Charles James, Michuzi TV
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza Walimu nchini kuhakikisha wanaanzisha mchakato wa kufanya mazoezi asubuhi kwa wanafunzi kabla ya kuingia darasani ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza
Mhe Waziri Mkuu pia ameziagiza Wizara za Kilimo, Michezo kushirikiana na Wizara ya Afya katika mapambano ya kutokomeza magonjwa yasiyoambukiza kwa kikubwa yamekua yakichangia vifo vya watoto na vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa.
Waziri Mkuu ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akizindua Wiki ya Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Yasioambukiza sambamba na Mpango wa Taifa wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza yaliyoenda sambamba na siku ya kisukari duniani.
Amewataka wananchi kuchukua hatua stahiki za kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza ikiwa ni pamoja na kubadili tabia na mwenendo wao wa ulaji wa vyakula kwa kuongeza ulaji wa mbogamboga, matunda.
Amesema kila mtu ana wajibu wa kudhibiti matumizi ya vilevi kama sigara na pombe; kuhamasisha jamii kushiriki mazoezi au shughuli za nguvu; kuzingatia mlo unaofaa hasa kwa kuondoa au kupunguza chumvi, sukari na mafuta. “Tujipange kukabiliana na madhara mengine yatokanayo na uharibifu wa mazingira na tabianchi.”
Waziri Mkuu amesema wananchi wanatakiwa wajenge utamaduni wa kufanya mazoezi angalau dakika 30 mara tatu kwa wiki.
“Katika eneo hili, niweke msisitizo kwa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuendeleza utaratibu wa mazoezi uliozinduliwa na Makamu wa Rais Mama Samia Suluh Hassan.
“Tuendelee kuhamasisha kuanzisha na kujiunga kwenye vikundi vya mazoezi ya pamoja ambavyo husaidia sana kuleta hamasa ya kufanya mazoezi. Tutumie vikundi vya joggingvilivyopo kwenye kata na mitaa au vijiji vyetu ili kupata mwendelezo wa jitihada zao," Amesema Mhe Majaliwa.
Ameziagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinatenga na kuyaendeleza maeneo ya wazi katika kila kata au mitaa ili pamoja na shughuli nyingine wananchi pia watumie maeneo hayo kwa ajili ya kufanya mazoezi.
“Kwa upande wa wanafunzi kuanzia sasa kabla ya kuingia darasani wawe wanakimbia mchaka mchaka ili waweze kujiimarisha kiafya jambo ambalo litawaepusha na magonjwa yasiyoambukiza," Amesema.
Amesema magonjwa yasiyoambukiza yamekuwa tishio kwenye jamii na ulimwenguni kote, takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa mwaka 2016 zinaonesha kuwa magonjwa hayo yanachangia zaidi ya vifo milioni 41, sawa na asilimia 71 ya vifo vyote milioni 57 vilivyotokea mwaka 2016.
“Taarifa za mwaka 2013 za Shirika la Maendeleo Duniani (UNDP) zinaonesha kuwa, pamoja na changamoto hizo za kiafya, magonjwa yasiyoambukiza yanaathiri sana nyanja nyingine za maisha. Inakadiriwa kuwa katika kipindi cha miaka 20, kuanzia mwaka 2013 gharama zitokanazo na magonjwa haya zitafikia Dola za Marekani trilioni 47.”
Kwa upande mwingine Mhe Waziri Mkuu amewataka watanzania kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 24 kwa kuchagua viongozi waadilifu na wazalendo huku akionya kuchukuliwa hatua kali za kisheria kwa yeyote atakayejaribu kuvuruga amani..
“Vikundi vya ulinzi wa jadi au vya ulinzi binafsi au vya mashabiki wa vyama vya siasa havitaruhusiwa kutumika kwenye maeneo ya mikutano ya kampeni au maeneo ya uchaguzi.”
Waziri Mkuu amesema kuwa vyombo vya Ulinzi na Usalama hususan Jeshi la Polisi, Mgambo wenye sare na Maafisa wanaosimamia ulinzi vitatumika kuhakikisha kunakuwepo na utulivu wakati wa kampeni na uchaguzi.
Awali,Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema magonjwa yasiyoambukiza yanajumuisha magonjwa ambayo hayawezi kusambazwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine.
Ameyataja magonjwa hayo kuwa ni pumu, shinikizo la juu la damu, kisukari, saratani, siko seli, magonjwa ya akili, ajali, magonjwa mengi ya macho, kinywa, masikio, pua na koo. “Magonjwa haya yamekuwa yakiongezeka duniani kote na kuathiri nyanja zote za kimaisha.”
Waziri Ummy amesema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita Tanzania ilishuhudia ongezeko la idadi ya watu waliopatiwa huduma za magonjwa yasiyoambukiza kutoka wagonjwa milioni 3.4 kwaka 2016 hadi wagonjwa milioni 4.2 mwaka 2018, ilkiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 24.
Kwa upande wao, wadau wa masuala ya afya wameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuongeza kiwango cha bajeti ya dawa kutoka sh. bilioni 31 hadi sh. bilioni 270.
Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO
0 Comments