyo bali wanamuangusha Rais Magufuli ambaye amekua mstari wa mbele kuleta maendeleo jijini Dodoma.
" Ndugu zangu kila kazi ina changamoto yake, niwasihi msifanye migomo ya kuacha kufanya kazi. Niwaombe mkikwamisha hii miradi mjue mnaikwamisha Nchi siyo mkandarasi. Naombeni mrudi kazini mkaendelee na kazi wakati ambao Mimi nashughulikia malipo yenu," Amesema DC Katambi.
Baada ya kikao hicho wafanyakazi hao wamerudi kazini kuendelea na kazi na kumshukuru Mhe DC kwa kusikiliza kero zao huku wakimuomba aendelee kuwasimamia na kuwatetea.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe Patrobas Katambi akiwa na viongozi wa kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya hiyo wakizungumza na wafanyakazi wa Kampuni ya Mohamed Builders waliokua wakiandamana kushinikiza kulipwa kwa fedha zao.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe Patrobas Katambi akizungumza na wafanyakazi wa Kampuni ya Mohamed Builders baada ya kufika kuwasikiliza kero zao za malimbikizo ya mishahara wanayodai kwa waajiri wao
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Mhe Patrobas Katambi akizungumza na wafanyakazi wa Kampuni ya Mohamed Builders inayosimamia ujenzi wa miradi mitatu ya Soko, Stendi ya Mabasi na Eneo la Michezo la Chinangali ambao wamefanya maandamano kwenda kuonana na DC kutokana na kile walichodai kutokulipwa mishahara yao.
Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO
0 Comments