TBS yawonya Wafanyabiashara wa Vyakula na vipodozi | ZamotoHabari.

Na Chalila Kibuda,Globu ya Jamii

SHIRIKA LA Viwango Tanzania (TBS), imesema hakuna bidhaa ya chakula au vipodozi itakayoruhusiwa kuingia kwenye soko la Tanzania kama haijasajiliwa au kuthibitishwa ubora wake na shirika hilo.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Saalam  na Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt Athuman Ngenya, kwenye hafla ya utoaji wa leseni na vyeti vya ubora 96 kwa wazalishaji wa bidhaa mbalimbali nchini ambao wamekidhi viwango vya ubora

Alisisitiza kwamba ni lazima majengo ya kuzalisha, kuhifadhi au kuuzia chakula, vipodozi pamoja na vyombo vinavyobeba bidhaa hizo ikiwemo magari ya kubebea nyama  yawe yamesajiliwa na Shirika hilo, ndipo yataruhusiwa kutumika.

Alisema majukumu ya shirika hilo ni pamoja na usajili wa vyakula, vipodozi na majengo kwa mujibu wa marekebisho ya Sheria ya Viwango na mabadiliko Sheria ya Fedha Namba 8 ya mwaka 2019.

Kwa upande wa vyeti na leseni zilizotolewa, Dkt. Ngenya alisema  zimetolewa kwa wazalishaji wa bidhaa wakubwa, wa kati na wadogo baada ya mifumo inayotumika kuzalishia bidhaa zao kuthibitishwa na kukidhi matakwa ya viwango kwa kipindi cha  Oktoba hadi Desemba, mwaka jana.

Alisema zimetolewa leseni na vyeti 27 kwa wajasiriamali wadogo na moja ni kutokana na ubora wa mifumo. Dkt.Ngenya aliwataka wazalishaji wa bidhaa mbalimbali nchini kuhakikisha wanazalisha bidhaa zinazokidhi matakwa ya viwango vya ubora  kwa mustakabali ya kulinda afya za watumiaji wa bidhaa hizo ndani na nje ya nchi.

Alisema leseni na vyeti hivyo vilivyotolewa kwa wazalishaji hao, vitazisaidia bidhaa zao kuongeza imani kwa umma juu ya ubora wa bidhaa wanazozizalisha, kukubalika sokoni na kupata faida ya kushindana na kuingia katika soko la Afrika mashariki pasipo kufanyiwa vipimo zaidi.

"Natoa na pongezi kwa Wazalishaji aliofanikiwa kupata vyeti na leseni za ubora  muwe mabalozi wazuri kwa kuzingatia matumizi ya viwango ili kuweza kutimiza malengo ya ujenzi wa Tanzania ya viwanda," alisema na kuongeza;

"Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli inaendelea kuwahudumia wajasiriamali kwa kupata huduma za TBS bila malipo ya gharama za ukaguzi na upimaji."

 Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania Dkt.Athuman Yussuf Ngenya akipewa maelezo kuhusu bidhaa zilizozalishwa na wajasiriamali waliopata alama ya ubora mapema jana katika hafla ya utoaji vyeti iliyofanyika makao makuu ya TBS Ubungo.TBS  ilitoa jumla ya leseni 96 kati ya hizo leseni 27 ni wajasiriamali wadogo na leseni 1 ni ya mfumo. Leseni hizi ni majumuisho kwa kipindi cha mwezi oktoba mpaka Disemba mwaka 2019.


Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini