MTANGAZAJI kutoka nchini Kenya ambaye ni mzazi mwenza wa staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Tanasha Donna Oketch, amelamba shavu dodo, ikiwa ni mwezi mmoja tu tangu ajifungue mtoto wa kiume, Naseeb Junior.
Malengo ya Tanasha kwenye tasnia ya muziki yanaelekea kutimia baada ya kuachia nyimbo mbili na sasa ameanza kula mashavu ya ubalozi.
Tanasha mwenye umri wa miaka 24 aliyekuwa akitangaza Kituo cha Redio cha NRG cha Mombasa, Kenya, amesaini mkataba wake wa kwanza wa ubalozi na kampuni ya bidhaa za urembo hasa mikufu ya madini mbalimbali.
“Nina furaha kutangaza kuwa mimi ni Balozi wa Ley_ Jewellers. Kwa mahitaji yako ya dhahabu, almasi na madini mengine kwa asilimia mia moja, Ley_Jewellers ndiyo suluhisho lako,” ametangaza Tanasha kupitia ukurasa wake wa Instagram baada ya kuondoka Dar kwa Mondi na kutimkia nyumbani kwao nchini Kenya.
Tanasha alitumbukia kwenye muziki Aprili, mwaka huu huku wengi wakiamini Diamond au Mondi ndiye aliyemvutia kuingia humo.
Miezi miwili baadaye, aliachia wimbo wake wa Nah Easy ambao ulipokelewa vizuri na mashabiki kwenye Mtandao wa YouTube.
Hivi karibuni, Tanasha alifunguka kuwa, yupo mbioni kuachia projekti yake mpya ya muziki.
Stori: Neema Adrian, Dar
Tembelea Website ya Nyimbo za Injili Africa. Pakua na Kusikiliza bure bila malipo
BOFYA HAPA
0 Comments