Mkataba wa Harmonize, WCB Ulivunjika Tangu Mwaka 2016 Baada ya Kufunguka Macho | ZamotoHabari.



Harmonize amethibitisha kilichonong’onwa muda mrefu kwamba menejimenti ya Wasafi Classic Baby, maarufu kwa jina la WCB, ilimtaka staa huyo wa Umakondeni alipe Sh500 milioni aweze kung’oka.

Ametumbua jipu kwamba ilibidi auze nyumba zake tatu apate fedha za kuwalipa WCB. Kwamba yalikuwa masharti ya mkataba Harmonize akitaka kuondoka WCB, ailipe Sh500 milioni na gharama za utengenezaji wa nyimbo zote.


Kwa nini wamefika huko? Jibu ni vipengele vya mkataba (contractual terms) ambavyo Harmonize ameona havimtendei haki. Ameridhia kulipa kila dai ili awe huru.


Kwa nini alisaini mkataba kama aliona vipengele vinamnyonya? Jibu ni hili: Chifu Mangungo wa Msovero, Usagara (Kilosa ya sasa) alisaini mkataba na Karl Peters wa Ujerumani ulioandikwa Kijerumani. Akauza himaya yake na watu wake bila kujua.

Ni nyakati hizo, mkataba wa Mangungo na Peters katika zama za sasa, ungevunjika siku ambayo Mangungo alijua kile ambacho alikisaini. Kwamba haukuwa mkataba (makubaliano), bali ulaghai.


Hapa ndipo kwenye hoja. Kuna mkataba (makubaliano) yenye utashi wa pande zote zenye kusaini na ulaghai au shuruti. Wanasheria huliweka vizuri kwa lugha yao. Huita duress contracts, yaani mikataba isiyo na utashi au ufahamu.


Tafsiri ya duress ni nguvu, lazima au ushawishi wa kumfanya mtu atende jambo bila ridhaa yake. Mathalan, mtu anasaini mkataba akiwa ameshikiwa bunduki, anaambiwa asiposaini atauawa.

Anatekwa mwanaye, mkewe au mumewe, mzazi wake au ndugu yake, halafu anaambiwa asaini mkataba, vinginevyo mateka atauawa. Mikataba ya aina hiyo ni duress.



Kutokana na kesi mbalimbali na hukumu zake, duress imetanuka. Ulaghai kama wa Mangungo na Peters, umo ndani ya duress, kwamba mtu alisaini pasipo kuwa na ufahamu wa kutosha.

Kusaini mkataba na mtoto au mtu asiye na ufahamu wa kutosha kuhusu vipengele vya mkataba, hutafsiriwa kuwa aina nyingine ya duress.

Turejee mwaka 2015

Mwaka 2015, Harmonize alikuwa kijana mdogo. Asiye na fedha. Ndoto yake ilikuwa kuwa mwanamuziki. Anaishi mjini Dar es Salaam, Mmachinga. Lakini Diamond Platnumz ni staa aliyekaa juu ya nchi. Yes, Diamond was and still on top! Alikuwa na bado yupo kileleni!


Huwezi kupata picha ya duress katika mikataba ya wasanii kama hutavaa viatu vya msanii anayetaka kutoka au underground, na anayetamani kutoka kimuziki. Ukimuuliza Afande Sele alivyomuona Sugu enzi hizo akitaka asaidiwe kimuziki, akiwa mkweli, utaelewa maana yake.

Jicho la msanii underground kwa msanii aliyefanikiwa ni kama malaika wa pepo. Kwa mantiki hiyo, mwaka 2015, Harmonize ambaye hakuwa akijua chochote, alimuona Diamond kuwa ni malaika wa pepo yake.

Jiulize, siku ya kiyama, unaona jehanamu ilivyo. Halafu unaitwa na malaika wa pepo, anakwambia saini mkataba uingie, utapoteza muda? Tusiongopeane, utasaini harakaharaka na kuingia.

Ukishaingia peponi na kuijua pepo ilivyo, ndipo unaweza kumuona malaika wako wa pepo alikupiga. Kwamba ulistahili zaidi.


Kumbuka pia kuwa wakati unasaini mkataba wa kuingia peponi, utakuwa na furaha iliyopitiliza, umakini hautakuwepo. Utataka usaini ili ukajionee yaliyomo. Ufaidi simulizi za mito ya maziwa na asali.

Njoo kwa Harmonize. Hajui pepo ya muziki ilivyo ila alifahamu kuwa Diamond yupo peponi na ni malaika wa pepo. Akatokeza kumvuta peponi. Unadhani Harmonize angedengua?

Harmonize alipoambiwa asaini mkataba aingie kwenye pepo ya muziki, angelaza damu? Bila shaka, alisaini akiwa na furaha iliyopitiliza.

Mwaka 2015 akatoa “Aiyola”, jamii ikamjua. Mwaka 2016 “Bado” ilifuata kisha “Matatizo”. Mpaka hapo, Harmonize alikuwa ameshaijua pepo ya muziki. Hakuwa mshamba tena. Kipindi hicho angeambiwa asaini upya mkataba wake na WCB, kuna vipengele angevikataa. Kumbe sasa, kiuhalisia, mkataba wa Harmonize na WCB, kwenye fikra za Harmonize, ulivunjika tangu mwaka 2016.

Tafsiri nzuri ya mkataba wa duress ni ule ambao anayesaini, muda mrefu unaofuata akiambiwa asaini upya, lazima akatae. Ni kama Harmonize, bila shaka akili yake ya sasa inamwambia alikosea kusaini.


  • Dhambi ya mkataba


Mkataba ni makubaliano ya kisheria. Na asili ya mikataba ya muziki ni wajibu wa kila upande. Unachotoa na unachoingiza. Masharti lazima yawe sawa kuhusu mzigo ambao kila upande utabeba kwa kuvunja mkataba.

Mathalan, iliandikwa kuwa Harmonize alitakiwa kulipa Sh500 milioni na kurejesha gharama zote za nyimbo ambazo zilirekodiwa chini ya Wasafi ili kuvunja mkataba.

Sawa! Je, wajibu wa Wasafi kuvunja mkataba ni upi? Kama wao wangeamua kuachana na Harmonize, wangepaswa kumlipa nini? Mkataba wa masharti ya upande mmoja, ni aina nyingine ya duress. Ni u’Mangungo na u’Peters.


Kuna sharti la hovyo amelisema Harmonize. Eti kurejesha gharama za matengenezo ya nyimbo. Hii ya wapi? Wimbo umeshatoka, umefanya biashara, pande zote mbili zimefaidi matunda ya biashara iliyofanyika. Muda wa kuvunja mkataba, msanii anatakiwa kulipia gharama za wimbo? Harufu ya unyonyaji ipo hapa!

Mfano, “Kwangwaru” uliotoka Aprili 2018 umefikisha watazamaji zaidi ya milioni 50. Biashara kubwa imefanyika. Na mkataba wa muziki katika mgawanyo wa mapato, huzingatia uwiano wa mrabaha (royalty rates).

Kwa maana hiyo, kila mia iliyoingia, WCB walipata na Harmonize alipokea chake kulingana na makubaliano ya mgawanyo wa mrabaha. Mwaka mmoja na nusu baadaye, Harmonize ili awe huru, analazimika kulipia gharama za matengenezo ya wimbo.

Swali, WCB wanarejesha fedha ambazo waliingiza kutokana na wimbo huo? Haukuwa mkataba mzuri. Harmonize alisaini wakati huo kwa sababu alikuwa hajui kitu. Leo anafahamu kila kitu.

Kama ndivyo, sijui Harmonize kalipa kiasi gani, lakini leo hii, akiambiwa asaini, hatasaini.

Chipukizi wazingatie

Kampuni ya kusimamia muziki huwekeza katika maeneo ya aina mbili; label (utengenezaji na usimamizi wa muziki) na imprint (masoko ya muziki na mwanamuziki).

Kampuni kama Wasafi inapomchukua msanii, inabeba maudhui ya kutengeneza na kusimamia muziki pamoja na masoko. Hufanya hivyo kupata faida. Sio msaada!

Wasanii wengi chipukizi wanapochukuliwa na mastaa wakubwa, hudhani wanasaidiwa, hivyo hunyenyekea. Wafahamu kuwa hakuna recording company ya usamaria mwema. Husaka fedha.

Kampuni inapofikia hatua ya kukusainisha, maana yake huona faida ndani yako. Kwa hiyo hupaswi kwenda kikondoo, kudhani unasaidiwa. Ni biashara. Soma vipengele bila ushawishi, amua kwa maisha yako, tena, shirikisha wanasheria.

Pia recording company nyingi hutaka kummiliki msanii muda mrefu. Mikataba ya muziki huwa haiendi kwa umri, bali kazi.

Wasiseme unasainiwa kwa miaka 20, kama WCB na Harmonize, bali, mnatengeneza albamu ngapi au nyimbo ngapi. Siku hizi soko la kidigitali, zinaangaliwa nyimbo zaidi kuliko albamu.

Suge Knight alipomtoa Tupac jela mwaka 1995 na kumlipia dhamana ya dola milioni moja, Tupac hakusaini umri wa kukaa Death Row Records miaka mingapi, bali walisaini albamu tatu.

Februari 2014, 50 Cent, aliposaini mkataba na kampuni ya usambazaji ya Caroline, inayomilikiwa na taasisi ya Universal Music Group (UMG), alisema, alikuwa bado anadaiwa albamu moja na lebo ‘joint’ ya Shady-Aftermath, lakini alikubaliana kiroho safi na Dre pamoja na Eminem.


Kama Harmonize na Wasafi wangekubaliana idadi ya nyimbo au albamu, wala wasingeingia kwenye mgogoro. Wangeachana salama. Kama kungekuwa na idadi ya nyimbo anadaiwa, Harmonize angeingia studio kumalizia. Miaka 20 au 10 ya nini? Saini idadi ya nyimbo, zikitimia, kama kuna haja, mnasaini tena.


 By Luqman Maloto



Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipo
BOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini