JAMII YASHAURIWA KUONDOKANA NA MILA POTOFU ZA KUAMINI KWAMBA CHANJO HUSABABISHA MADHARA KWA WATOTO | ZamotoHabari.

Na, Jumbe Ismailly IKUNGI 

JAMII imeshauriwa kuondokana na mila potofu na zilizopitwa na wakati za kuamini kuwa endapo mtoto akipatiwa chanjo ya ugonjwa wa Surua Rubela na Polio upo uwezekano wa kupata madhara katika siku za baadaye na haitaweza kumkinga na magonjwa yatakayomkabili.

Akiongea wakati wa Uzinduzi wa kampeni za chanjo ya kuzuia magonjwa ya Surua,Rubela na Polio uliofanyika kwenye Kituo cha Afya cha Ikungi,Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Huduma za jamii wa Halmashauri ya wilaya ya Ikungi,Abeli Richard Sui alisisitiza kwamba ni wakati muafaka kwa wataalamu wa Afya kwa kushirikiana na wanasiasa kwenda kuwahamasisha wananchi kwa kuwapatia elimnu sahihi ili waweze kuondokana na dhana hiyo potofu.

“Yapo mambo ambayo yapo katika jamii ambayo kwa umoja wetu sisi kama alivyosema mheshimiwa mgeni rasmi twende tuiathiri jamii kufahamu umuhimu wa hiki kwamba jamii kule wanaona mtoto akichanjwa pengine anaweza akapata madhara pale baadaye na wala si kwamba inamkinga na maradhi yatakayomkabili.”alisisitiza mwenyekiti huyo wa kamati.

Kwa mujibu wa Sui dhana hiyo ni potofu ambayo kwa umoja wao wanapaswa kuikemea ikiwa ni sambamba na kutoa elimu sahihi ili wananchi wa wilaya hiyo waweze kuelewa kikamilifu pamoja na kuondokana na dhana hiyo inayokwamisha kupeleka watoto kwenye chanjo hizo.

“Kwa hiyo twende kusambaza ujumbe huu,lakini mgeni rasmi tukuombe kwa wakati mwingine endelea kushiriki nasi kwani suala la huduma za jamii ni pana na lina mambo mengi kama nilivyotangulia kusema kwamba ili tufike mahali sasa huduma hizi zimfikie mlengwa kwa karibu ni lazima tuongeze vituo vya kutolea huduma.”aliweka bayana Mwenyekiti.

Naye Mwakilishi wa Wizara ya Afya,Honest Nyaki alitumia fursa hiyo kuwaomba wazazi na walezi wa watoto wenye sifa za kupatiwa chanjo ya magonjwa ya surua rubella na polio wawapeleke watoto wao kupatiwa chanjo.

Aidha Mwakilishi huyo alibainisha kwamba mzazi au mlezi yeyote yule ambaye hataweza kumpeleka mtoto wake kupatiwa chanjo atahesabika kufanya vitendo vya hujuma kwa watoto wao ambapo alitoa mfano wa hujuma hizo kuwa ni pamoja na kushindwa kuwapeleka watoto wao kupatiwa chanjo inayoendelea kutolewa nchi nzima.

Akizindua kampeni ya chanjo hiyo ya Surua Rubela na Polio,Mkuu wa wilaya ya Ikungi,Edward Mpogoro aliwapongeza wazazi pamoja na walezi wote waliojitokeza na kupeleka watoto wao kupata chanjo kwa kile alichodai kwamba wanatekeleza sera za Chama Cha Mapinduzi(CCM).

Akitoa taarifa fupi ya maandalizi ya chanjo ya magonjwa hayo,Mratibu wa chanjo wa Halmashauri ya wilaya ya Ikungi, Godeliva Mutasa aliweka bayana kwamba Halmashauri hiyo inatarajia kuchanja jumla ya watoto 48,245 kwa chanjo ya Surua Rubela na Polio na jumla ya watoto 23,833 wanatarajiwa kupatiwa chanjo ya polio.

“Magonjwa haya yanasababisha ulemavu,upofu pamoja na vifo kwa watoto kinga yake ni chanjo kabla ya mtoto hajaugua na tunategemea kutoa chanjo ya Surua Rubela kwa watoto wote walio katika umri wa miezi tisa mpaka miaka minne na miezi 11.”alifafanua Mratibu huyo.

Wilaya ya Ikungi,Mkoani Singida inatarajia kutoa chanjo ya Surua Rubela kwa watoto 48,245 wenye umri wa kati ya miezi 9 mpaka miaka 4 na miezi 11 wakati zaidi ya watoto 23,000 wenye umri wa mwaka mmoja na nusu mpaka miaka mitatu na nusu watapatiwa chanjo ya Polio.
 baadhi ya wazazi na walezi wa watoto wenye sifa za kupatiwa chanjo ya Surua Rubela na Polio wakiwa kwenye Kituo cha Afya cha Mji mdogo wa Ikungi wakishuhudia uzinduzi wa Kampeni ya chanjo ya Surua Rubela na Polio.


Baadhi ya wazazi na walezi wa watoto wenye sifa za kupatiwa chanjo ya Surua Rubela na Polio wakiwa kwenye Kituo cha Afya cha Mji mdogo wa Ikungi wakishuhudia uzinduzi wa Kampeni ya chanjo ya Surua Rubela na Polio.
 Mkuu wa wilaya ya Ikungi,Bwa.Edward Mpogoro akizindua kampeni ya chanjo ya Surua Rubela pamoja na Polio uliofanyika katika kituo cha afya cha Mji mdogo wa Ikungi.


Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini