MGONJWA MWINGINE WA CORONA AONGEZEKA, NI DEREVA WA LORI, SASA WAFIKIA 13 | ZamotoHabari.

 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akizungumza na wandishi wa habari leo jijini Dodoma, alipokua akitangaza mgonjwa mpya wa ugonjwa wa Corona nchini. Kulia ni Waziri wa Afya wa Zanzibar, Hamad Rashid.
Waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Hamad Rashid akizungumza na wandishi wa habari jijini Dodoma leo katika mkutano wa pamoja na Waziri Ummy kuhusiana na idadi mpya ya wagonjwa wa Corona.

Charles James, Globu ya Jamii
IDADI ya wagonjwa wenye maambukizi ya virusi vya Corona imeongezeka kutoka watu 12 hadi watu 13 huku Mkoa wa Dar es Salaam ukiendelea kuwa na idadi ya wagonjwa wengi kulinganisha na mikoa mingine yenye maambukizi.

Mgonjwa wa 13 ambaye ameongezeka kutoka idadi ya watu 12 ya awali amepatikana Mkoani Kagera ambapo ni Dereva wa Lori ambaye aliingia nchini akitokea nchi jirani ya Burundi.

Akizungumza na wandishi wa habari leo jijini Dodoma, Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema kati ya wagonjwa hao 13, Dar es Salaam inaongoza ikiwa na wagonjwa nane, Arusha wawili, Zanzibar wawili na Kagera ikiwa na magonjwa mmoja.

Ummy amesema Wizara imeendelea kutoa huduma za upimaji sampuli za washukiwa wa ugonjwa huo wa Corona katika maabara kuu ya Taifa ya Afya ya Jamii ambapo hadi kufikia leo jumla ya watu 273, Tanzania bara 242 na Zanzibar 30 walichukuliwa sampuli za kupima virusi hivyo.

Amesema kuanzia Machi 23 mwaka huu abiria wote wanaowasili nchini kutokea nchi zilizoathirika zaidi na virusi hivyo wanawekwa kwenye karantini ya lazima ya siku 14 katika Hoteli, maeneo maalum yaliyobainishwa na serikali kwa gharama zao.

" Tangu kuanza kutekeleza agizo la  Rais jumla ya wasafiri 111 wametengwa kwenye maeneo maalum yaliyoandaliwa, Mikoa yote nchini imeelekezwa kuendelea na zoezi la kubainisha maeneo yatakayotumika kuwaweka wasafiri pamoja na kuweka utaratibu mzuri wa kutekeleza maelekezo haya bila kusumbua wasafiri.

Wagonjwa hawa 13 nane kati yao ni raia wazawa na watano wakiwa wageni. Wagonjwa wote isipokua mmoja walisafiri nje ya Nchi katika siku 14 zilizopita kabla ya kuthibitishwa kuugua na huyu mmoja alipata maambukizi kutoka kwa mtu aliyetoka nje ya Nchi," Amesema Ummy.

Amebainisha kuwa mgonjwa wa kwanza, Isabella kutoka Arusha tayari ameshapona ugonjwa huo baada ya kufanyiwa vipimo mara tatu na kukutwa akiwa mzima bila maambuzi na kilichopo ni kumruhusu kurejea nyumbani baada ya kupona.

Akizungumzia kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ya kumtangaza mmoja wa wagonjwa ambaye ni Mtoto wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), Freeman Mbowe, Waziri Ummy amesema watanzania wanapaswa kuziamini taarifa zinazotolewa na Waziri Mkuu, Wizara yake na Msemaji Mkuu wa Serikali kama ambavyo Rais Magufuli alielekeza.

" Sisi kama wizara tunazingatia sheria na miiko yetu kwa kutomtangaza mgonjwa yoyote, ukiangalia kuanzia Isabella, Mwana FA na Sallam SK hawa waliamua wenyewe kujitangaza, kama Wizara hatutomtangaza mgonjwa yoyote na tunaomba watanzania waamini taarifa zinazotolewa na mamlaka zilizoelekezwa na Mhe Rais," Amesema Waziri Ummy.

Amesema pamoja na hayo wizara inaendelea na jukumu lake la kutoa huduma za Afya kwa watu ambao wamepatwa na maambukizi ya ugonjwa ikiwa ni jitihada za serikali katika kuzuia maambukizi mapya.

Kwa upande wake Waziri wa Afya wa Zanzibar, Hamad Rashid amesema katika kuchukua tahadhari ya ugonjwa huo wazanzibar waliopo nje ya Nchi hawatoruhusiwa kuingia visiwani humo kuanzia Jumamosi.

" Kama kuna Mzanzibar yupo nje ya Nchi na anataka kurudi basi arudi kabla ya siku ya Jumamosi kinyume na hapo hatutoruhusu mtu kuingia nchini mwetu," Amesema Hamad Rashid


APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini