MKURUGENZI MAKAMBAKO KUTOA MOTISHA KWA WALIMU WATAKAOFAULISHA WANAFUNZI KATIKA MASOMO YAO | ZamotoHabari.

Na Shukrani Kawogo, Njombe.

Mkurugezi wa halmashauri ya mji Makambako mkoani Njombe, Paulo Malala ametoa motisha kwa walimu watakaoweza kufaulisha wanafunzi katika masomo yao kwa kupata alama A ambapo watapata posho ya shilingi elfu hamsini kwa kila mwanafunzi atakayepata alama hiyo katika somo lake.

Mkurugenzi aliyasema hayo Hayo katika kikao cha tathimini ya elimu ya halmashauri hiyo na kusema kuwa motisha hiyo ni chachu kwa walimu kwani itawapelekea kufanya juhudi katika kufundisha ili wanafunzi waweze kufaulu vizuri katika masomo yao.

Aliongeza kuwa suala hili fedha hizi zitawasaidia walimu hao katika kujikwamua kiuchumi kwakuwa anapofaulisha wanafunzi wengi kwa alama hiyo ndivyo kiwango cha posho kinavyoongezeka.

“Walimu mnapaswa kuchangamkia motisha hii maana endapo utajitahidi ukafaulisha wanafunzi 10 kwa alama A utajinyakulia kiasi cha shilingi laki tano ambayo itakusaidia katika mambo yako”, Alisema Malala.

Alisema endapo walimu watajitoa na kufanya juhudi katika kufundisha itasaidia kuinua kiwango cha elimu na ufaulu kuongezeka zaidi.

Aidha mwenyekiti wa halmashauri ya mji makambako Hanana Mfikwa amesema posho hizo zinazotolewa na mkurugenzi hazijaidhinishwa na baraza la madiwani hivyo ni msukumo wake yeye ambao ameupata ili kuinua kiwango cha elimu.

Alisema uamuzi huo unaonyesha ni jinsi gani mkurugenzi alivyo na uchungu wa kukua kwa elimu katika halmashauri yake hivyo walimu wanapaswa kumuunga mkono na kuhakikisha kuwa wanafunzi wanafanya vizuri.

Katika hatua nyingine mkuu wa wilaya ya Njombe, Ruth Msafiri ambaye ndiye aliyekuwa mwenyekiti wa kikao hicho aliwapa onyo baadhi ya walimu wanaotoa lugha chafu na ubaguzi juu ya walimu wageni wanaopangia katika shule za wilaya hiyo.

Alisema baadhi ya walimu wamekuwa wakiwatenga na kuwasema wenzao vibaya waajiriwa wageni kutoka maeneo mbalimbali na kutowaonyesha ushirikiano wa kutosha kitu ambacho kinarudisha nyuma maendeleo ya elimu. 
 


APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini