MADIWANI WATAKIWA KUTATUA KERO ZA WANANCHI KATIKA KATA ZAO KWA WAKATI | ZamotoHabari.

Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Lindi, Mohamed Lihumbo akiongea katika Mkutano wa mafunzo ya haki za binadamu na utawala bora yaliyotolewa na THBUB kwa kushirikiana na Taasisi ya Haki Maendeleo kwa Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi yaliyofanyika Mkoani Lindi, Februari 7, 2020. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Lindi, Judica Sumari na Kushoto ni Kamishna wa THBUB, Mhe. Amina Talib Ali.

Sehemu ya Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi wakifuatilia kwa umakini mafunzo ya haki za binadamu na utawala bora yaliyotolewa na THBUB kwa kushirikiana na Taasisi ya Haki Maendeleo.
Mkurugenzi wa Sheria kutoka THBUB, Nabor Assey akisisitiza jambo kwa Madiwani (hawapo pichani) katika Mkutano wa mafunzo ya haki za binadamu na utawala bora yaliyotolewa na THBUB kwa kushirikiana na Taasisi ya Haki Maendeleo, Februari 7, 2020.



Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Lindi, Mohamed Lihumbo (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, Viongozi wa THBUB na wawakilishi wa Taasisi ya Haki Maendeleo. Wa kwanza kulia waliokaa ni Mwakilishi wa Taasisi ya Haki Maendeleo, Wilfred Warioba, wa pili kulia ni Kamishna wa THBUB, Amina Talib Ali. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa sheria-THBUB, Nabor Assey na Wa pili kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, Judica Sumari. 
 
 
Na Mbaraka Kambona,

Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi wametakiwa kutatua kero zinazowakabili wananchi katika maeneo yao ya kazi kwa wakati ili kupunguza migogoro isiyokuwa ya lazima.

Kauli hiyo ilitolewa na Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Amina Talib Ali alipokuwa akifungua mafunzo ya haki za binadamu na utawala bora kwa madiwani hao yaliyotolewa na THBUB na taasisi ya Haki Maendeleo mkoani Lindi Februari 7, 2020.

Kamishna Amina aliwaeleza madiwani hao kuwa wananchi wana kero na malalamiko mengi ambayo yanahitaji kutatuliwa na viongozi, na wao ndio viongozi waliokaribu na wananchi kuweza kutatua kero zao.

Aliendelea kuwaeleza kuwa wasiwaache wananchi wanahangaika na kero zao mpaka wakakata tamaa wakati madiwani wapo, washughulike na kero zao ili wananchi wajenge imani kwao.

“Tusiwaache wananchi mpaka wakakata tamaa na sisi, tuwashughulikie, tusikae mpaka Mhe. Rais John Magufuli aje kutatua kero hizo, rais atafanya mangapi? tusimbebeshe mzigo usio muhusu, tumechaguliwa na wananchi kuwaongoza, hivyo tuwafanyie kazi kwa lengo la kuwapa ahueni ya matatizo yao”, alisema Amina

Aliendelea kuwasisitiza madiwani hao kuwa sio kila jambo linapaswa kupelekwa Mahakamani au Polisi, bali vipo vyombo kama THBUB ambavyo kazi yake ni kusuluhisha migogoro, madiwani wawaelimisha wananchi kutumia vyombo hivyo ili kusaidia kutatua kero zao.

“Kwa kutambua umuhimu wa vyombo vya usuluhishi, serikali iliamua kuvianzisha na kuvipa mamlaka ya kuisaidia serikali kutatua migogoro mbalimbali nchini, waheshimiwa madiwani waelimisheni wananchi katika maeneo yenu wapi pa kwenda kupata msaada pindi wanapokuwa na malalamiko yao”, alisisitiza

“Wasaidieni na waelimisheni wananchi kutambua haki zao na wajue wapi pa kwenda kupeleka malalamiko yao ili yashughulikiwe, sio kila jambo liende mahakamani, kuna mengine yanaweza kumalizwa na vyombo vya usuluhishi”, alieleza Amina

Aidha, katika hatua nyingine, Amina aliwakumbusha madiwani kuwa mwaka huu ni wa uchaguzi mkuu hivyo ni muhimu kuwaelimisha wananchi kuhusu haki na wajibu wao wa kushiriki katika mchakato mzima wa uchaguzi kwa amani.

Amina aliwahimiza madiwani kuwaelimisha wananchi ili wajue umuhimu wa kutekeleza haki yao ya kidemokrasia ya kuchagua na kuchaguliwa, na ni muhimu kufanya hivyo kwa mustakabali mzuri wa taifa.

“Mkawahimize wananchi pia kujiepushe na vitendo visivyofaa, wazingatie sheria na taratibu zilizowekwa na serikali na kuendelea kubaki kama raia wema na kushiriki shughuli mbalimbali za kujiletea maendeleo yao bila usumbufu wowote”, aliongeza Kamishna

Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, Mohamed Likumbo aliwasisitiza madiwani kwenda kuyatumia mafunzo hayo waliyopatiwa na THBUB kwa kushirikiana na taasisi ya Haki Maendeleo kwenda kuwaelimisha wananchi kuhusu haki zao na kushiriki kuwasidia wananchi kutatuta migogoro mbalimbali inayowakabili.

“Katika maeneo yetu kuna migogoro ya aina mbalimbali hususani migogoro ya ardhi, tukamie ujuzi huu tulioupata leo kwenda kuwasaidia wananchi kutatua migogoro yao kwa kufuata taratibu na sheria zilizowekwa”, alisema Meya


APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini