Usajili wa Line za Simu wafikia 71.6% | ZamotoHabari.

Tunakushauri kutumia APP yetu ili kusoma kwa urahisi ZAMOTOHABARI APP Sasa ipo Playstore, ili ku-download BOFYA HAPA.

Na. Immaculate Makilika - MAELEZO

Juma la laini za Simu milioni 31.4 sawa na asilimia 71.6 zimesajiliwa kwa alama za vidole hadi kufikia Februari 2 mwaka huu.

Akizungumza leo, Bungeni jijini Dodoma, wakati wa akihitimisha Bunge la 18, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema kuwa zoezi la usajili wa laini za simu kwa alama za vidole ni endelevu na uzimaji wa laini za simu unaendelea.

Aidha, Waziri Mkuu aliwataka wananchi kwenda kusajili laini zao mara baada ya kupata namba ama kitambulisho cha uraia kutoka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ili kuepuka usumbufu wa kusitishiwa huduma za mawasiliano.

“Ninatoa wito kwa NIDA wasogeze huduma za kutoa namba za vitambulisho karibu na wananchi kwa kadiri inavyowezekana. Lengo ni kutoa fursa kwa wananchi wengi zaidi kupata namba za vitambulisho kwa ajili ya kuwawezesha kusajili laini zao za simu na vilevile, kupata Vitambulisho vya Taifa kwa matumizi mengine muhimu” alisema Waziri Mkuu Majaliwa

Katika hotuba yake hiyo ya kuhitimisha Mkutano wa 18 wa Bunge, Waziri Mkuu Majaliwa alizungumzia maeneo mengine ambayo kumekuwepo Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kuyaboresha.

Akizngumzia kuhusu viashiria vya uwepo wa nzige nchini Mhe. Majaliwa alisema kuwa Serikali inafuatilia kwa karibu na kubaini endapo kuna viashiria au uwepo wa nzige hao sambamba na kuendelea kujipanga vizuri katika kudhibiti tishio hilo la nzige wa jangwani pamoja na visumbufu vyote vya mazao vitakavyotokea katika msimu huu wa kilimo.

Waziri Mkuu alisema kuwa hadi kufikia Januari 30, mwaka huu upatikanaji wa mbegu za kilimo ulikuwa tani 71,155 kati ya hizo, tani 58,509 zimezalishwa hapa nchini, tani 5,175 zimeingizwa kutoka nje ya nchi na tani 7,469 ni bakaa ya msimu wa 2018/2019.

Pia upatikanaji wa mbolea hadi kufikia Januari 30, mwaka huu umefikia tani 410,499 sawa na asilimia 70. Aidha, kwa kuwa mbolea hizo hutumika kulingana na hatua za ukuaji wa mazao, Serikali inaendelea kuhakikisha asilimia 30 iliyobaki inapatikana na kusambazwa kwa wakulima kwa wakati.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeendelea na zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa awamu ya kwanza ambapo hadi kufikia Februari, 2 mwaka huu imekamilisha uandikishaji wa wapiga kura katika kanda ndogo kumi na mbili kati ya kumi na nne zilizopangwa katika ratiba ya uboreshaji wa awamu ya kwanza.

“Nitumie nafasi hii kutoa wito kwa Tume kuongeza kasi ya uandikishaji. Kadhalika, natoa rai kwa wananchi kutumia haki yao hiyo ya kikatiba na kujitokeza kwa wingi kwa lengo la kuboresha taarifa zao na kujiandikisha upya kwa wale wenye umri wa miaka 18 au watakaofikisha umri huo ifikapo Oktoba, 2020” alisema Waziri Mkuu Majaliwa

Waziri Mkuu Majaliwa ameahirisha Bunge hadi tarehe 31 Machi, 2020 siku ya Jumanne



APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini