ELIMU YA KUJIKINGA, KUUTAMBUA UGONJWA WA EBOLA YATOLEWA KWA VIONGOZI KUTOKA KADA MBALIMBALI JIJINI DAR | ZamotoHabari.

Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV

WIZARA ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam imeamua kuandaa mafunzo maalumu yanayohusu namna ya kutambua na kujikinga na ugonjwa wa ebola kwa makundi ya kada mbalimbali ikiwemo ya wakuu wa wilaya, wakurugenzi, makatibu tawala, viongozi wa dini na wasanii.

Lengo na kutolewa mafunzo hayo kwa makundi hayo ni kuhakikisha yanajengewa uelewa wa kutosha kuhusu ugonjwa huo ili wawe mabalozi ambao watakuwa na jukumu la kutoa elimu hiy kwa jamii ya Watanzania kama hatua muhimu za kukabiliana na ugonjwa huo hatari waebola ambao kimsingi haujaingia nchini lakini baadhi ya nchi jirani ikiwemo ya Jamhuri ya Democrasia ya Congo ugonjwa huo upo na umesababisha watu kupoteza maisha.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam,Mratibu wa utoaji elimu ya ugonjwa wa Ebola ambaye pia ni Mratibu wa elimu ya Afya katika Shule za Mkoa wa Dar es Salaam Dk.Ndeniria Swai amesema sababu za kukutana na viongozi hao wa makundi hayo ni kuendelea kuoa elimu kuhusu ugonjwa wa Ebola, ambao bado haujaingia nchini Tanzania lakini nchi za jirani na tanzania zimekuwa zikiripotiwa kuwa na wagonjwa wengi wa ebola hususani nchi ya Congo.

"Nchi ya Congo ambayo imekuwa na wagonjwa wa Ebela imekuwa na muingilia mkubwa na nchi ya Tanzania na hiyo inatokana na raia wengi wa nchi ya Congo wamekuwa wakija jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kununua bidhaa.Watanzania nao wanatoka Dar es Salaam na kwenda Congo kufanya biashara.

"Wapo wengine ambao wanakwenda kwa ajili ya kupeleka magari ya mafuta na wengine wamekuwa wakipeleka vyombo vya moto na wakati huo huo wapo raia wa Congo ambao wanakuja nchini Tanzania kwa ajili ya mikutano mbalimbali na Watanzania nao wanakwedna huko kwenye mikutano, hivyo muingiliano ni mkubwa na hivyo nchi yetu kuwa hatarini kupatwa na ugonjwa huo,"amesema Dk.Swai.

Amesema hivyo Wizara ya Afya, imeona kuna kila sababu sasa Watanzania wote wakapewa elimu kuhusu ugonjwa Ebola na kuongeza wizara hiyo inapenda kila mtanzania mwenye uwezo wa kuelewa afahamu kuhusu ugonjwa wa ebela, afahamu dalili na kubwa zaidi afahamu namna ya kujikinga ili kuepuka maambukizi.

"Hivyo leo hii tumeita viongozi mbalimbali wakiwamo wakurugenzi , wakuu wa wilaya, makatibu tawala , tumeita viongozi wa afya ngazi ya halmashauri , viongozi wa dini, wanamichezo , wasanii, wakurugenzi wa taasisi wanaosimamia usafiri wa anga, majini nchi kavu, mameneja wanaosimamia vituo vya mabasi ubungo na wadau wengine.Tunapenda kila mmoja kupata nafasi hiyo ili wawe mabolozi ambao watatoa elimu sahihi kuhusu ugonjwa wa Ebola.

"Elimu hiyo itahusu kuwa na uelewa kuhusu nini maana ya ebola nini, inapatikana vipi, namna gani ya kutoa taarifa ya ugonjwa huo katika sehemu sahihi na jinsi gani mgonjwa wa ebola anaweza kusaidiwa.Hivyo viongozi wa Serikali watapeleka ujumbe, viongozi wa dini nao watapeleka ujumbe, tunataka wasanii nao wawe sehemu ya kutao elimu hiyo kwa kutunga nyumba,"amesema.

Ameongeza kuwa mlipuko wa kumi tangu ugonjwa umeanza lakini nchi yetu ina kila sababu ya kuchukua hatua ili kujikinga ebola isiingie nchini na hiyo itawezekana kwa kuhakikisha elimu sahihi kuhusu ugonjwa huo inafika kwa jamii ikiwa sahihi.

Kwa upande wake Oscar Kapela ambaye anatoka Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Kitengo cha elimu ya afya kwa umma ambacho kipo chini ya idara ya kinga amesema lengo na mafunzo hayo ni kuhusu elimu ya ebola, lakini ni mafunzo ambayo yanalenga kushirikisha jamii ili iweze kuchukua tahadhari ya ugonjwa huo.

"Lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha jamii inakuwa na uelewa mpana kuhusu ugonjwa wa ebola , jinsi gani ya kujikinga,tunafahamu kuwa kinga ni bora kuliko tiba. Elimu imezidi kutolewa kwa njia mbalimbali, na waandishi wamekuwa wakifikisha elimu hiyo, elimu tunataka ifike nyumba kwa nyumba,"amesema.

Wakati huo huo Simon Kadogosa ambaye anatoka Taasisi ya Tanzania Red Cross amesema wameungana na Serikali katika kampeni hiyo ya kutoa elimu ya uelewa kuhusu namna ya kujikinga na ugonjwa ebola kwa kuanza na viongozi 

"Red cross tuko pamoja na Serikali kwa kila hatua kuhakikisha lengo linafikiwa na ukweli baadhi ya nchi jirani zinakabiliwa na ugonjwa huo , hivyo lazima jamii ya watanzania wajue na wafahamu namna ya kujikinga kwa kuchukua tahadhari,"amesema na kuongeza ugonjwa huo upo nchi za Congo, sudan, sera lioni pamoja na baadhi ya nchi ambazo zimeendelea kupata shida ya Ebola.

Kwa upande wake Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Mashariki na Pwani Usharika wa Tegeta Wazo Hili jijini Dar es Salaam Richard Hananja amesema mafundisho kuhusu ugonjwa wa ebola ni muhimu kwao ili nao kutoa elimu hiyo kwa waumini wao.

Amesema katika Tanzania ya viwanda, yeye kama kiongozi wa dini, kiwanda chake ni waumini ambao anawaongoza Kanisani na hivyo lazima waumini hao wawe wenye afya iliyobora na hivyo elimu ambayo wameipata watahakikisha inafika kwa jamii wanayoingoza.

Naye Mjumbe wa Kamati ya Amani Mkoa wa Dar es Salaam ambaye ni kiongozi wa dini kutoka Kigamboni Seif Muyenga amesema kwa kweli mafunzo hayo ni muhimu katika maisha ya mwanadamu na wao kama viongozi wa dini na wajumbe wa kamati ya amani ni lazima wayapokee mafunzo hayo kwa mikono miwili na kufanyia kazi.

"Kama mwili hauna amani maana yake hata amani kwenye jamii haitapatkana. Mwili ukiumwa akili nayo haitafanya kazi na hivyo amani haitakuwepo.Hivyo baada ya kupata mafunzo hayo tutakwenda kuyafikisha kwa waumini na jamii kwa ujumla .Kwa kweli ugonjwa huo ni mkubwa na tishio kwa ulimwengu, hivyo kinga ni bora kuliko tiba.

"Na moja ya kinga ni mafunzo ambayo yametolewa ambayo yatasaidia jamii kujikinga, gharama za kutibu ugonjwa huo ni kubwa, hivyo nitoe pongezi kwa walioandaa mafunzo haya kwetu kwan wamefanya jambo lenye tija kubwa , nasi tutaenda kuisambaza elimu hii kwa wengine na nitoe ombi tunaomba mafunzo hayo yatolewe kwa makundi mengine ambayo kwa leo hawakuwpo hapa,"amesema.
 Mratibu wa utoaji elimu ya ugonjwa wa Ebola ambaye pia ni Mratibu wa elimu ya Afya katika Shule za Mkoa wa Dar es Salaam Dkt.Ndeniria Swai akielezea namna Ugonjwa wa Ebola unavyoambukizwa kwa binadamu na njia za kujikinga na ugonjwa huo hatari
  Mratibu wa utoaji elimu ya ugonjwa wa Ebola ambaye pia ni Mratibu wa elimu ya Afya katika Shule za Mkoa wa Dar es Salaam Dkt.Ndeniria Swai akielezea namna mgonjwa aliyekumbwa na Ugonjwa wa Ebola anavyokuwa baada ya kuathiriwa na ugonjwa huo na hatua za kuchukua kuhakikisha ugonjwa huo hausambai kwa mtu mwingine.
 Mkurugenzi wa jiji la Dar es Salaam,Bi Spora Liana akizungumza jambo huku akiwashukuru viongozi mbalimbali wa Dini na kada nyinginezo waliofika kwenye Mafunzo maalumu yanayohusu namna ya kutambua na kujikinga na ugonjwa wa Ebola . 

Viongozi kutoka Kada mbalimbali wakiwemo viongozi wa Dini wakimsikiliza kwa makini  Oscar Kapela ambaye ni mratibu Kitengo cha elimu ya afya kwa umma ambacho kipo chini ya idara ya kinga katika Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Mratibu Kitengo cha elimu ya afya kwa umma ambacho kipo chini ya idara ya kinga katika Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Oscar Kapela akifafanua jambo kwenye mkutano huo uliondaliwa makhususi kwa mafunzo maalumu yanayohusu namna ya kutambua na kujikinga na ugonjwa wa ebola kwa makundi ya kada mbalimbali ikiwemo ya wakuu wa wilaya, wakurugenzi, makatibu tawala, viongozi wa dini na wasanii. 
 Viongozi kutoka Kada mbalimbali wakiwemo viongozi wa Dini wakifuatilia yaliyokuwa yakijiri kwenye mkutano huo muhimu katika kutoa Mafunzo maalumu yanayohusu namna ya kutambua na kujikinga na ugonjwa wa ebola kwa makundi ya kada mbalimbali ikiwemo ya wakuu wa wilaya, wakurugenzi, makatibu tawala, viongozi wa dini na wasanii. 
 



Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini