NAIBU WAZIRI MABULA AAGIZA KUTAMBULIWA WAMILIKI WA MAENEO WASIOTAKA KUMILIKISHWA HAI | ZamotoHabari.

Na Munir Shemweta, WANMM HAI

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameagiza ofisi ya Ardhi Kanda ya Kaskazini kuwatambua wamiliki 2,019 wa maeneo katika halmashauri ya wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro ambao hawataki kumilikishwa maeneo yao na kupatiwa hati.

Agizo hilo linafuatia Dkt Mabula kuelezwa na Afisa Ardhi Mteule wa Halmashauri hiyo Jacob Muumba kuwa pamoja na halmashauri hiyo kupima viwanja 2,019 lakini wamiliki wake hawajajitokeza kumilikishwa jambo lililomstua Naibu Waziri wa Ardhi.

‘’Watu wana maeneo lakini hawataki kumilikishwa, wanakwepa kitu gani maana hawalipi kodi’’ alisema Dkt Mabula.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ameagiza wale wote wenye maeneo yaliyopimwa katika halmashauri ya wilaya ya Hai kutambuliwa na kujulikana wanamiliki maeneo yao toka muda gani na kusisistiza kuwa hakuna atakayeachwa na zitaangaliwa hatua za kuchukua.

Katika hatua nyingine Dkt Mabula ameagiza kufuatiliwa kwa maeneo yote ya biashara ya hamashauri ya wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro ambayo hayalipiwi kodi ya pango la ardhi ili yaweze kulipiwa.

Alisema, pamoja na halmashauri hiyo kuwa na maeneo ya kibiashara yaliyopimwa kama vile Stendi na Soko lakini hakuna hata eneo moja lililolipiwa kodi ya pango la ardhi hivyo basi Mkurugenzi wa halmashauri lazima ahakikishe analipia maeneo yake ya biashara.

‘’DED wa Hai hujawahi kulipia kodi ya pango la ardhi ya Stendi na Soko wakati vimepimwa na kama halamashauri hailipi je mtu wa kawaida itakuaje? alihoji Dkt Mabula.

Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya aliagiza kupatiwa taarifa ya maandishi kuhusiana na halmashauri ya wilaya ya Hai kushindwa kulipia kodi ya pango la ardhi katika maeneo yake ya biashara na kumuahidi Naibu Waziri Mabula kuwa atalifanyia kazi suala hilo katika kipindi cha muda mfupi pamoja na lile la wamiliki wa maeneo wasiotaka kumilikishwa.

Hata hivyo, Ole Sabaya alimueleza Dkt Mabula kuwa pamoja na changamoto mbalimbali katika sekta ya ardhi wilayani humo Ofisi yake kwa kushirikiana na idara ya ardhi imeweza kuzipatia ufumbuzi kero za ardhi za wananchi wa wilaya hiyo zipatazo 350 kati ya 432 zilizowasilishwa wakati wa siku maalum ya ardhi maarufu kama Ardhi Day. 

Wakti huo huo, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amekagua ujenzi wa mradi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro unaojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa ofisi hiyo ambapo alilitaka Shirika la Nyumba kukamilisha ujenzi katika muda uliopangwa.

Kwa mujibu wa Kaimu Meneja wa Shirika la Nyumba mkoa wa Kilimanjaro Mradi huo unaogharimu takriban shilingi milioni 910 unatarajiwa kukamilika Desemba mwaka 2019.
 Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akioongozana na Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro Lengai Ole Sabaya kuelekea kukagua jengo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro wakati wa ziara yake ya siku moja katika wilaya hiyo kukagua miradi inayosimamiwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
 Mhandisi anayesimamia ujenzi wa jengo la ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro kutoka Shirika la Nyumba la Taifa Peter Mwaisabura akimueleza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula Maendeleo ya Ujenzi wa Ofisi hiyo jana wakati Naibu Waziri alipofanya ziara kukagua mradi huo. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya.
  Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akifafanua jambo wakati alipokwenda kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa jengo la Ofisi ya Mkuu wa  Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro unaosimamiwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) jana.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akikagua jalada la ardhi katika ofisi ya ardhi ya halmashauri ya wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro jana wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi. Kulia ni Afisa Ardhi Mteule wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai Jacob Muumba.(PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)



Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini