Wanafunzi zaidi 1,000 wa mkoani Katavi waliomaliza elimu ya msingi na hawajachaguliwa kuendelea na sekondari wanatarajiwa kujiunga na Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Msaginya ili kuwawezesha kupata ujuzi utakaowasaidia kuendesha maisha yao hapo baadaye.
Akizungumza mkoani humo wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi wa ukarabati na ujenzi wa miundombinu ya sekta ya elimu, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako ameupongeza mkoa huo kwa uamuzi waliochukua wa kuhakikisha wanafunzi wote waliomaliza darasa la saba na hawakuchaguliwa kuendelea na masomo wanajiunga na chuo hicho ili kujipatia ujuzi kwani wanafunzi hao bado ni wadogo kuachwa mitaani bila kuwa na ujuzi wowote.
“Uamuzi wa kuwachagua wanafunzi hao kujiunga katika chuo hiki cha Msaginya ni mzuri kwani unawapa fursa ya kujipatia ujuzi na kuwaondoa mitaani ambapo wangeweza kujiingiza katika makundi hatarishi na kupata mimba za utotoni kwani wangekuwa wapo tu mitaani bila ujuzi wowote wa kuwasaidia kuendesha maisha yao,” amesema Waziri wa Elimu.
Waziri Ndalichako amesema ubunifu uliofanywa na uongozi wa Mkoa ni wa busara kwani pamoja na kuwasaidia vijana kujipatia ujuzi lakini umewezesha kukifanya chuo hicho kutumika kwani katika baadhi ya maeneo ambayo kuna vyuo kama hivyo idadi ya udahili wa wanafunzi ni ndogo ukilinganisha na miundombinu iliyopo katika eneo husika na amewataka viongozi wengine katika maeneo mbalimbali nchini kuhamasisha vijana kujiunga katika vyuo vya ufundi ili kujipatia ujuzi.
Profesa Ndalichako amesema chuo hicho ni kati ya vyuo 54 vilivyohamishiwa katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia mwaka 2016 kutoka Wizara ya afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na Watoto huku vikiwa na miundombinu ya majengo iliyochakaa. Wizara baada ya kuvipokea iliamua kwa makusudi kuvikarabati na kujenga majengo ambayo hayakuwepo ili kuviweka katika hali nzuri ya utoaji wa elimu bora.
“Katika Chuo hiki wanafunzi watakaojiunga watasoma katika mazingira mazuri majengo yamekarabatiwa yako Vizuri , kuna walimu waliobobea katika kufundisha fani zote zinazotolewa katika chuo hiki. Huvyo naamini watakapomaliza hapa watakuwa na ujuzi tofauti na wale walioshia darasa la saba na kukaa tu nyumbani,” amesisitiza Profesa Ndalichako.
Aidha, Waziri huyo amesema ili kuongeza nafasi zaidi na miundo mbinu ya kufundishua na kujifunzia katika chuo hicho Wizara inajenga majengo mapya kwa ajili ya karakana nne, mabweni na jengo la Utawala sambamba na kufanyia ukarabati majengo ya zamani na kwamba lengo la kutoa mafunzo katika Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi ni kuchochea maendeleo katika maeneo mbalimbali kwa kutoa mafunzo yanayoendana na mazingira wanaoishi katika eneo husika ili washiriki katika kujenga uchumi wa nchi.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Juma Homera amesema Uongozi wa mkoa wake baada ya kuona serikali imewekeza kiasi kikubwa cha fedha katika kujenga na kukarabati miundombinu wakadhamiria kuongeza wanafunzi wengi zaidi ili kutumia vizuri uwekezaji huo kwa faida ya vijana na wananchi wa Katavi katika kuwapatia ujuzi na maarifa yatakayowasaidia katika kuendesha maisha yao ya kila siku.
“Wanafunzi tunaowaleta hapa ni 1,027, pamoja na lengo la kuwapatia ujuzi lakini pia tupo kwenye mkakati wa kuondoa tatizo la mimba za utotoni na kuondoa na wapiga debe kwa sababu mtoto anapomaliza darasa la saba wengine wanakuwa wadogo hawana kitu kingine cha kufanya zaidi ya kuingia katika makundi haya ambayo hayana tija katika maisha yao, hivyo tunawatengeneza ili waweze kujitegemea,” amesema Mkuu wa Mkoa.
Naye Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Msaginya, Injinia Petro Mwita ameishukuru serikali kwa kuvikumbuka vyuo hivyo na kuvifanyia ukarabati mkubwa ,unaokwenda kubadilisha muonekana pamoja na kuboresha mchakato wote wa ufundishaji na ujifunzaji katika chuo hicho.
Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Msaginya ambacho miundombinu yake ya majengo na maji safi na maji imeharibika kwa muda mrefu inafanyiwa ukarabati na kujengewa mingine kwa zaida ya shilingi milioni miatano.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akikagua ujenzi wa jengo la utawala katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Msaginya kilichopo wilayani Mpanda Mkoani Katavi
Mkuu wa Mkoa wa Katavi Juma Homera akizungumza na wananchi wa mkoa huo wakati wa ziara ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akikagua mabomba katika bweni linalojengwa katika shule ya sekondari ya wasichana Mpanda mkoani Katavi.
Jiunge Grupu la Mishono ya Vitenge VITENGE MISHONO
0 Comments