Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wa Tatu kutoka Kushoto akizungumza na Uongozi wa Chuo cha Muziki wa Nchi za Jahazi {DCMA} kilichopo Mtaa wa Mizingani pembezoni mwa Fukwe ya Forodhan.
Mkurugenzi Mkuu wa Chuo cha Muziki wa Nchi za Jahazi {DCMA} Bibi Alessia Lombardo Kushoto akimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi muelekeo wa Chuo hicho wa hapo baadae.
Mkufunzi wa Chuo cha Muziki wa Nchi za Jahazi {DCMA} Kassim Ali Basalamu akimueleza Balozi Seif changamoto zinazokikabili Chuo hicho kwa wakati huu.
Mwalimu Mkuu wa Chuo cha Muziki wa Nchi za Jahazi {DCMA} Mohamed Othman akielezea Mfumo wa Chuo cha CDMA kinavyotoa Mafunzo wa Watoto wenye mahitaji Maalumwa Skuli ya Kisiwandui.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kulia akiupongeza Uongozi wa DCMA Kwa juhudi unazochukuwa wa kufinyanga Vijana katika Tasnia ya Muziki wa Taarab.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Zanzibar itaendelea kupata umaarufu katika maeneo mbali mbali Duniani kupitia Muziki wake wa Taarab ambao umekuwa na mvuto wa kipekee hasa kwa wale wanaoamua kuufuatilia ili kujiburudisha.
Alisema Taasisi zinazosimamia masuala ya Muziki Nchini bado zina wajibu na jukumu la kuhakikisha Sanaa hiyo muhimu kwa Jamii inalindwa, inakuzwa na kuendelezwa kwa vile mbali ya kuburudisha lakini pia husaidia Taaluma kupitia Kazi hiyo muhimu inayotoa Ajira kwa kundi kubwa la Vijana.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati wa mazungumzo yake na Uongozi wa Chuo cha Muziki wa Nchi za Jahazi {DCMA} kilichopo Mtaa wa Mizingani pembezoni mwa Fukwe ya Forodhan alipokutana nao Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inafarajika kwa kuwa na Chuo kinachofundisha Muziki wa Taarab uliopata maarufu tokea Karne ya 18 katika Mwambao wa Afrika ya Mashariki, Kusini na hata Ulimwenguni kwa kutumia Lugha ya Kiswahili inayozidi kukuza Utamaduni wake.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi wa Chuo hicho cha Muziki wa Nchi za Jahazi {DCMA} kwa jitihada unazochukuwa wa kufinyanga Vijana katika Tasnia hiyo ya Taarab ikiwa ni Tanuri la kupata Ajira katika vikundi mbali mbali vya Muziki mara wamalizapo Mafunzo yao.
“ Chuo cha Muziki cha Nchi za Jahazi kinastahiki kuungwa mkono na Washirika wa Maendeleo kutokana na kuwa Tanuri la kuwafinyanga Vijana ili kuingia katika Ajira kupitia Tasnia na Muziki wa Taarab”. Alisisitiza Balozi Seif
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alizishauri na kuziomba Taasisi na Washirika wa Maendeleo kukiunga mkono Chuo hicho wakati Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiangalia mazingira na kutafuta mbinu zitakazosaidia kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazokikabili Chuo hicho.
Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Chuo cha Muziki wa Nchi za Jahazi {DCMA} Bibi Alessia Lombardo alisema Wahitimu wapatao 170 humaliza Mafunzo yao Kila Mwaka tokea kilipoanzishwa Chuo hicho Mnamo Mwaka 2002 kikiwa na Miaka 18 sasa.
Bibi Alessia alisema Chuo hiko kimebarikiwa kupata Wataalamu wa kujitolea kutoka Mashirika na Taasisi mbali mbali za Kitaifa na Kimataifa ambao hutoa Mafunzo kwa Wafanyakazi na Wanafunzi wa chuo hicho.
Alisema Mwanafunzi anayepitia Mafunzo ya Chuo hicho anapomaliza Taaluma yake lazima awe na ujuzi na uwezo kamili utakaomuwezesha kubadilishana mawazo na Msanii mwenzake popote atakapoamua kwenda Duniani katika masuala ya Muziki.
Mkurugenzi Mkuu huyo wa Chuo cha Muziki wa Nchi za Jahazi {DCMA} alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba uwezo huo ndio uliyoonyesha wazi kwa Wasanii wa Chuo hicho kupata mialiko mbali mbali nje ya Nchini wa kushiriki kwenye Warsha, Matamasha pamoja na Maonyesho ya Muziki Kimataifa.
Bibi Alessia Lombardo alifahamisha katika muelekeo wa baadae wa kukijengea uwezo zaidi wa Ufundishaji Chuo hicho umelenga kutoa Mafunzo yake katika Ngazi ya Cheti na Stashahada kupitia Mfumo wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi Tanzania {NACTE}.
Alisema Uongozi wa Chuo kupitia Bodi yake umeshatayarisha Mitaala kamili itakayostahiki kufundishwa kwa mfumo huo wa Nacte lakini kinachosubiriwa kwa wakati huu ni ukamilishwaji wa Taratibu zinazohusika kwa ajili ya kuanza mfumo huo.
Nao kwa upande wao Mwalimu Mkuu wa Chuo hicho Mohamed Othman pamoja na Wakufunzi wenzake Kassim Ali Basalamu na Hassan Mahenge walisema kwa mbali ya jukumu lao chuoni hapo lakini pia hutenga muda wa kutoa Mafunzo kwa Wanafunzi wenye mahitaji Maalum katka Skuli ya Msingi ya Kisiwandui.
Walisema mafunzo hayo Maalum yalikwenda sambamba na kuwapatia mafunzo ya Muziki wana Sanaa wa Kikundi cha Taraabu kilichopo Mahonda Mkoa Kaskazini Unguja.
Hata hivyo Wakufunzi hao walimuomba Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kutumia nafasi yake itakayowezesha kupatikana kwa Taasisi na Mashirikia yatayokiunga Mkono Chuo hicho kutokana na kumalizika kwa zaidi ya Mwaka Mmoja sasa ufadhili waliokuwa wakiutegemea.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments