NAIBU WAZIRI KWANDIKWA AWATAKA TEMESA KUJITANGAZA | ZamotoHabari.

Muonekano wa daraja la zamani la Ruaha Mkuu linalounganisha wilaya za Kilosa na Kilombero ambalo ujenzi wake unaendelea.
Muonekano wa barabara ya Kidatu-Ifakara Km 68.9 inayojengwa kwa kiwango cha lami na Mkandarasi M/s Reynolds Construction Company mkoani Morogoro.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya ujenzi), mhe. Elius John Kwandikwa (katikati) akikagua ujenzi wa barabara ya Kidatu-Ifakara Km 68.9 inayojengwa kwa kiwango cha lami na mkandarasi M/s Reynolds Construction Company mkoani Morogoro (wapili kushoto), ni Mtendaji Mkuu wa TEMESA Eng. Japhet Masele.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya ujenzi), mhe. Elius John Kwandikwa akiteta jambo na Mhandisi Mshauri wa M/s Nicholas O’ Dwyer and Co. Ltd anayesimamia ujenzi wa barabara ya Kidatu-Ifakara Km 68.9 na daraja la Ruaha Mkuu linalounganisha wilaya za Kilosa na Kilombero.
Muonekano wa barabara ya Kidatu-Ifakara Km 68.9 eneo la Mang’ula inayojengwa kwa kiwango cha lami mkoani Morogoro.

……………………

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya ujenzi), mhe. Elius John Kwandikwa ameutaka Wakala wa huduma za Ufundi na Umeme nchini (TEMESA), kuongeza kasi katika mkakati wake wa kuanzisha karakana katika ngazi za wilaya ili kuwezesha taasisi nyingi za umma na watu binafsi kupata huduma hizo kwa urahisi.

Akizungumza mara baada ya kukagua karakana mpya na ya kisasa katika wilaya ya Kilombero mjini Ifakara Naibu Waziri Kwandikwa amesema huduma hiyo itawapunguzia adha wananchi wa maeneo ya Mlimba, Ulanga, Malinyi na Ifakara kutembea umbali mrefu kufuata huduma za TEMESA mjini Morogoro.

“Ongezeni wigo wa huduma zenu za ufundi wa magari, mitambo na umeme, hakikisheni zinatolewa kwa wakati, ubora na unafuu ili mjiimarishe kimapato na kutoa fursa za ajira kwa vijana wengi zaidi”, amesisitiza Naibu Waziri Kwandikwa.

Amewataka TEMESA kununua vipuri kwa bei ya jumla ili kuwawezesha kutoza bei nafuu katika huduma zao na hivyo kuwavutia wadau wengi.

Naibu Waziri huyo amesisitiza umuhimu wa TEMESA kusimamia uwekaji wa mifumo ya umeme katika miradi ya ujenzi inayosimamiwa na Serikali ili kuifanya iwe imara na kuepusha majanga ya moto yanayoweza kusababishwa na uunganishaji holela wa umeme katika majengo ya Serikali. 

Naye Mtendaji mkuu wa TEMESA Eng. Japhet Masele amesema Wakala huo umejipanga kujenga karakana nne za kisasa katika wilaya za Same, Kahama, Simanjiro na Chato ili kuwapunguzia wananchi na taasisi za umma kutembea umbali mrefu kutafuta huduma hizo.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Kwandikwa amekagua ujenzi wa barabara ya Kidatu-Ifakara Km 68.9 kwa kiwango cha lami na daraja la Ruaha Mkuu na kumtaka mkandarasi M/s Reynolds Construction Company kutoka Nigeria anayejenga barabara hiyo kujipanga upya ili kukamilisha ujenzi huo kwa wakati.

Amesema kasi ya sasa hairidhishi na hivyo itachukua muda mrefu hivyo kumtaka mkandarasi huyo kujipanga upya na kuongeza nguvu kazi ili mradi huo ukamilike kwa wakati.

Kukamilika kwa wakati kwa barabara ya Kidatu-Ifakara Km 68.9 inayopita katika eneo lenye uzalishaji mkubwa wa miwa na mpunga licha ya kurahisisha huduma za uchukuzi, kilimo na biashara pia kutakuza uchumi wa wananchi wa mkoa wa Morogoro.


Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini