WAJUMBE WA BODI YA TRA WAIPONGEZA ITA | ZamotoHabari.

CHUO cha Kodi (ITA) kimeshauriwa kupanua wigo wa kutoa mafunzo ya utawala na uongozi katika taasisi na mashirika pamoja na wadau wengine ili wananchi wengi waipate elimu hiyo ambayo ni muhimu kwa viongozi.


Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Dr. Suleiman Missango wakati akifunga mafunzo ya uongozi na utawala kwa wajumbe na wakuu wa idara za TRA ambayo yaliyotolewa na Chuo cha Kodi na kufanyika jijini Dododma kwa siku tatu.

“Tumekuwa tukileta wataalam kutoka nje kutoa mafunzo kama haya, lakini ITA imeonyesha uwezo mkubwa wa kutoa mafunzo hivyo kutokana na umuhimu wa mafunzo haya ni vema rasilimali na muda ukiruhusu yaeolewa pia kwa taasisi nyingine za serikali, binafsi pamoja na mashirika ili kupanua wigo wa uelewa”, alisisitiza Dr. Missango.

Dr. Missango amekiri kwamba inapendeza kutambua kuwa Chuo cha Kodi kina wataalam waliobobea katika kutoa mafunzo ya uongozi na utawala ambayo ni nyenzo muhimu kwa viongozi kutimiza wajibu wao na kufanikisha malengo ya taasisi wanazoziongoza.

Amesema kwamba kama bodi wataangalia maeneo ambayo yanawahitahi kubadilika na kuyafanyia kazi na kwa menejimenti ya TRA mafunzo hayo yawe kichocheo cha kujiendeleza zaidi.

Mwenyekiti huyo wa Bodi amewataka washiriki wa mafunzo hayo kutekeleza kwa vitendo yale yote waliyojifunza ili yajidhihirishe katika utendaji wa kazi zao. “Elimu tuliyoipata iboreshe utendaji wa kazi zetu”, alisisitza.

Naye mjumbe wa bodi ambaye alishiriki mafunzo hayo Dr. Eliab Luvada amesema kwamba mafunzo hayo sio tu kwamba yatamsadia katika kutekeleza majukumu ya bodi bali pia yatamsadia katika shughuli zake nyingine za kila siku. Amesema kwamba sasa dhana ya Chuo kutambulika kuwa kituo cha umahiri katika mafunzo ya forodha na kodi Afrika masharika inajidhihirisha.

Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Dkt. Edwin Mhede aliwashukuru wajumbe wa bodi kwa kukubali kuhudhuria mafunzo hayo na kuongeza kwamba kujifunza ni zoezi endelevu na umuhimu wa mafunzo hayo sio kwa TRA tu bali ni wa taifa kwa ujumla.

Akizungumzia mafunzo hayo Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi Richard Kayombo amekipongeza Chuo kwa ubora wa mafunzo na kusema kwamba wameongeza maarifa katika utekelezaji wa majukumu yao kama menejimenti ya TRA.

Mafunzo hayo ya siku tatu yalitolewa na Chuo cha Kodi kwa Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania na Menejimenti ya TRA.

Pamoja na mada nyingine, mafunzo hayo yalihusu misingi ya utawala bora katika taasisi za kodi, hatua za uongozi na falsafa za uongozi.

Chuo cha Kodi ni sehemu ya Mamlaka ya Mapato Tanzani ambacho hutoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu kwa watumishi wa TRA na wadau wengine ili kuwajengea uwezo katika kutekeleza majukumu yao. Pia Chuo hicho kinaithbati ya kudumu kutoa mafunzo ya muda mrefu katika taaluma ya forodha na kodi kuanzia ngazi ya cheti hadi Shahada ya Uzamili.Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Dr. Suleiman Missango (wa sita mbele) katika picha ya pamoja na wajumbe wa Bodi na Wakuu wa Idara za TRA mara baada ya kufungua mafunzo ya uongozi na utawala. Kushoto kwake ni Kamishna Mkuu wa TRA Dkt Edwin Mhede.

 Baadhi ya Wakuu wa Idara wa TRA katika majadiliano wakati wa mafunzo.
 Mwenyekiti wa Bodi na wajumbe wengine wa Bodi katika majadiliano wakati wa mafunzo.
 Mkuu wa Chuo cha Kodi Prof. Isaya Jairo (kushoto) akimkabidhi Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TRA Dr. Suleiman Missango Cheti cha ushiriki wa mafunzo.
Mkuu wa Chuo cha Kodi Prof Isaya Jairo akimkabidhi Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TRA Dr. Eliab Luvanda cheti cha ushiriki wa mafunzo.
Mkuu wa Chuo cha Kodi Prof Isaya Jairo akimkabidhi Naibu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa TRA, Bi. Alice Lukindo cheti cha ushiriki wa mafunzo.


APP YETU MPYA: Sasa unaweza kusoma kwa urahisi kupitia APP yetu. Download hapa kwa KUBOFYA HAPA

Post a Comment

0 Comments

close
Banner iklan disini