TANZANIA TUIFIKIRIE VAR, NI GHARAMA LAKINI ITATUFAA... | ZamotoHabari.



Ni maoni yangu kama Mdau wa Michezo na Mwandishi wa Habari za Michezo kutoka Tanzania, kwa Soka letu lilipofikia sasa na utata wa maamuzi uliopo katika Soka hili la Bongo, sina shaka wala ubishi tuifikirie Video Assistant Referee (VAR) ijapokuwa ni gharama kuiendesha.

Kwa hakika VAR itatusaidia kufika mbali na itawasaidia Waamuzi wetu wanaochezesha Soka lenyewe, naamini pia itaondoa utata na hata kupunguza makosa hasa wanayokutana nayo Waamuzi wanaoamua michezo mbalimbali hususan ile ya Ligi Kuu Soka Tanzania Bara (VPL).

Kama tunavyoona ulimwenguni katika Dunia ya kwanza namaanisha barani Ulaya, VAR imeondoa utata kwa kiasi kikubwa kwenye michezo ya Ligi mbalimbali zikiwemo Ligi maarufu na bora duniani Ligi Kuu za Uingereza (EPL), Hispania (La Liga) na nyingine nyingi tu.

Sina shaka wala hakuna ubishi kumekuwa na manung'uniko kwa baadhi ya Wadau wa Soka nchini kuwa VAR inaondoa uhondo katika mchezo, la hasha hili tusiliangalie wala kulitilia maanani sana. Kwa wenzetu wa Dunia ya kwanza (Ulimwenguni) wanaitumia VAR kama kawaida bila kujali kupoteza muda wala kuondoa uhondo wa mchezo husika, Je sisi ni akina nani tunaopinga hili?

Naendelea kusema na kuwaza kwa Mamlaka husika zinasosimamia mchezo wa Mpira wa Miguu nchini, VAR kwa Soka letu la Tanzania tuifikirie ijapokuwa ni gharama kuitumia katika mchezo mmoja. Sijui pengine baadae tunapoendelea tunaweza kuona umuhimu wake licha ya gharama zake lakini bado nawaza nakusema tuifikirie basi hata kwa michezo muhimu ya Ligi lakini michezo yote ya Ligi Kuu ni muhimu.

Utata wakuamua OFFSIDE kwa Waamuzi wetu, Mashabiki wa Soka wanasema ni Sheria mojawapo ya Soka ngumu zaidi katika zile Sheria 17 za Soka zilizowekwa na Shirikisho la Kandanda Ulimwenguni (FIFA), kwa hakika huenda ikawa kweli ni Sheria ngumu kuitafsiri kwa Waamuzi wetu lakini kwa wenzetu (Ulaya) wanasaidiwa na VAR kutatua changamoto hiyo ya tafsiri ya Sheria hiyo wao wanaangalia pande (Angle) zote kuhakikisha kama ni Offside au la.

Utata mwengine ni MAGOLI yanayofungwa bila kugusa Nyavu yaani kuvuta mstari wa goli, hii nayo ni sehemu nyingine ya utata katika Soka letu la Tanzania, lakini kwa wenzetu hakuna utata huo, VAR lazima ichukue nafasi kuwasaidia Waamuzi, kwa kweli inapendeza mnoo.

Sijajua kwa Ligi kubwa barani Afrika hasa kule Uarabuni kama kuna matumizi ya VAR lakini mwaka jana tulishuhudia moja ya Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League) kati ya Esperance de Tunis ya Tunisia na Wydad Casablanca ya Morocco ambapo ulizuka utata mpaka Bingwa wa Michuano hiyo kushindwa kupatikana kwa wakati, Fainali iliyopigwa mwezi May, Bingwa kutangazwa mwezi August mwaka 2019.

Kwa maoni yangu, VIDEO ASSISTANT REFEREE ikija nchini na hata barani Afrika kwa ujumla nadhani Utata wote utaisha katika Soka letu na hata zile shutma za Waamuzi wetu hazitakuwepo wala kupata nafasi bila kujali kuondoa uhondo wa mchezo wa Soka nakupoteza muda.


APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini