Na Ripota Wetu, Tunduru
MKURUGENZI wa Halmashauri ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Gasper Balyomi,amewaonya Waandishi wasaidizi wa Daftari la kudumu la wapiga kura kujiepusha na tabia ya ulevi wakati wote wa zoezi hilo.
Alisema, ulevi na ukiukwaje mwingine wa maadili ya utumishi wa umma unaweza kuharibu na kukwamisha zoezi hilo ambalo ni muhimu kwa mustakabali wa maendeleo ya Nchi yetu.
Balyomi ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati akifungua semina ya siku mbili kwa Waandishi Wasaidizi 200 wa Daftari la wapiga kura ambao wameteuliwa kufanya kazi ya kuandikisha wananchi kwenye zoezi la Uboreshaji wa Daftari la kudumu la wapiga kura katika vijiji na kata mbalimbali za wilaya ya Tunduru.
Alisema,zoezi hilo linahitaji sana mtu makini,muadilifu,anayejituma na muaminifu,kwa hiyo haitakuwa rahisi kwa mtu mlevi kutekeleza majukumu hayo na kusisitiza kuwa,hatosita kumuondoa kituoni Mwandishi atakayebainika kunywa pombe saa za kazi na atakayeondoka katika kituo chake bila ruhusa maalum.
Alisema, Taifa linawategemea sana kutekeleza jukumu hilo na kuchaguliwa kwao kutokana na uwezo na ujuzi mkubwa walioonesha wakati wa semina ya kuwajengea uwezo kwani kila mmoja amepata elimu ya kutosha itakayomwezesha kutekeleza wajibu na majukumu yake katika kufanikisha zoezi hilo muhimu.
Balyomi amewaeleza Waandikishaji hao kuwa, serikali ina Imani na wale wote waliobahatika kushiriki katika zoezi la Uboreshaji wa Daftari la kudumu la wapiga kura, kwa hiyo uzoefu wao katika kuratibu na kusimamia utekelezaji wa Uandikishaji wa wapiga kura utasaidia sana ambapo amewataka kuwasaidia wale wasiokuwa na uzoefu.
Aidha,amewaomba Waandishi hao kutoa ushirikiano kwa wadau wengine wakiwemo mawakala wa Vyama vya Siasa ambao watafika katika vituo vya kujiandikisha, kwani sheria ya Uchaguzi imewapa haki kufuatilia zoezi zima litakavyokwenda ili kuleta uwazi katika zoezi zima.
Hata hivyo, amewataka mawakala hao kutoingilia kazi za watendaji pindi wanapotekeleza wajibu,badala yake kuwa waangalizi wa kazi na zoezi zima la uandikishaji inavyofanyika katika vituo.
Kwa upande wake, Afisa Uchaguzi wa Jimbo la Tunduru Kusini na Tunduru Kaskazini Abbas Ali alisema, waandikishaji wote watapelekwa katika vituo vyote 216 vilivyotengwa kwa ajili ya kufanikisha zoezi hilo.
Alisema, lengo la kuwapatia mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo katika kutekeleza majukumu waliyopewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ili kuhakikisha zoezi hilo linafanyika vizuri.
Kwa mujibu wake,Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC)inafanya maboresho katika Daftari la kudumu la wapiga kura kwa ajili ya kuboresha taarifa mbalimbali za wananchi na linalenga hasa kwa wale waliohama kutoka sehemu moja kwenda nyingine,kuwaondoa waliokosa sifa na waliotimiza umri wa miaka 18 ambao walikosa sifa ya kujiandikisha mwaka 2015.
Mwenyekiti wa Mafunzo Bartzal Mkwera alisema, mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo namna ya kujaza fomu na kutumia mashine za BVR na yatakwenda sambamba na kuanza zoezi zima la Uandikishaji katika Daftari la wapiga kura katika tarafa saba za wilaya ya Tunduru.
Mkwera alisema,jumla ya vijana 241 kati ya 255 wameteuliwa kufanya kazi hiyo ambapo alisisitiza kuwa wako tayari kwa ajili ya kutekeleza jukumu hilo la Kitaifa
Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO
0 Comments