Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Bw. Hargeney Chituturo akizungumza wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kuelimisha jamii kuhusu ugonjwa wa Corona Maafisa Ustawi na Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Arusha, katika ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha jana tarehe 28/03/2020.
Maafisa Ustawi na Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Arusha wakifuatilia mada zilizokuwa zikitolewa wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kuelimisha jamii kuhusu ugonjwa wa Corona katika ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha jana tarehe 28/03/2020.
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya jamii Wizara ya Afya Bw. Patrick Golwike akitoa mada ya namna ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona kwa Maafisa Ustawi na Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Arusha, katika ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha jana tarehe 28/03/2020.
Afisa Ustawi wa Jamii Mkuu kutoka Wizara ya Afya Bi. Zakia Mohamed akitoa mada kuhusu ugojwa wa Corona kwa Maafisa Ustawi na Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Arusha, katika ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha jana tarehe 28/03/2020.
Dkt. Meshack Chinyuli akitoa mada kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kuelimisha jamii kuhusu ugonjwa wa Corona kwa Maafisa Ustawi na Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Arusha, katika ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha jana tarehe 28/03/2020.
Picha Zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW
………………………………………………………
Wizara ya Afya kupitia Idara kuu ya maendeleo ya Jamii imeanza kutoa mafunzo kwa Wataalamu wa Ustawi wa Jamii pamoja na Maendeleo ya Jamii kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kuelimisha Jamii kuhusu ugonjwa unaoenezwa na Virusi vya Corona.
Akifungua mafunzo hayo kwa maafisa wa Wilaya na kata zote za Mkoa wa Arusha jana tarehe 28/03/2020 jijini Arusha, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Bw. Hargeney Chitukuro amewataka kutumia fursa hiyo kuwaelimisha wananchi kwa usahihi kuhusu maambukizi na namna ya kujikinga na ugonjwa wa Corona bila hofu.
Bw. Chitukuro amesema kuwa, tangu ugonjwa huo ulipoingia Mkoani Arusha, mafunzo mbalimbali yameshatolewa kwa wataalamu na kuwaelekeza namna ya kuelimisha jamii jinsi ya kujikinga.
“Katika kipindi cha takribani wiki mbili tangu ugonjwa huu uingie tayari tumeshatoa mafunzo kwa wataalamu wa Afya 240 kwenye Wilaya zetu na Halmashauri zote. Kwa mafunzo ya leo tunatarajia kuwafikia wataalamu wa Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Jamii zaidi ya 185” amesema.
Amewaomba pia wadau wote kuelekeza nguvu zao kushirikiana na Serikali katika kufanikisha ukarabati wa kituo cha dharura Mkoani Arusha pamoja na kuwezesha upatikanaji wa vifaa vya kujikinga.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii, Idara kuu ya Maendeleo ya Jamii Patrick Golwike ametoa wito kwa Maafisa hao ili kuepusha msongamano watumie Redio za Jamii zilizopo kwenye maeneo yao kuelimisha jamii.
“Baadhi ya Halmashauri zina Televisheni zao pamoja na Redio za kijamii. Vyombo hivi vikitumika vizuri kwenye kusambaza elimu ya kujikinga na virusi vya Corona ili kuepuka msongamano, zitakuwa ni sehemu mojawapo ya kusaidia kufikisha ujumbe” amesema.
Akitoa mada kwa washiriki hao, Dkt. Meshack Chinyuli kutoka Wizara ya Afya, kitengo cha Elimu kwa Umma amewasisitiza kutumia takwimu sahihi zinazotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na hapa nchini ni Wizara ya Afya.
Awali akitoa lengo la mafunzo hayo kwa washiriki, Afisa Ustawi wa Jamii Mkuu kutoka Wizara ya Afya, Idara ya Maendeleo ya Jamii Zakia Mohamed amesema kuwa mafunzo hayo yatawajengea uelewa wa kufahamu njia za maambukizi, dalili zake na inapotokea mtu amepata dalili ni wajibu wa maafisa hao kuelekeza wapi pa kwenda kupata huduma.
Akishukuru kwa niaba ya washiriki, Afisa maendeleo ya Jamii Mkoa Bi. Blandina Mkini amewahimiza Maafisa hao kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha kuwa Mkoa wa kwanza kuundoa ugonjwa huo hapa nchini.
“Sasa tutakuwa kifua mbele kwa sababu tuna tuna uwezo wa kumueleza mwananchi kuhusu ugonjwa huu na kukanusha upotoshaji” amesema.
Mgonjwa wa kwanza kuripotiwa nchini alitokea Mkoa wa Arusha hapo tarehe 16 Machi, 2020 ambaye amepona na hadi sasa wagonjwa waliothibitishwa ni 13.
APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA
0 Comments