Msibomoe Majengo Haya ya Afya Mliokwisha Jenga – Serikali | ZamotoHabari.


 Naibu Katibu Mkuu Dkt. Dorothy Gwajima, akizungumza na timu ya Afya ya Manispaa ya Songea hawapo pichani
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dkt. Jairy Khanga, akizungumza eneo la Zahanati ya Mtakanini katika Halmashauri ya Namtumo mkoani Ruvuma.
Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Mtakanini, Magreth Pastory akitoa ufafanuzi juu ya maamuzi waliyoyafikia na kamati ya kituo katika kukiendeleza kituo hicho na mipango iliyopo.
Naibu Katibu Mkuu akiwa ameambatana na baadhi wa Wajumbe kutoka TAMISEMI na Mkoa wakikagua Jengo ambalo lilikuwa linabishaniwa juu ya hatma yake.
(Picha na OR-TAMISEMI)
……………
Na. Atley Kuni, Namtumbo: RUVUMA
Serikali imezitaka Halmashauri ambazo zilipelekewa fedha kwaajili ya ujenzi na upanuzi wa Vituo vya Afya pamoja na Zahanati kuacha mara moja mipango yakubomoa baadhi ya majengo yaliyokuwepo hapo awali na badala yake wayafanyie tathmini ya kina na ikiwezekana wayafanyie maboresho.

Rai hiyo imetolewa mkoani Ruvuma na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, anayeshughulikia Afya, Dkt. Dorothy Gwajima akiwa njiani akitokea Mikoa ya Songwe na Rukwa alipokwenda kwa shughuli za kikazi kukagua  miradi mbali mbali ya afya kwenye mikoa hiyo.

Dkt. Gwajima, amefikia hatua hiyo akiwa katika Zahanati ya Mtakanini iliyopo katika Halmashauri ya Namtumbo mkoani Ruvuma, ambapo Zahanati hiyo ilipelekewa kiasi cha shilingi milioni 400 kwaajili ya upanuzi wa kituo hicho lakini tayari ilikuwa imesha anza ujenzi wa jengo la uzazi.
Halmashauri hiyo baada yakupokea fedha, yalitokea malumbano yakutokuelewana kwa baadhi ya viongozi wa eneo hilo na kutaka kubomoa jengo hilo kwa madai kuwa lilikuwa tofauti na ramani   zilizo tolewa na ofisi ya Rais TAMISEMI kwa ujenzi wa vituo vya afya na zahanati.

“Kuyatelekeza majengo ambayo yalisha jengwa hapo awali au kuyabomoa bila kufanya tathmini ya kina itakuwa nikupoteza fedha za serikali, hivyo wito wetu Ofisi ya Rais TAMISEMI, tunaielekeza Mikoa na Halmashauri kama kuna majengo yalishajengwa waanze kwakuyafanyia tathmini na yanayoweza kurekebishika basi yafanyiwe hivyo na sio kuyatelekeza au kuyabomoa”, alisema Dkt. Gwajima.

Kwa upande wake Mratibu wa ujenzi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Shaban Sonda, alisema Zahanati hiyo ya Mtakanini ilipokea fedha hizo ili kufanya upanuzi wa kituo lakini kwakuwa tayari walikuwa na jengo la uzazi ni vema fedha hizo zifanye maboresho sambamba na kujenga majengo mengine yaliyo kusudiwa ikiwapo jengo la upasuaji.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dkt. Jairy Khanga alisema, Mkoa huo ulipokea kiasi cha shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya upanuzi wa Zahanati za Mtakanini, Matimila pamoja na Magagula, ambapo amedai kuwa, nguvu kubwa itaelekezwa kwenye majengo ya Wodi ya uzazi, upasuaji pamoja na maabara lakini pia nyumba za watumishi kulingana na mahitaji kwa kila Zahanati.

Kwa mujibu wa Mganga mfawidhi wa kituo cha Mtakanini, Tabibu Magreth Pastory, alisema kituo cha Mtakanini kwa sasa kinahudumia zaidi ya watu 300 hivyo upanuzi wa kukifanya kuwa kituo cha Afya umekuja kwa wakati muafaka.

Ofisi ya Rais TAMISEMI, imeendelea kuboresha miundombinu ya Afya na huduma zake kote nchini, shabaha ikiwa nikuhakikisha nchi inakuwa na watu wenye afya njema watakao shiriki ujenzi wa taifa kwa shughuli za maendeleo na kuifikisha nchi katika uchumi wa kati ifikapo 2025.


Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini