Mwalimu huyo alikutwa ameuawa kwa kunyongwa eneo la mpakani la Sirari wilayani Tarime akiwa ndani ya gari lake, huku mtoto anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka mitano naye akikutwa ndani ya gari hilo akilia.
Akizungumza na Mwananchi jana kuhusu kifo hicho, kamanda wa Polisi kanda Maalum ya Tarime/Rorya, William Mkondya alisema mpaka sasa chanzo cha mauaji hayo hakijajulikana, ingawa inasadikiwa aliuwawa kwa kunyongwa, huku waliomnyonga wakiwa bado hawajafahamika.
Alisema mwili wa mwalimu Rose aliyeuawa usiku wa Januari 31, 2020 ulikutwa ndani ya gari yake, “Tunaendelea na uchunguzi wa kina kuwanasa waliohusika na mauaji haya; uchunguzi huu tunaufanya kwa kushirikiana na wenzetu wa Kenya,” alisema Kamanda Mkonda.
Wakati wa uhai wake, marehemu Rose alikuwa akifundisha shule ya msingi Sirari ambapo mwalimu mkuu wa shule ya msingi Sirari, Kenedy Mniko alisema alipokea taarifa za kifo hicho kwa njia ya simu kutoka kwa mmoja wa walimu wa shule hiyo.
“Baada ya kufika eneo la tukio tulitoa taarifa Polisi upande wa Kenya ambao walifika na kulivuta gari la marehemu lililokuwa liko mtaroni ndipo tulipomtambua kuwa ni mwalimu mwenzetu aliyekuwa akifundisha darasa la kwanza,” alisema Mniko.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana wa CCM (UVCCM) Wilaya ya Tarime, Godfrey Francis aliomba Serikali kupitia vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina kuwabaini wahusika na kuwachukulia hatua za kisheria. Tukio hilo limelotokea ikiwa imepita miezi miwili tangu mwalimu mwingine Justine Ogigo kuuawa kwa kuchomwa mkuki shingoni.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments